Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhandisi Mussa Iyombe,
akizungumza kabla yakuanza makabidhiano ya zilizo kuwa Nyumba za CDA
kutoka Manispaa ya Dodoma iliyopewa hapo awali kwenda kwa Wakala wa
majengo Tanzania (TBA).
Katibu Mkuu Mkuu OR-TAMISEMI,Mhandisi Mussa Iyombe, pamoja na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa majengo nchini, Msanifu Majengo Elius Mwakalinga, wakiweka saini makubaliano ya kukabidhiana zilizokuwa nyumba za CDA.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhandisi Mussa Iyombe, akipokea Nyaraka kutoka kwa Mkurugenzi wa manispaa ya Dodoma kabla yakuzikabidhi kwa Mtendaji Mkuu wa wakala wa majengo Tanzania.
Katibu Mkuu Mussa Iyombe akifanya makabidhiano rasmi na Mtendaji mkuu wa Wakala wa Majengo nchini. TBA.
Baadhi ya washuhudiaji wakiwa katika makabidhiano hayo hapa wakishuhudia.
Na. Angela Msimbira- TAMISEMI.
Katibu Mkuu Ofisi ya Ras Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Mussa Iyombe amesema kuwa zaidi ya kaya 438 za watumishi wa umma watakaohamia Dodoma na wenye sifa ya kupatiwa nyumba na Serikali watakuwa na uhakika wa kupata nyumba zilizokuwa zikimilikiwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA)
Akikabidhi Nyumba zilizokuwa zikimilikiwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu kwa Wakala wa Majengo (TBA) Mhandisi Mussa Iyombe amesema, nyumba hizo zitakuwa maalum kwa watumishi wenye sifa kulingana na miundo ya kitumishi.
‘’Nyumba ambazo zinakabidhiwa kwa Wakala wa Majengo ni nyumba za kuishi ambazo awali zilimilikiwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu na kuhamishiwa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma” Amesema Mhandisi Iyombe.
Akitoa Maelezo ya awali Mhandisi Musa Iyombe amesema baada ya kuivunjwa kwa CDA iliagizwa kuwa watumishi wote waliokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kupangiwa kazi kwenye Ofisi za Serikali na kipaombele cha kwanza kilikuwa ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma kuchagua watumishi wanaomfaa kwa ajili ya kuendeleza kazi zilizokuwa zikifanywa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kazi ambayo kwa sasa imekamilika.
Mhandisi Iyombe amesema mali zilizokuwa zikimilikiwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu yakiwemo majengo ya kibiashara kama vile maduka na ofisi zimeelekezwa zibaki chini ya Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma lakini majengo ya makazi yakabidhiwe kwa Wakala wa Majengo Tanzania(TBA)
‘’Hatuna lengo la kuidhoofisha Manispaa ya Dodoma lakini Serikali inaangalia wanafaidika nini na nyumba hizo wakati majengo yote ya serikali yanatakiwa kuwa chini ya Wakala wa Majengo Tanzania na wakati huohuo watumishi wote wa Serikali wanahamia Dodoma na hawana maeneo ya kuishi,nyumba zipo zilizokuwa zinamilikiwa na CDA zinapangishwa kwa wapangaji ambao hawalipi pango za nyumba kwa wakati” Amesema Iyombe
Akifafanua zaidi Mhandisi Iyombe amesema majengo yaliyopo ni 141 kati ya hayo kuna magorofa 45 hivyo familia ambazo zinaweza kuingia katika majengo hayo ni kaya 438 hivyo matarajio ya Serikali ni kwamba watumishi 438 wenye sifa ya kupatiwa nyumba waliopo Dar-es-salaam watapata makazi hapa Dodoma.
Amesema kuwa nyumba ambazo zinakabidhiwa kwa Wakala wa Majengo ni nyumba za kuishi ambazo awali zilimilikiwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu na kuhamishiwa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma na kutokana na agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli nyumba hizo kwa sasa zitakuwa zikimilikiwa na Wakala wa Majengo (TBA) ili nyumba hizo zitumike kwa watumishi wa Serikali wanaohamia Dodoma.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi amesema kuwa wamepokea maelekezo ya Serikali ya kukabidhi nyumba za makazi kwa Wakala wa Majengo Tanzania kwa kuwa Dodoma sasa ni Makao Makuu ya Nchi.
‘‘Kumekuwepo na changamoto ya makazi kwa watumishi wanaohamia Dodoma lakini nyumba zinazokabidhiwa zipo katika hali ya matumizi na nyingine zinahitaji ukarabati ambao tunadhani wenzetu wa TBA wataendelea nao.
Wakati huo Mkurugenzi Mkuu Wakala wa Majengo Tanzania Msanifu Majengo Elius Mwakalinga amesema kuwa kumekuwepo na tatizo kubwa la upatikanaji wa nyumba kwa watumishi wa umma hivyo nyumba 438 zitasaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa nyumba hasa kwa watumishi wanaohamia Dodoma.
Amesema kuwa kwa Mkoa wa Dodoma Wakala wa majengo,Tanzania (TBA) ilikuwa na nyumba zaidi ya 400 ambazo zilikuwa kwenye maeneo ya Area D na Kisasa hivyo kwa nyumba hizo sasa watakuwa na jumla ya nyumba zaidi ya 800.
Amesema pia mbali ya nyumba hizo, ‘’Wakala wa Majengo Tanzania inampango wa kujenga nyumba 100 Mkoani Dodoma kwa mwaka huu na wanategemea ndani ya miaka miwili kukamilisha ujenzi wa nyumba 500 hivyo watajitahidi kuhakikisha nyumba hizo zinakamilika ili kuondoa upungufu wa nyumba kwa watumishi wanaohamia makao makuu ya nchi.
0 comments:
Post a Comment