Rais John Magufuli
By Kelvin Matandiko, Mwananchi
Dar es Salaam. Rais John Magufuli, ametoa onyo kwa wakurugenzi wanne wa halmashauri nchini walioanza kujihusisha na matumizi ya kilevi, akiwataka waache mara moja na ikiwezekana waokoke.
Rais Magufuli ambaye hakuwataja
wakurugenzi hao, amesema wapo na tayari taarifa zao ameshazipata hivyo
waache tabia hizo na badala yake wajikite kuwatumikia wananchi.
Tabia
ya ulevi imeonekana kuwa ni dosari kubwa kwa wateule wake, baada ya
kutengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles
Kitwangwa mwaka jana kutokana na ulevi.
Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Kitwanga baada ya kuingia bungeni kujibu swali linalohusu wizara hiyo akiwa amelewa.
“Nimesikia
kuna wakurugenzi watatu, wanne waache mara moja na ikiwezekana waokoke
kabisa,” ameonya Rais Magufuli wakati wa kufungua Mkutano Mkuu wa 33 wa
Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (Alat) unaofanyika Dar es Salaam leo
na kesho Jumatano.
Katika mkutano huo uliowakutanisha
mameya kutoka mikoa yote nchini, mwenyekiti wa jumuiya hiyo Gulamhafeez
Mukadam aliwasilisha changamoto kadhaa ikiwamo hali ngumu ya madiwani
hivyo waongezewe posho kutoka Sh350, 000 hadi Sh800,000, ombi ambalo
lilikataliwa na Rais Magufuli.
Hata hivyo, Rais
Magufuli ameeleza umuhimu wa Alat katika utekelezaji wa Ilani na
mikakati yake kwa Watanzania, kubaliana na kuahidi kushughulikia
changamoto za uhaba wa watumishi katika halmashauri na ucheleweshwaji na
uhaba wa ruzuku za miradi ya maendeleo.
Akijibu
mapendekezo hayo, amesema Serikali licha ya kutoajiri mwaka jana, tayari
imeshatangaza ajira mpya 52,000 zitakazojaza nafasi zilizoachwa wazi na
watumishi hewa zaidi ya 20,000 pamoja na walioondolewa kwa vyeti feki
12,000.
Katika hotuba hiyo, Rais Magufuli alitumia
zaidi ya saa mbili kueleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha
miezi 23 ya uongozi wake, kueleza miradi mipya ya Serikali, dhamira yake
katika kudhibiti mitandao ya ufisadi huku akiwataka Watanzania
kuvumilia katika mabadiliko aliyoanzisha.
0 comments:
Post a Comment