Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
ametoa agizo kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kuhakikisha haitoi
rufaa ya matibabu nje ya nchi ikiwa wana uwezo wa kutibu maradhi husika
hapa nchini.
Ummy
amesisitiza wataalamu kutowaogopa wanasiasa ikiwa wana uwezo wa kumtibu
mgonjwa hapa nchini haina ulazima wa kumwandikia rufaa nje ya nchi hata
akiwa ni Rais John Magufuli.
Ametoa
agizo hilo leo Jumatatu wakati akipokea msaada wa vifaa vipya kwa ajili
ya vyumba viwili vya upasuaji vya watoto wadogo na wodi ya watoto ya
upasuaji vyenye thamani ya Dola za Marekani 675,000 sawa na Sh1.5
bilioni, kutoka kwa wataalamu na wahisani kutoka nchini Uingereza
kupitia taasisi ya Archie Wood Foundation.
"Rais
aliponiteua aliniagiza kwamba lazima niachane na rufaa za nje, hatuwezi
kuachana nazo ikiwa magonjwa yanayoweza kutibiwa ndani yatatibiwa nje,"
amesema Ummy.
Amesema
Watanzania wana imani na Muhimbili na hivi sasa wengi wanatoka
hospitali za kulipia na kufuata matibabu ila changamoto iliyopo ni
majengo lakini wapo mbioni kujenga jengo la ghorofa kwa ajili ya
wagonjwa wa kulipia.
"Msitoe
rufaa ya mgonjwa kama hamjajiridhisha kwamba mnaweza kumtibu hapa hata
kama awe Rais, waziri au nani msitoe rufaa kwani maana yake mtakuwa
mmeshindwa ni lazima ninyi mseme kwamba hamuwezi na sisi
tutashughulikia," amesema.
Amewatahadharisha
wataalamu hao na wanasiasa kwamba lazima wahakikishe kweli hawawezi
kutibu na kwamba wizara ipo tayari na itawaunga mkono.
0 comments:
Post a Comment