Na. Tiganya Vincent – RS Tabora
MKUU wa Mkoa wa Tabora Aggrey
Mwanri amemtaka Katibu Tawala mkoa huo kuuandikia uongozi wa Halmashauri
ya Wilaya ya Tabora kuwachukulia hatua wajumbe wa timu ya mradi wa
Miombo Wilayani Uyui kwa sababu za kushindwa kufanya kazi na kuchelewa
kuanza kwa mradi wa ufugaji kuku wenye thamani shilingi milioni tano.
Mwanri alitoa agizo hilo jana
wakati alipotembea Halmashauri hiyo kwa ajili ya kukagua miradi
mbalimbali inayotekelezwa chini ya ufadhili wa Miombo ambayo ni pamoja
na ufugaji nyuki, kuku, samaki, mbuzi, utengezaji wa mkaa mbadala na
mingine mingi.
Alisema kuwa haiweziekani fedha
ziingie kwenye Akaunti ya Halmashauri ya Wilaya ya Tabora toka mwezi
Julai hadi hivi sasa hazijaelekezwa katika mradi uliokusudiwa wa
uanzishaji wa kikundi cha ufugaji wa kuku kwenye vijiji husika.
Mwanri alisema kuwa Mradi huo
uliokuwa utekelezwa katika vijiji vya Inonelwa, Ibiri na Msimba ungekuwa
umeanza kutekelezwa mara baada ya fedha zilizopingia miezi mitatu
iliyopita, hivi sasa wananchi wangekuwa wanaendelea na uzalishaji lakini
wao wamezikalia tu.
“Muda wa ngonjera umekwisha
…ukifanya kosa mimi nakushughulikia pale pale ili waje wanaokutetea nao
niwashughulike…haiwezekana tukaendelea kufanyakazi kwa mazoea fedha
zinakuja, hazipelekwi kwenye miradi iliyokusudiwa kwa sababu ya uzembe
wa wachache” alieleza Mwanri.
Wajumbe ambao amegizwa
wachukuliwe hatua ni wale walioko katika timu ya mradi wa miombo
wilayani hapo ambao ni pamoja na Mratibu wa Mradi Wilaya Kaliua, Afisa
Mifugo, Afisa Kilimo, Afisa Ushirika na Afisa Nyuki.
Kwa upande wa Mratibu wa Miombo
Kitaifa Yobu Kiungo alisema kuwa athari za ucheleweshaji wa mradi wowote
unaweza kusababisha mradi huo kupelekwa katika maeneo mengine ambayo
yatakuwa tayari kuuchangamkia.
Alisema kuwa athari nyingine kuwa endapo miradi iliyopangwa kutekelezwa katika eneo husika katika kipindi fulani isipofanyika kwa zaidi ya asilimia 80 inathiri hata maeneo meninge ya mkoa husika.
Kiungo alitoa wito kwa
Wakurugenzi Watendaji wa Manispaa ya Tabora, Wilaya ya Tabora, Urambo na
Kaliua ambapo ndipo miradi hiyo inatekelezwa kuunga mkono juhudi
zinafanyika ili iweze kukamilika kwa wakati na iweze kuwa na manufaa kwa
wakazi wa eneo husika.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji
Hadija Makuwani alisema kuwa alilazimika kuzuia fedha baada ya
kutoridhishwa na maandalizi ya mabanda ya kuku katika vijiji hivyo.
Alisema kuwa aliamua kuchukua
taadhari ili fedha hizo zisije zikapotea kwa kupeleka katika eneo ambao
wanakijiji hawajiandaa na mradi.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa amemwagiza Mkaguzi wa Hesabu za Serikali za Mitaa kutoka ofisini
kwake Hamis Mjanja kupitia miradi yote ya Miombo iliyopo katika Wilaya
ya Uyui ili kuona kama thamani yake inalingana na fedha zilizotolewa na
mradi.
Alisema kuwa hatua hiyo inalenga
kutaka kujiridhisha kama kweli kinachoenda kwa wananchi ndio kile
kilichoandikwa katika vitabu na siovinginevyo.
0 comments:
Post a Comment