Sunday, October 1, 2017

DCI atinga Interpol, asifu vyombo vya ulinzi

MKURUGENZI wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Tanzania (DCI), Robert Boaz Mikomangwa amesema Jeshi la Polisi nchini Tanzania na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vinao uwezo mkubwa wa kuchunguza matukio ya uhalifu, yakiwemo ya mauaji na utekaji bila kusaidiwa na vyombo vya nje.

DCI Mikomangwa aliyasema hayo nchini hapa baada ya kuhudhuria Mkutano Mkuu wa 86 wa Taasisi ya Polisi ya Kimataifa (Interpol) wa Kuzuia Uhalifu wa Kijinai wenye lengo la kuziweka pamoja taasisi za usimamizi wa sheria ili kukabiliana na uhalifu duniani. 

Mkutano huo uliohudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi wanachama 192, ulifunguliwa na Rais wa China, Xi Jinping ambapo Tanzania iliwakilishwa na DCI Mikomangwa, Mkuu wa Kitengo cha Interpol Tanzania, Daniel Nyambabe na Ofisa Mratibu wa China katika Kitengo cha Interpol Tanzania, Damas Nyungula.

Akizungumza na HabariLeo Jumapili, DCI alisema Jeshi la Polisi Tanzania linao uwezo wa kutambua ni wakina nani wanajihusisha na vitendo vya uhalifu ikiwemo mauaji bila kuingiliwa na vyombo vya kimataifa. 

Alisema ni katika uimara huo, jeshi hilo litapata mafanikio katika kuchunguza pia tukio la kushambuliwa kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) hivi karibuni.

“ Hatuwezi kuzuia fikra za watu katika tukio hili, kwani tukio lolote likitokea kila mtu ana tafsiri yake…sasa haiwezekani kupiga ramli kuwa fulani ndiyo alihusika ni vema kutupa nafasi tuchunguze suala hili watakuja kujua ni nani alihusika,” alisema

DCI ambaye alisema tukio hilo ni la kawaida kama ilivyo kwa matukio mengine. Hivi karibuni, viongozi wa Chadema waliitaka serikali iruhusu vyombo binafsi vya usalama kuchunguza tukio la kupigwa risasi kwa Lissu na watu wasiojulikana. 

Walitaja taasisi binafsi za uchunguzi wa kimataifa kutoka vyombo kama FBI au ‘Scotland Yard’ ili kuwatambua na kuwathibitisha waliohusika na kitendo hicho.

Akizungumzia mkutano huo wa Interpol wa siku nne, DCI Mikomangwa alisema mjadala mkubwa ulijikita katika vitendo vya uhalifu vinavyosumbua dunia hasa ule unaovuka mipaka makosa ya kimtandao kwani uhalifu huo unaweza kufanyika China na kuathiri Tanzania. 

Alisema uhalifu huo umekuwa ukiongezeka kwa kadri teknolojia inavyokua na kuathiri nchi zinazoendelea na zile zilizoendelea hivyo mikakati ya pamoja inatakiwa katika kukabiliana na uhalifu huo.

“Tanzania tunakabiliwa sana na uhalifu huo ambao kwa asilimia kubwa kwa sasa lazima uhalifu unafanywa kwa kutumia mtandao, hivyo kupaswa kwenda sambamba na ukuaji wa teknolojia katika kupambana na uhalifu huo, jambo ambalo ni changamoto kubwa,” alisema.

Alisema katika mkutano huo wameweka mikakati katika ushirikiano kukabiliana na uhalifu huo huku nchi wanachama zisizo na mifumo ya mawasiliano na nchi nyingine wakipatiwa fedha kununua vifaa ili kuhakikisha mhalifu yeyote kwenye nchi mwanachama anadhibitiwa. 

DCI alisema pia walipata fursa ya kukaribisha wanachama wapya wawili ambao ni nchi ya Palestina na Visiwa vya Solomon kwa vigezo kuwa uhalifu hauna mipaka hivyo lazima vyombo vya usalama kushirikiana.

Akifungua mkutano huo, Rais wa China aliahidi kusaidia taasisi hiyo vifaa mbalimbali vya ulinzi na usalama ili kusaidia nchi 100 za Afrika, ambapo DCI alisema anaamini Tanzania itakuwa nchi mojawapo itakayonufaika na misaada hiyo.

Rais Jinping alisema China itaendelea kushirikiana na taasisi hiyo kuhakikisha wanakabiliana na vitendo vya uhalifu duniani na kutangaza msaada wa kifedha na vifaa mbalimbali kukabiliana na changamoto za uhalifu. 

Baadhi ya vitendo vya uhalifu alivyotangaza kutoa msaada kukabiliana navyo ni ugaidi, uhalifu wa kimtandao na ulinzi na usalama wa jamii kwa ajili ya kuleta maendeleo.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Tanzania (DCI), Robert Boaz (kushoto)

No comments:

Post a Comment