METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, October 28, 2017

Jenga Mahusiano Bora Na Mteja ili Kukuza Biashara Yako

Habari ndugu msomaji wa makala haya na msaka mafanikio? Ni matumaini yangu makubwa u mzima wa afya tele na unaendelea na michakato yako ya kila siku. Kwa upande wangu mimi ni mzima wa afya tele, naendelea vyema na pilikapilika za kila siku ili kuhakikisha mafanikio makubwa yanakuwa upande wangu.

Nichukue fursa hii adhimu na kwa moyo mkunjufu kuweza kukukaribisha tuweze kujifunza kwa pamoja kuhusu ukuaji wa kibiashara hususani katika suala zima la mahusiano bora kati yako na mteja wako.

Kimsingi ni kwamba biashara yeyote ile ni mjumuisho kati ya mfanyabiashara na mteja. Pindi inapotokea mtafaruku kati yao, mfanyabiashara hali yake huwa ni ngumu kibiashara. Lakini kinyume chake ni kwamba pindi pawapo na mahusiano mazuri kati ya mfanyabiashara na mteja, mfanyabiashara huneemeka kutoka kwa mteja huyo.

Lakini Ukichunguza kwa umakini kati ya mfanyabiashara na mteja utagundua ya kwamba mteja huwa ni mtu wa kujishusha sana pindi akutanapo na mfanyabiashara katika suala zima la kubadilishana huduma. Hata ule usemi usemao mteja ni mfalme hukaa kushoto kwa wakati huo.

Ndio maana mteja akienda kununua kitu fulani atasema naomba kitu fulani na mwisho siku mteja huyo atatoa na hela licha ya kutanguliza neno. Lakini pamoja  hayo wapo wafanyabiashara ambao wamekuwa wakiwafukuza wateja wao bila wao wenyewe kujua.

Na kutatokea kwa hali kumesababishwa biashara nyingi kudolola huku chanzo ikiwa mfanyabiashara mwenyewe. Unakuta mfanyabiashara hata "biashara kauli" hata  siku moja, Ukichunguza kwa umakini itaniunga mkono kwa hiki  ninachosema.

Hivi hujawahi kwenda dukani ukakuta mhudumu hana muda na wewe? Achilia mbali hilo hivi hujawahi kwenda dukani kwa ajili ya kupata huduma fulani ukajibiwa vibaya?  Bila shaka hilo litakuwa si geni Kwako. Sasa tujiulize huo usemi usemao mteja ni mfalme upo wapi sasa? Bila shaka haupo.

Hivyo kwa kuwa unataka kukua kibiashara huna budi kujenga utamaduni bora na mahusiano mazuri kati yako na mteja wako. Kwani kutokuwepo kwa mahusiano mazuri ya mteja na mfanyabiashara na chanzo kikubwa cha kufa kibiashara.

Hapa ndipo ambao huwa nakumbuka mwalimu wangu wa ‘personal brand’ Charles Nduku siku moja aliwahi kuniambia ya kwamba "ukimuhudumia mteja mmoja vizuri mteja huyo anauwezo wa kukuletea wateja wapya kumi, lakini ukimuhudumia vibaya mteja mmoja anauwezo kuwapoteza wateja wapya kumi na kuwazuia wateja wengine watano uliowazoea.  Hapo sasa inakubidi uchague mwenyewe".

Hapo ndipo nikagundua ya kwamba mteja mmoja ana thamani kubwa sana katika biashara yako. Hivyo mteja mpya ambaye atakuja kwako leo kwa ajili ya kupata huduma yeyote ile, hakikisha ya kwamba humpotezi, kwani mteja huyo ana uwezo wa kuja na wateja wapya wengi endapo utamhudumia vizuri.

Haya ni baadhi ya maneno ambayo yatamfanya mteja wako ajisikie vizuri zaidi:
# Karibu sana jisikie upo nyumbani.
# Samahani sijui unahitaji/ tukuhudumie nini.
# Karibu tena kwetu mteja ni mfalme.
# Asante sana na karibu tena.
# Kwa chochote usisite kuwasiliana nasi kupitia mawasiliano yetu.

Pia kama una uwezo wa kumpa mteja wako zawadi pindi anunuapo bidhaa au huduma jaribu kufanya hivyo kwani kitendo hicho humfanya mteja asihame kwenda kupata huduma sehemu nyingine. Pia kufanya hivyo humfanya mteja ajione yeye ni wa thamani sana mbele yako.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com