METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, October 15, 2017

DKT TIZEBA AWASIHI VIONGOZI NA WANANCHI KUSHIRIKI MAADHIMISHO YA SIKU YA CHAKULA MKOANI GEITA

Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles John Tizeba

Na Mathias canal, Geita

Viongozi wa serikali, Taasisi binafsi, Wadau wa kilimo, Mifugo na Uvuvi na Wananchi kwa ujumla wake wameombwa kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya siku ya Chakula Duniani ambayo Kitaifa yanafanyika Katika VIwanja vya CCM Kalangalala Mkoani Geita.

Msisitizo huo umejikita zaidi kwa wananchi wote ambapo umuhimu zaidi umeelekezwa Kwa wakazi wa Mkoa wa Geita na mikoa jirani ukiwemo mkoa wa Mwanza, na Kagera ili kujionea Maonyesho ya kazi mbalimbali zinazolenga kuongeza uzalishaji, tija na upatikanaji wa chakula na usindikaji wa mazao ya kilimo, ufugaji na uvuvi.

Kusikiliza Nyimbo, ngonjera, mashairi na ngoma za asili zinazohamasisha uzalishaji na upatikanaji wa chakula sambamba na Kupata elimu juu ya hifadhi ya mazingira – udongo, maji na viumbe hai.

Akizungumza na waandidhi wa habari Ofisini kwake Jijini Dar es salaam Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles John Tizeba alisema kuwa maadhimisho hayo ya wiki ya chakula ambayo hufanyika kuanzi Octoba 10 mpaka Octoba 16 kila mwaka huwa na dhamira ya Kuwawezesha Wakulima, Wafugaji na Wavuvi kujifunza teknolojia sahihi za kuongeza uzalishaji na tija katika Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa lengo la kupata chakula bora na cha kutosha kwa kila mtu na kwa wakati wote.

Alisema ni njia mojawapo kwa wakulima kupata utambuzi wa Kuongeza jitihada na mbinu za kutokomeza njaa, utapiamlo na hatimaye kuondoa umaskini, Kufahamu mikakati thabiti inayoainishwa ya kuhakikisha kila mtu anapata chakula bora na cha kutosha wakati wote, na Wataalamu mbalimbali wa kilimo kuwaelimissha Wananchi ili kuondokana na mila potofu zinazozuia baadhi ya jamii kula aina fulani za vyakula, kwa mfano kutokula mayai kwa akina mama wajawazito.

Dkt Tizeba alizitaja faida zingine za maonesho hayo kuwa ni pamoja na Kuimarisha Ushirikiano wa Kitaifa na Kimataifa katika masuala ya kukuza na kuendeleza kilimo, ufugaji na uvuvi, ikiwa ni pamoja na Kuelezea kihistoria, nafasi ya mila na utamaduni katika kuendeleza sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi kwa lengo la kuongeza tija na uzalishaji.

Alisema kuwa Kila mwaka Makao Makuu ya FAO huchagua Kaulimbiu ambayo huwa ndiyo dira ya kuhamasisha wadau wote wa sekta ya kilimo kuchangia katika kuhakikisha kila mtu anawezeshwa kupata chakula bora na cha kutosha wakati wote wa maisha yake.

Kaulimbiu ya mwaka huu inasema Badili mwelekeo wa uhamaji; Wekeza katika usalama wa chakula na maendeleo Vijijini”.

Kaulimbiu hii inaweka umuhimu katika kuweka Mipango na Programu zinazolenga kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo Vijijini; kupuza utegemezi na kuongeza usawa katika Jamii, sambamba na uhifadhi mazingira ambayo ndiyo muhimu katika maendeleo ya kilimo na hifadhi ya Jamii ili yachochee jitihada za kuondoa umaskini kwa kutumia nguvukazi ya Rasilimali Watu hususani  Vijana ambayo imekuwa ikihamia Mijini kwa lengo la kujitafutia mahitaji ya muhimu na mazingira bora.

Chimbuko la Siku ya chakula ni Mkutano wa mwaka 1979 ambapo nchi wanachama wa FAO zilikutana Jijini Quebec nchini Canada na kujadili kiundani masuala mbalimbali kuhusu chakula. Mojawapo ya maazimio ya mkutano huo ilikuwa kutenga siku moja ya kila mwaka ili kuzungumzia na kutafakari njia na mbinu mbalimbali za kupata chakula cha kutosha kwa watu wote duniani na kwa wakati wote.

Maadhimisho ya kwanza ya siku hii yalianza mwaka 1981. Hivyo maadhimisho ya mwaka huu ni ya 36 na yanasherehekewa kwa pamoja na maadhimisho ya  miaka 72 ya kuanzishwa kwa FAO tarehe 16 Oktoba, 1945.

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com