METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, October 17, 2017

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI, ATEMBELEA UJENZI NYUMBA ZA POLISI, JIJINI ARUSHA

____________________
Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Mwigulu Nchemba leo Jumanne Oktoba 17,2017 mchana ametembelea, Jijini Arusha, na kujionea maendeleo ya Ujenzi wa Nyumba za Polisi zinazoendelea kujengwa, baada ya ajali ya moto iliyotokea mwishoni mwa mwezi Septemba, ambayo ilisababisha familia za Askari 13 kuunguliwa vitu mbalimbali na kukosa makazi.

Mhe. Mwigulu Nchemba, alitumia fursa hiyo kwa kuishukuru kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa ambayo inaoongozwa na Mkuu wa Mkoa Mhe. Mrisho Gambo, lakini pia aliwashukuru wadau ambao wote kwa pamoja walichukua hatua za haraka za kurejesha makazi ya askari ambao walikumbwa na janga la moto huku akisisitiza kwa kusema kwamba hali ilioonyeshwa na wadau hao ni mfano mzuri wa kuigwa na mikoa mingine waone nchi inajengwa na wananchi.

Alisema kwamba suala la makazi ya askari lipo katika kipaumbele cha Serikali ya Jamhuri ya Muugano wa Tanzania, na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameonyesha kwa vitendo katika maeneo tofauti ikiwemo hapa Arusha.

Alisema Serikali ikishamaliza hilo itaendelea na utaratibu mwingine wa kujenga majengo ya kisasa ili askari wapate makazi bora huku akimuagiza Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha awafikishie salamu askari wa Arusha kwamba, Mhe. Rais yupo pamoja nao na Wizara ipo pamoja nao.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo mbali na kuendelea kuwashukuru wadau hao kwa kujitolea na kumuunga mkono Mhe. Rais ambaye alionyesha njia siku hiyo hiyo usiku kabla hakujapambazuka kwa kutoa mchango wake kama Serikali ya Jamhuri ya Muugano wa Tanzania, lakini pia alisema bado milango ipo wazi kwa watu wengine ambao hawakuwa na taarifa juu ya tukio hilo ili kulisaidia Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha liweze kufanikisha ujenzi wa makazi ya askari hao.

Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo aliongeza kwa kusema ujenzi wa makazi bora ya askari mkoani hapa utasaidia kuwaongezea morali zaidi wa kazi askari hao hali ambayo itazidi kuimarisha usalama na shughuli za maendeleo kusonga mbele.

Jumla ya nyumba 29 za askari katika moja ya kambi iliyoathirika na ajali ya moto zilianzwa kujengwa toka tarehe 2 mwezi huu jijini hapa na saba ambazo zipo katika ngazi ya msingi zinatarajiwa kujengwa katika kituo kidogo cha Polisi Morombo kata ya Murieti.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com