METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, October 28, 2017

Dkt Shein aipongeza wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto na kuitaka kuendelea na juhudi zake za kuyashughulikia makundi yote katika jamii sambamba na kutatua changamoto walizonazo kwani hiyo ni Wizara mama.

 Dk. Shein aliyasema hayo leo, Ikulu mjini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto ilipowasilisha utekelezaji wa Mpango Kazi wa Mwaka 2016/2017, Mpango Kazi wa Utekelezaji kwa mwaka 2017/2018 na Utekelezaji wake kwa  kipindi cha robo ya kwanza ya Julai hadi Septemba, 2017.

Dk. Shein alieleza kuridhishwa na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na uongozi wa Wizara hiyo na kuupongeza uongozi wa Wizara hiyo kwa juhudi kubwa unazozichukua katika kutekeleza majikumu yake na kuutaka kuendelea na kasi waliyonayo

Katika maelezo yake, Dk. Shein alisisitiza haja kwa Wizara hiyo kuendelea kujitahidi kufanya kazi katika kuhakikisha inawashugulikia watu wote katika jamii kwani iwapo itawatumikia vyema wananchi itaipa sifa kubwa Serikali.

“Hii ni Wizara ya watu wote licha ya kuonekana ni ya kina mama lakini kina baba nao wamo” alisema Dk. Shein huku akisisitiza kuwa maendeleo ya kweli yanapatikana pakiwa na ushirikiano mzuri kati ya akina baba na akina mama kwani kila mmoja ana mchango wake katika jamii.

Pia, Dk. Shein alisisitiza haja ya kulipa kipaumbele suala zima la uwajibikaji kwa viongozi na watendaji wa Wizara hiyo ili kuleta ufanisi mkubwa zaidi.

Aidha, Dk. Shein alisisitiza umuhimu wa kufanya utafiti hasa ikizingatiwa kuwa Wizara hiyo ina mambo mengine yanayoihusu jamii.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa kutokana na mafanikio yaliopatikana katika kuwatunza wazee, tayari zaidi ya nchi 8 kutoka sehemu mbali mbali duniani kuanzia mwezi ujao zitakuja kujifunza namna Zanzibar ilivyofanikiwa katika kutoa Penjeni Jamii.

Aliongeza kuwa licha ya kuja kujifunza kuhusu Pencheni Jamii, lakini pia, nchi hizo zinakuja kujifunza ni kwa namna gani Zanzibar imefanikiwa katika suala zima la kuwatunza wazee.

Dk. Shein alieleza kuwa hakuna nchi yoyote katika ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kati inayotoa huduma za afya bure kama ilivyo Zanzibar na kueleza haja kwa Wizara kuangalia utaratibu wa kuwarahisishia huduma za afya wazee wa Zanzibar pamoja na huduma nyengine muhimu ikiwemo ya usafiri kwa vile ni wazee ambao wengi wao wameitumikia nchi hii muda mrefu na kwa njia mbali mbali.

Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliipongeza Wizara hiyo pamoja na taasisi zake zote kwa mafanikio makubwa iliyoyapata huku akisisitiza haja ya mashirikiano ya pamoja katika suala zima la uwezeshaji hatua ambayo itawasaidia sana vijana na akina mama.

Mapema Mshauri wa Rais katika Ushirikiano wa Kimataifa, Fedha na Uchumi Balozi Mohammed Ramia Abdiwawa alieleza umuhimu wa vijana kuwa tayari kufanya kazi mbali mbali za halali ili kuweza kujipatia kipato na kuendesha maisha yao, ambapo katika kipindi hichi cha uchumaji karafuu alisisitiza kwamba ni vyema vijana wanaoishi katika maeneo yenye kuzalisha zao hilo wakashiriki katika uchumaji hali ambayo itawasaidia kupata kipato sambamba kusaidia ukuaji wa uchumi.

Waziri wa Wizara ya Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Maudline Cyrus Castiko alitumia fursa hiyo kumpongeza Dk. Shein kwa kazi nzuri anayoifanya na naamna anavyosaidia katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuhakikisha maendeleo yanapatikana katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na ustawi wa jamiii.

Aidha, Waziri Castiko alimpongeza Dk. Shein kwa busara zake na kudumisha amani na utulivu nchini inayopelekea kuongeza kasi ya maendeleo.

Waziri Castico alieleza kuwa  Wizara hiyo inaendelea kusimamia vyema utekelezaji wa miongozo ya kazi ya Kitaifa na Kimataifa, kupunguza tatizo la ajira kwa vijana, kuwawezesha wananchi kiuchumi na kuimarisha maendeleo na Ustawi wa Wanawake, Vijana, Watoto na Wazee.

Alieleza kuwa Wizara hiyo pia, inaendelea kuratibu uzingatiaji wa masuala ya jinsia katika Sera, Sheria, Mipango na Bajeti za Kitaifa na Kisekta.

Nao uongozi wa  Wizara hiyo ulieleza jinsi hatua za makusudi zilizochukuliwa na katika kuwatunza wazee waliokuwemo katika nyumba za wazee na kueleza jinsi wanavyoridhika na huduma zinazotolewa katika vituo hivyo ikiwemo chakula pamoja na kumpongeza Rais kutokana na nyongeza ya posho yao baada ya kuongezwa mishahara kwa wafanyakazi wa sekta ya umma.

Aidha, uongozi huo ulieleza namna unavyoshirikiana vyema na Mabaraza ya Vijana na kueleza jinsi wanavyowasaidia katika kuwapa elimu juu ya stadi za maisha pamoja na kuwatengea kiasi cha fedha kutoka katika Bajeti ya Wizara hiyo ambacho kimeweza kuwasaidia katika kuendesha shughuli zao.

Sambamba na hayo, uongozi huo ulieleza kuwa wafanyakazi waliowengi bado hawajui namna ya kujiangalia afya zao wakiwa kazini na kueleza juhudi kubwa wanazozichukua za kutoa elimu kwa wafanyakazi pamoja na jamii nzima kwa jumla.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
The post Dk. Shein aipongeza wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto. appeared first on Zanzibar24.
Zanzibar 24
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com