Takriban mita 700 kusini mwa barabara ya
Nachingwea-Liwale pembezoni mwa kisima kifupi cha wazi katika Kijiji cha
Lionja B, Severine Conrad (16) anakunywa maji kwa kutumia kidumu kidogo
cha lita tatu kilichokatwa mdomoni.
Maji anayokunywa
Conrad, anayesoma kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Lionja
wilayani Nachingwea mkoani Lindi, yanatoka katika kisima hicho kifupi
cha udongo kilichochimbwa kwenye shamba la miwa ambalo huwa ni eneo oevu
wakati wa masika.
“Siwezi kuhofia kuumwa kwa kunywa
maji haya hata kama ni machafu kwa kuwa nimeyazoea. Haya maji ndiyo
tunayokunywa kila siku na hakuna mengine,” anasema Conrad licha ya
kukiri kufundishwa shuleni umuhimu wa kuchemsha maji.
Conrad
siyo mkazi pekee wa eneo hili anayekunywa maji machafu bila ya
kuyatibu. Wananchi wengi wanakunywa maji hayo kutokana na uhaba wa
vyanzo vya maji safi na salama jambo linalowaweka katika hatari ya
kushambuliwa na magonjwa ya tumbo mara kwa mara na kudhorotesha afya
zao.
Katika vijiji vya Lionja A, Lionja B,
Litandamtama, Nangunde, Namikango A na Namikango B vyanzo vyote vya maji
si safi na salama kasoro kisima kimoja tu cha pampu ya mkono.
Kisima
hicho cha pampu nacho kimejengwa Juni mwaka huu katika Kitongoji cha
Mayaka katika Kijiji cha Lionja A na asasi ya kiraia ya GAIN ambacho
tayari kimeanza kuzidiwa na msongamano wa watu kwa kuwa hakina maji ya
chumvi kama vingine.
Kisima hicho kinahudumia watu
zaidi ya 3,200 wa kijiji hicho, kiwango ambacho ni kikubwa mara 12 ya
utaratibu uliopangwa na Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002 inayoagiza
kituo kimoja cha maji kuhudumie wastani wa watu 250.
Visima
vingi katika vijiji hivi ni vya udongo vilivyowazi na vingi havizidi
urefu wa kati ya futi sita hadi 10. Sehemu kubwa vimezungukwa na vichaka
na vipo mbali na makazi huku baadhi wakilazimika kusafiri zaidi ya
kilomita tano kufuata maji katika visima hivyo.
Ndani
ya visima hivyo kama cha Kwa Bakari Libea katika Kijiji cha Litandamtama
kuna takataka zimetumbukia, vyura wanaogelea na kukimbia pale mtu
anapoingiza kopo la kuchotea maji. Maji yamebadilika na kuwa rangi ya
kutu.
“Unashangaa takataka za miti na fimbo, kuna
wakati wanafia panya humu ndani na tunachota tu. Hata kama tukihofia
kuathirika tutaenda kuchota maji wapi ambako siyo mbali na nyumbani?”
anasema Asia Ibu, mkazi wa Kijiji cha Litandamtama.
Ni
Kijiji cha Lionja A pekee kilichobahatika kuwa na visima vifupi 12
vilivyojengwa na saruji bila kufunikwa ambavyo maji yake ni ya chumvi na
Lionja B chenye kisima kimoja kilichojengewa na saruji.
Utaratibu
uliopo ni kwamba kila mchotaji anakuja na kichoteo chake chenye kamba
ndefu anachokitumbukiza kisimani ili mradi awahi kupata huduma hiyo
muhimu kwa mwanadamu.
Sehemu kubwa ya wachota maji
katika kisima maarufu cha Chengo wanavifaa kukuu kama vibuyu na vidumu
vya lita tano vilivyokatwa midomoni ili vichote maji kwa wingi. Ni
wachache wanavifaa vya kisasa kama ndoo mpya za plastiki za lita 10.
Kisima
cha Chengo kilichopo Lionja A wakati wa kiangazi kuanzia Septemba hadi
Desemba kwa mujibu wa diwani wa Lionja, Joachim Mnungu kinahudumia
vijiji vya kata tatu vikiwemo Litandamtama, Lionja B, Namikango A,
Namikango B, Nangunde, Nalengwe na Naulingo kwa kuwa kinadumu misimu
yote na kina maji yenye chumvi kidogo kuliko vingine.
“Kupata
maji ya kunywa ni shida. Kuna kipindi cha kiangazi tunatoka asubuhi
kwenda Chengo au mabondeni na kurudi jioni kutokana na foleni ya
wachotaji,” anasema Calcansia Tindwa anayeishi katika Kijiji cha Lionja
B.
Ili afike katika Kisima cha Chengo kutoka nyumbani kwake, Calcansia analazimika kutembea umbali wa takriban kilomita nne.
Pamoja
na kwamba maji hayo si salama, Calcansia aliyekutwa akichota maji
kisimani akiwa na mwanaye wa miezi mitatu, anasema maji hayo huwanywesha
pia watoto wao wadogo bila kuchemsha au kutia dawa za kutakatisha.
Wananchi
hao wanapata shida ya maji licha ya lengo namba 4.4 la Sera ya Taifa ya
Maji ya mwaka 2002 kutaka wakazi wa vijijini wapate angalau lita 25 za
maji safi na salama kwa mtu mmoja kwa siku na ndani ya mita 400 yalipo
makazi yao.
Uelewa duni wa kutibu maji
Hata
pamoja na kwamba maji hayo yanaweza kutibiwa kuua vijidudu
vinavyosababisha magonjwa ya tumbo, sehemu kubwa ya wakazi hao
hawachemshi wala kutakatisha maji na dawa kama ‘Waterguard’.
“Tanakunywa
tu hivyo hivyo bila ya kuchemsha. Hakuna mtu hapa mwenye utaalamu huo
wa kuchemsha maji ya kunywa,” anasema Abas Mussa (78).
Hata
hivyo, wapo wanaojua umuhimu wa kuchemsha maji hususan akina mama ambao
hupatiwa elimu hiyo kliniki kama Calcansia, lakini hawachemshi kwa kile
wanachodai ni ‘utamaduni’ wao.
“Huu ni utamaduni wetu
kunywa maji bila kuchemsha na sisi tumekuta kwa wazee wakifanya hivyo
tangu zamani na wote tunatumia maji hayo hayo,” anasema Calcansia.
Ukiachana
na ukosefu wa elimu ya kuchemsha maji, bado upatikanaji wa dawa za
kusafisha maji katika vijiji hivi ni shida. Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa hakuna duka linalouza dawa hizo wala zahanati ambayo inawapatia bure.
Madhara ya maji machafu
Matumizi
ya maji yasiyo safi na salama yanawagharimu wakazi wa vijiji hivyo
kiasi cha baadhi yao kukumbwa na magonjwa ya kuhara mara kwa mara na
kusababisha baadhi wasifanye shughuli zao za uzalishaji.
Mkazi
wa Kijiji cha Lionja A, Fabiola Nnali (48) anasema ni kawaida kwa
familia yao kukumbwa na magonjwa ya kuharisha na wakienda zahanati au
hospitali madaktari huwa wanawaambia hali inatokana na kunywa maji
machafu.
“Kuharisha siyo jambo geni, mwaka jana
niliumwa sana ugonjwa wa kuhara damu ilibidi nienda hospitali Mnero
kutibiwa. Kwa shida hizi tunaomba Serikali itusaidie kutujengea visima
vizuri angalau tupate maji safi na salama,” anasema Fabiola.
Siyo
wote wanaoumwa kama Fabiola wanaenda kutibiwa hospitali. Baadhi kama
Fatuma Ismail (75) huwa anatumia mitishamba au kununua dawa katika
maduka ya dawa muhimu kujitibu.
Muuguzi wa Zahanati ya
Lionja, Rehema Salumu anasema ni nadra kupokea watu wazima wanaoumwa
magonjwa ya tumbo kwa kuwa baadhi huenda moja kwa moja kwenye hospitali
ya misheni ya Mnero iliyopo kilomita zaidi ya 10 kutoka kijiji hapo.
“Watoto
wa chini ya miaka mitano wanaoharisha ni wengi ambao kwa mwezi unaweza
kupata sita na mkubwa mmoja tu. Hata hao watoto muda mwingine siyo kwa
sababu ya maji machafu,” anasema Salumu.
Ugonjwa wa kuhara
Takwimu
kutoka hospitali ya Mnero zinabainisha kuwa mwaka jana ugonjwa wa
kuhara ulikuwa ni wa tatu kwa kuwa na wagonjwa waliolazwa wenye miaka
zaidi ya miaka mitano, nyuma ya Malaria na magonjwa ya upumuaji, ukiwa
na wagonjwa 109 kati ya 1,203 waliorekodiwa.
Kwa
wagonjwa wasiolazwa wenye miaka zaidi ya miaka mitano, ugonjwa wa kuhara
ulikuwa ni wa nne baada ya Malaria, homa ya mapafu na maambukizi ya
njia ya mkojo (UTI).
Uhaba wa maji safi na salama
vijijini unaikabili sehemu kubwa ya Halmashauri ya Nachingwea baada ya
takwimu za Mkoa wa Lindi za hadi Juni mwaka huu kubainisha kuwa ni
wakazi 45 tu kwa kila 100 wanaopata maji safi na salama ikilinganishwa
na wastani wa kitaifa wa watu 72 kwa kila 100.
Uhaba
huo umechangia wananchi wa wilaya hiyo kukabiliwa na magonjwa ya tumbo
kama ilivyo katika vijiji vingi vya kata za Namikango na Lionja.
Takwimu
kutoka ofisi ya Mganga Mkuu wa wilaya hiyo zinabainisha kuwa katika
robo ya kwanza ya mwaka 2017 ugonjwa wa kuhara ulikuwa ni wa tatu nyuma
ya Malaria na maambukizi ya njia ya mkojo (UTI), ukiwa na wagonjwa 3,028
waliobainika kuharisha huku zaidi robo wakiishiwa maji.
Wataalamu
wa afya wanasema magonjwa ya tumbo kikiwemo kipindupindu yataepukika
kwa uwepo wa maji safi na salama wakati wote na watu kusafisha mazingira
yao ikiwemo kunawa mikono wanapotoka msalani.
“Wakati
wa mvua wagonjwa ni wengi sana lakini wakati wa kiangazi wanapungua.
Kuna wakati unakuta wodi nne wagonjwa wengi ni wa magonjwa ya kuharisha
tu…na huenda hata takwimu zetu hizi ni ndogo kuliko uhalisia,” anasema
Dk Leonard Shitanda, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Misheni ya Mnero.
Anasema
magonjwa yanawapotezea watu muda mwingi wa kufanya kazi zao ndiyo maana
huwa wanawapa elimu ya kutibu maji ili waepukane na magonjwa hayo
ambayo yanaepukika kwa kufuata kanuni za usafi.
“Ila
hakuna suluhu ya kudumu kama Serikali kusambaza maji safi na salama kwa
vijiji vyote. Asasi za kiraia zenye uwezo ziangalie namna ya kusambaza
dawa za kutibu maji kama Waterguard kama ilivyokuwa zamani ili
kuwasaidia wananchi,” anasema.
Alipoulizwa wanatatua
vipi wimbi la ugonjwa wa matumbo yanayotokana na maji machafu, Kaimu
Mganga Mkuu wa halmashauri hiyo, Godfrey Mjungu anasema njia endelevu
wanayotumia ni kutoa elimu ya kutibu maji kupitia kampeni ya usafi wa
mazingira katika vijiji vyote 127.
“Huwa tunakusanya
taarifa kila mwezi kujua kama elimu imefanya kazi na ni njia hii
iliyosababisha kupunguza kesi za magonjwa ya tumbo japo bado yapo
kidogo. Jambo kubwa ni kubadili tabia za wananchi wawe wasafi kwa kuwa
wakati mwingine unakuta maji safi na salama yapo na bado wanaugua
matumbo,” anasema Mjungu.
Ofisi ya mkurugenzi
Kaimu
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Arbogast Kiwale anakiri kuwepo kwa
uhaba wa maji vijijini kuliko mijini akieleza kuwa hadi sasa asilimia 71
ya wakazi Nachingwea wanapata maji ikilinganishwa na asilimia 45 ya
waishio vijijini.
“Kuna juhudi nyingi zinafanywa
kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama ila miradi
inatekelezwa kwa awamu. Tatizo kubwa ni kwamba vyanzo vikuu vya maji ni
ardhini kwa kuwa hakuna mito ya kudumu kwa sababu mnaweza kuchimba
visima mnakuta vyote maji hayafai kwa binadamu,” anasema.
Anasema
mapema mwaka huu halmashauri kwa kushirikiana na kampuni ya utafiti wa
madini walijenga kwa saruji visima vifupi 10 katika vijiji vya Lionja A
na B na ndani ya miezi mitatu wataenda kuvifunika na kufunga pampu za
maji ili kuvisitili na uchafu.
Kiwale anaeleza kuwa
zimeshatengwa Sh585.6 milioni kwa ajili ya maji katika mwaka 2017/18 na
baadhi ya maeneo yatakayonufaika ni Mituguru, Mitigera na Lupondera.
“Wakati
tukiendelea kujenga visima na mabwawa kwenye baadhi ya vijiji vyenye
shida ya maji safi na salama, tunawasihi wananchi kuvuna maji ya mvua
wayatunze na wawe wanayechemsha ili kuepuka magonjwa ya tumbo,” anasema.
Taarifa za ziada
“Utoaji
wa dawa za kutibu maji haiewezi kuwa njia endelevu kutatua magonjwa ya
matumbo. Halmashauri zinajukumu kuhamisisha wananchi kuishi katika hali
ya usafi na zimeshapewa miongozo hii na wizara ikiwemo kutoa elimu ya
kuchemsha maji,” Nsacris Mwamaja, Msemaji wa Wizara ya Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment