METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, September 5, 2022

WANAWAKE WAOMBWA KUREJESHA MIKOPO KWA WAKATI


Salma Mdaki kutoka Jukwaa la wanawake wilaya ya Dodoma akipokea cheti cha pongezi toka kwa Afisa biashara wa Jiji la Dodoma Donatila Donisi baada ya kushiriki mafunzo ya kujiinua kiuchumi yaliyofanyika juzi Dodoma.(kulia) Afisa masoko Jiji la Dodoma Getrude Lumambo kushoto wa pili Mwenyekiti wa Jukwaa la wanawake mkoa wa Dodoma Mary Mabhaye.


Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake Kiuchumi mkoa wa Dodoma Mary Mbwire Mabhaye akizungumza kwenye semina ya mafunzo ya kuwainua kiuchumi iliyofanyika Dodoma jana.

MWENYEKITI wa Jukwaa la Wanawake wa mkoa wa Dodoma Mary Mabhaye amewataka  wanawake wanaochukua mikopo kutoka taasisi za kifedha kutokuwa watumwa kwa kushindwa  kurejesha kwa wakati.

Aidha,badala yake wawe na elimu ya matumizi na nidhamu ya fedha za mikopo,ili waweze kumudu kurejesha kwa wakati na wapatiwe mikopo tena.

Mabhaye amesema hayo alipokuwa akizungumza na Wanawake kwenye semina  ya Jukwaa la Wanawake kwa ajili ya mafunzo ya kuwainua kiuchumi iliyofanyika Jijini Dodoma.

Alisema wanawake wengi wamekuwa wakianzisha vikundi kwa malengo ya kukopa fedha ili waondokane na utegemezi na umasikini lakini matokeo yake wakati wa kurejesha wanageuka kuwa watumwa.

Alisema wanawake hao badala yake wamekuwa watumwa na kusababisha hata familia zao kushindwa kuzilea kutokana na kuwa na muda mwingi wa kuishi kwa kujificha.

“Tatizo walilonalo baadhi ya wanawake wanaochukua mikopo hawana elimu ya kutosha juu ya ujasiriamali,badala yake wanajikuta wakiangukia kwenye matumizi yasiyokuwa na tija ambayo ujikuta wakishindwa kurudisha mikopo hiyo kwa wakati”alisema.  

Mwenyekiti huyo,hata hivyo amewashauri wanawake hao kujitokeza kugombea kwenye  nafasi za uongozi mbalimbali hapa nchini, ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Alisema wakijitokeza wataweza kupata fursa mbalimbali nchini ambazo zitakazo wainua kiuchumi na kuwasaidia wanawake wengine katika suala zima la kujipatia maendeleo.

Kwa upande wake Afisa Biashara wa Jiji la Dodoma Donatila Donisi, amesema wanawake wamekuwa na mchango mkubwa katika kuleta maendeleo kwa lengo la kukuza  uchumi nchini hivyo wamejiandaa vyema kutoa  elimu kwenye vikundi vyao .

Donisi amesema kuwa wanawake wengi wamekuwa wakianzisha vikundi mbalimbali katika  suala zima la kujikwamua kiuchumi.hivyo kwa upande wao kama Jiji wamejipanga katika kuwapatia elimu ya ujasiliamari.

“Halmashauri ya Jiji wataweza kutoa elimu hususani katika biashara wanazofanya kwa lengo la kurasimisha ili kuwasaidia katika kutambulika na  kupata masoko ya kufanyia biashara kwa urahisi.

"Sisi kama Jiji hususani kwenye ofisi ya biashara tutakuwa tayari kwa ajili ya kuwapa elimu mbalimbali ikiwemo umuhimu wa kurejesha mikopo kwa wakati pamoja na ulipaji wa kodi ili kuwezesha serikali kufanya maendeleo,"alisema.

Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo ya kujikwamua kiuchumi Juliana Sakaine,Ailen Salvatory wamewashauri wajasiliamari kutengeneza bidhaa zitakazowafanya kuingia kwenye soko la ushindani ndani ya nje ya nchi.

Walisema kuwa tatizo lililopo kwenye bidhaa nyingi zinazo tengenezwa hazina viwango na zilizo nyingi zinakosa masoko na kwa sababu hiyo watu bado wataendelea kuzipenda zinazotoka nje ya nchi.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com