METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, October 27, 2017

KAMPENI YA ‘KIWANDA CHANGU, MKOA WANGU’ KUANZA MIKOANI

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi) Mhe. Selemani Jafo ameagiza mikoa yote kuanza Kampeni kabambe iitwayo ‘Kiwanda changu Mkoa wangu’ ili kuharakisha maendeleo na kuongeza upatikanaji wa ajira kwenye maeneo hayo.

Jafo ametoa maagizo hayo ya wizara yake kwa Wakuu wa mikoa yote ya Tanzania bara wakati alipokuwa akizungumza na Wakuu wa mikoa sita wapya walioapishwa leo na Rais Dk.John Magufuli.

Akizungumza na Wakuu hao baada ya kukamilisha kwa zoezi la kiapo, Jafo amesema kampeni hiyo inatarajiwa kuzinduliwa rasmi mwanzoni mwa mwezi Desemba mwaka huu.

Amesema Mpango huo kabambe ni wa kuhamasisha ujenzi wa viwanda vidogo na vya kati katika mamlaka za serikali za mitaa.

“Hii sasa ni changamoto kwenu wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya hapa nchini nataka kila mkoa ujenge angalau viwanda 100 kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Desemba 2017 hadi Desemba 2018,”anasema jafo

Amebainisha malengo yake ni kwamba ndani ya kipindi hicho cha mwaka mmoja zaidi ya viwanda vidogo na vya kati 2600 viwe vimejengwa nchini.

Katika kufanikisha mpango huo, Waziri Jafo amewataka maafisa wa maendeleo ya jamii kufanya kazi ya kuviunganisha vikundi vilivyopo katika halmashauri zao ili viweze kupata fursa za mifuko mbalimbali ya uwezeshaji iliyo chini ya Ofisi ya Waziri mkuu na fedha za uwezeshaji vijana na wanawake katika halmashauri zao.

Kampeni hiyo endapo itafanikiwa basi itakuwa ni mchango mkubwa kutoka wizara ya TAMISEMI katika ajenda ya viwanda hapa nchini.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com