Geita. Ukistaajabu ya Musa utaona ya firauni, ndivyo unavyoweza kusema baada ya watu wasiofahamika kumfunga kuku kitambaa cheupe mithili ya sanda na kumweka nyumbani kwa Emanuel Kabodi, mkazi wa Mtaa wa 14 Kambarage mjini Geita.
Tukio hilo lililovuta watu wengi limetokea leo Jumanne saa 11:00 alfajiri.
Mama
wa familia hiyo, Scholastica Nicodemus alipoamka kuanza shughuli za
siku alishangaa kumkuta kuku huyo nje ya nyumba yake huku geti likiwa
limefungwa.
Akizungumza nyumbani kwake, Nicodemus
amesema ni kawaida yake kuamka alfajiri kwa ajili ya shughuli za
nyumbani ili baadaye aweze kwenda kwenye biashara zake sokoni.
“Nilivyotoka
nje nilikuta kitu kimefungwa na kitambaa cheupe, nilirudi ndani
nikamwita mume wangu aje aone. Alitoka kwa hofu nikamwambia asiogope kwa
kuwa ameokoka,” amesema.
Nicodemus amesema alimuita
mchungaji ambaye baada ya kufungua kitambaa walikuta kuku mweusi akiwa
amepitishwa kwenye moto akiwa amefungwa kitambaa cheupe.
Amesema
tukio hilo wanalihusisha na ajali iliyotokea juzi Jumapili na mume wake
kunusurika kifo baada ya gari lake kuacha njia na kupinduka.
“Kuna
mambo ya ajabu, juzi alipata ajali ambayo hata haieleweki. Si mara ya
kwanza huwa anakuta chura ndani ya gari kwenye mazingira yasiyoeleweka
ila sisi tunamuamini Mungu wala hatuogopi,” amesema Nicodemus.
Askofu wa Kanisa la Pentekoste (TMRC), Stefano Sagada amesema tukio hilo la kuku linaonyesha jinsi watu walivyo na imani haba.
Amewataka wananchi waache kuamini ushirikina na badala yake wamtegemee Mungu.
“Mungu
yupo na yeye ndiye zaidi ya kila jambo. Watawatisha kwa vitu vya aina
nyingi lakini mkimtazama Mungu yote yatawezekana na adui zenu
hawatafanikiwa,” amesema Askofu Sagada.
Mjumbe
wa Serikali ya Mtaa wa 14 Kambarage, Justa Fungameza amesema yamekuwepo
matukio ya ajabu mtaani hapo yanayohusishwa na ushirikina.
Amesema
kwa mwaka huu, tukio hilo ni la tatu baada ya mawili yakihusisha mtoto
anayedaiwa kufufuka na mwingine mchanga aliyezikwa kufukuliwa na mwili
kukutwa kwenye boksi pembeni mwa kaburi.
Mjumbe
mwingine, Stefano Mayovu amesema kinachosababisha mambo hayo ni chuki
binafsi, wivu na wananchi kutoamini Mungu na badala yake kuamini
ushirikina.
0 comments:
Post a Comment