WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa(Tamisemi) Mhe. Selemani Jafo ameagiza mikoa yote kuanza Kampeni kabambe
iitwayo ‘Kiwanda changu Mkoa wangu’ ili kuharakisha maendeleo na kuongeza upatikanaji
wa ajira kwenye maeneo hayo.
Jafo ametoa maagizo hayo ya wizara yake kwa Wakuu wa mikoa
yote ya Tanzania bara wakati alipokuwa akizungumza na Wakuu wa mikoa sita
wapya walioapishwa leo na Rais Dk.John Magufuli.
Akizungumza na Wakuu hao baada ya kukamilisha kwa zoezi la
kiapo, Jafo amesema kampeni hiyo inatarajiwa kuzinduliwa rasmi mwanzoni mwa
mwezi Desemba mwaka huu.
Amesema Mpango huo kabambe ni wa kuhamasisha ujenzi wa viwanda
vidogo na vya kati katika mamlaka za serikali za mitaa.
“Hii sasa ni changamoto kwenu wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya
hapa nchini nataka kila mkoa ujenge angalau viwanda 100 kwa kipindi cha mwaka
mmoja kuanzia Desemba 2017 hadi Desemba 2018,”anasema jafo
Amebainisha malengo yake ni kwamba ndani ya kipindi hicho cha
mwaka mmoja zaidi ya viwanda vidogo na vya kati 2600 viwe vimejengwa nchini.
Katika kufanikisha
mpango huo, Waziri Jafo amewataka maafisa wa maendeleo ya jamii kufanya kazi ya
kuviunganisha vikundi vilivyopo katika halmashauri zao ili viweze kupata fursa
za mifuko mbalimbali ya uwezeshaji iliyo chini ya Ofisi ya Waziri mkuu na fedha
za uwezeshaji vijana na wanawake katika halmashauri zao.
0 comments:
Post a Comment