METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, October 17, 2017

DKT. NDUGULILE AFANYA ZIARA KUJIRIDHISHA NA HALI YA UPATIKANAJI WA DAWA

NA WAMJW-DAR ES SALAAM

Naibu Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amefanya ziara kwenye baadhi ya vituo vitoavyo huduma za afya kwa ajili ya kujiridhisha na hali ya upatikanaji wa dawa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza lengo la ziara hiyo Dkt. Ndugulile amesema kuwa ameamua kufanya hivyo ili kusimamia maagizo ya  Rais wa awamu ya tano Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ya kutatua tatizo la dawa katika vituo vinavyotoa huduma za afya mpaka kufikia 2020.

“Mpaka kufikia hivi sasa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetenga shilingi Bilioni 262 kwa ajili ya kutatua tatizo la uhaba wa dawa nchini kutoka shilingi bilioni 31 katika mwaka wa fedha 2015/2016 “ alifafanua Dkt. Ndugulile.

Aidha Dkt. Ndugulile amesema kuwa katika ziara hiyo amegundua kwamba vituo vinavyotoa huduma ya afya vina dawa zote muhimu isipokuwa kuna upungufu wa vifaa tiba ambapo tatizo hilo litafanyiwa kazi mara moja .

Mbali na hayo Dkt. Ndugulile aliwataka waganga wakuu na Wafamasia wa vituo vinavyotoa huduma za Afya kuboresha upokeaji, utunzaji wa dawa pindi zinapoingia  kwenye stoo zao na usimamizi mzuri wa dawa hizo.

“Vituo vinavyotoa huduma za afya lazima ziwe na kamati za afya ambazo zitashiriki katika kupokea dawa pindi zinapotoka MSD badala ya kupokelewa na mtu mmoja aidha mfamasia au mtumishi mwingine wa kitengo cha dawa” alisema Dkt. Ndugulile.

Dkt. Ndugulile leo amefanya ziara yake ya kutaka kujiridhisha na  hali ya upatikanaji wa dawa katika Hospitali ya Mwananyamala, Hospitali ya Sinza na Zahanati ya Mwenge za jijini Dar es salaam.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com