MKURUGENZI wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Tanzania (DCI), Robert
Boaz Mikomangwa amesema Jeshi la Polisi nchini Tanzania na vyombo
vingine vya ulinzi na usalama vinao uwezo mkubwa wa kuchunguza matukio
ya uhalifu, yakiwemo ya mauaji na utekaji bila kusaidiwa na vyombo vya
nje.
DCI Mikomangwa aliyasema hayo nchini hapa baada ya kuhudhuria Mkutano
Mkuu wa 86 wa Taasisi ya Polisi ya Kimataifa (Interpol) wa Kuzuia
Uhalifu wa Kijinai wenye lengo la kuziweka pamoja taasisi za usimamizi
wa sheria ili kukabiliana na uhalifu duniani.
Mkutano huo uliohudhuriwa
na wawakilishi kutoka nchi wanachama 192, ulifunguliwa na Rais wa China,
Xi Jinping ambapo Tanzania iliwakilishwa na DCI Mikomangwa, Mkuu wa
Kitengo cha Interpol Tanzania, Daniel Nyambabe na Ofisa Mratibu wa China
katika Kitengo cha Interpol Tanzania, Damas Nyungula.
Akizungumza na HabariLeo Jumapili, DCI alisema Jeshi la Polisi
Tanzania linao uwezo wa kutambua ni wakina nani wanajihusisha na vitendo
vya uhalifu ikiwemo mauaji bila kuingiliwa na vyombo vya kimataifa.
Alisema ni katika uimara huo, jeshi hilo litapata mafanikio katika
kuchunguza pia tukio la kushambuliwa kwa Mbunge wa Singida Mashariki,
Tundu Lissu (Chadema) hivi karibuni.
“ Hatuwezi kuzuia fikra za watu katika tukio hili, kwani tukio lolote
likitokea kila mtu ana tafsiri yake…sasa haiwezekani kupiga ramli kuwa
fulani ndiyo alihusika ni vema kutupa nafasi tuchunguze suala hili
watakuja kujua ni nani alihusika,” alisema
DCI ambaye alisema tukio hilo
ni la kawaida kama ilivyo kwa matukio mengine. Hivi karibuni, viongozi
wa Chadema waliitaka serikali iruhusu vyombo binafsi vya usalama
kuchunguza tukio la kupigwa risasi kwa Lissu na watu wasiojulikana.
Walitaja taasisi binafsi za uchunguzi wa kimataifa kutoka vyombo kama
FBI au ‘Scotland Yard’ ili kuwatambua na kuwathibitisha waliohusika na
kitendo hicho.
Akizungumzia mkutano huo wa Interpol wa siku nne, DCI Mikomangwa
alisema mjadala mkubwa ulijikita katika vitendo vya uhalifu
vinavyosumbua dunia hasa ule unaovuka mipaka makosa ya kimtandao kwani
uhalifu huo unaweza kufanyika China na kuathiri Tanzania.
Alisema
uhalifu huo umekuwa ukiongezeka kwa kadri teknolojia inavyokua na
kuathiri nchi zinazoendelea na zile zilizoendelea hivyo mikakati ya
pamoja inatakiwa katika kukabiliana na uhalifu huo.
“Tanzania tunakabiliwa sana na uhalifu huo ambao kwa asilimia kubwa
kwa sasa lazima uhalifu unafanywa kwa kutumia mtandao, hivyo kupaswa
kwenda sambamba na ukuaji wa teknolojia katika kupambana na uhalifu huo,
jambo ambalo ni changamoto kubwa,” alisema.
Alisema katika mkutano huo wameweka mikakati katika ushirikiano
kukabiliana na uhalifu huo huku nchi wanachama zisizo na mifumo ya
mawasiliano na nchi nyingine wakipatiwa fedha kununua vifaa ili
kuhakikisha mhalifu yeyote kwenye nchi mwanachama anadhibitiwa.
DCI
alisema pia walipata fursa ya kukaribisha wanachama wapya wawili ambao
ni nchi ya Palestina na Visiwa vya Solomon kwa vigezo kuwa uhalifu hauna
mipaka hivyo lazima vyombo vya usalama kushirikiana.
Akifungua mkutano huo, Rais wa China aliahidi kusaidia taasisi hiyo
vifaa mbalimbali vya ulinzi na usalama ili kusaidia nchi 100 za Afrika,
ambapo DCI alisema anaamini Tanzania itakuwa nchi mojawapo
itakayonufaika na misaada hiyo.
Rais Jinping alisema China itaendelea kushirikiana na taasisi hiyo
kuhakikisha wanakabiliana na vitendo vya uhalifu duniani na kutangaza
msaada wa kifedha na vifaa mbalimbali kukabiliana na changamoto za
uhalifu.
Baadhi ya vitendo vya uhalifu alivyotangaza kutoa msaada
kukabiliana navyo ni ugaidi, uhalifu wa kimtandao na ulinzi na usalama
wa jamii kwa ajili ya kuleta maendeleo.
0 comments:
Post a Comment