METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, September 23, 2024

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo afungua Maonesho ya Teknolojia za Uhifadhi na Uongezaji Thamani Mazao ya Kilimo - Arusha

                                 

Pichani: Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, akizungumza na wakulima na wadau mbalimbali waliojitokeza katika ufunguzi wa Maonesho ya Teknolojia za Uhifadhi na Uongezaji Thamani ya Mazao ya Kilimo, Septemba 23, 2024 katika viwanja vya Makumbusho ya Taifa (Mnara wa Mwenge - Arusha)

                                 

                                     


Pichani:
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, akikagua teknolojia za uongezaji thamani ya mazao ya kilimo katika Maonesho ya Siku Mbili, akionesha dhamira ya serikali katika kuboresha uzalishaji na masoko kwa wakulima leo Septemba 23, 2024 katika viwanja vya Makumbusho ya Taifa (Mnara wa Mwenge - Arusha)

                         

                           


Pichani: Mtendaji Mkuu wa TAHA, Dkt. Jacqueline Mkindi, akizungumza katika ufunguzi wa Maonesho ya Teknolojia za Uhifadhi na Uongezaji Thamani ya Mazao ya Kilimo, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali leo Septemba 23, 2024 katika viwanja vya Makumbusho ya Taifa (Mnara wa Mwenge - Arusha)



WazoHuru Media - ARUSHA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli,  Septemba 23, 2024 katika viwanja vya Makumbusho ya Taifa (Mnara wa Mwenge - Arusha) amefungua Maonesho ya Siku Mbili ya Teknolojia za Uhifadhi na Uongezaji Thamani ya Mazao ya Kilimo baada ya mavuno, yaliyoandaliwa na Asasi Kilele ya Sekta Binafsi (TAHA) chini ya Mradi wa Feed the Future Tanzania yakilenga kuwakutanisha pamoja wadau mbalimbali katika minyororo ya thamani ya mazao ya horticulture na nafaka

Katika hafla hiyo, Bw. Mweli alisisitiza kuwa serikali imejipanga vizuri katika kumsaidia mkulima, akigusia jinsi Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeboresha bajeti ya kilimo na kuweka mazingira wezeshi kwa wakulima kupata teknolojia na masoko ya mazao yao.


Maonesho hayo yalijumuisha wadau mbalimbali kutoka katika minyororo ya thamani ya mazao ya horticulture na nafaka. Wakulima walipata fursa ya kujionea teknolojia za uvunaji, uhifadhi, usindikaji, uongezaji thamani wa mazao, na vifungashio vya kisasa, vyote vikilenga kuboresha ubora na kuongeza thamani ya mazao yao.


Wadau wa sekta hiyo walihamasishwa kuchangia mawazo na teknolojia zinazoweza kusaidia katika maendeleo ya kilimo endelevu, huku wakijadili mbinu bora za kuvutia masoko na kuongeza mapato yao. Maonesho haya yanatarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya sekta ya kilimo nchini

Mtendaji Mkuu wa TAHA, Dkt. Jacqueline Mkindi, amemshukuru Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, pamoja na serikali kwa kuendelea kusaidia upatikanaji wa teknolojia za uhifadhi na uongezaji thamani ya mazao ya kilimo. Dkt. Mkindi alisema ushirikiano huu ni muhimu katika kuimarisha sekta ya kilimo nchini na kuboresha maisha ya wakulima.

Akiwa katika maonesho, Dkt. Mkindi aliahidi kwamba TAHA itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu na serikali ili kuhakikisha malengo ya kuboresha uzalishaji na masoko yanafikiwa. Alisisitiza kwamba kwa pamoja, wanaweza kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo, hivyo kuwanufaisha wakulima na kuimarisha uchumi wa taifa

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com