METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, September 25, 2017

Ndugai: Tundu Lissu ana Bima ya Bunge, Hapaswi Kutibiwa kwa Michango

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amefunguka na kudai matibabu ya Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu hayawezi kufanyika kwa kuchangishana michango kwa kuwa ana bima yake na haki zake ndani ya Bunge.
Spika Ndugai amebainisha hayo leo asubuhi wakati akizungumza kwenye kipindi cha East Africa Breakfast kutoka East Africa Radio baada ya kuulizwa swali kwamba kuna utaratibu gani endapo mbunge akiumia ama akiumwa akiwa kazini.

"Utaratibu ni kwamba wabunge wote wana bima pamoja na mimi mwenyewe, Mawaziri wote wana bima ndani ya bunge kwa sababu ni wabunge kwanza kabla ya kuwa Mawaziri. Kwa hiyo bima zao ndiyo zinazowahudumia na tunahudumiwa kupitia hospitali zote za serikali, tunalazwa kama watanzania wengine wowote wale. Ikitokea yanahitajika matibabu ya nje ya nchi, yatatoka mapendekezo katika hospitali ya Muhimbili kwamba matibabu ya huyo mtu  yanapaswa yakafanyikie nje ya nchi kutokana na upungufu wa jambo fulani hapa nchini", amesema Spika Ndugai.

Pamoja na hayo, Spika Ndugai aliendelea kwa kusema "Tukirudi kwa Mhe. Lissu ni kwamba tulikuwa wote hapa Dodoma, baada ya kuombwa na familia pamoja na Mhe. Mbowe kwamba ni vyema apelekwe kutibiwa katika hospitali ya Nairobi nchini Kenya tulikubaliana kwa pamoja kuwa ni vizuri aende huko. Lakini alienda huko kama vile ni hospitali binafsi ambayo ipo nje kidogo ya mkondo wetu wa kawaida. Kwa hiyo bado bima yake ipo hapa bungeni na utaratibu wa kumtibu upo".

Aidha, Spika Ndugai amesema bunge kwa ujumla haliwezi kumtupa Mhe. Lissu hata kidogo kuhusiana na masuala ya matibabu yake.

"Sisi kama bunge hatujamtupa mwenzetu na bahati nzuri serikali imetoa tamko lake kuwa halijamtupa, ni suala la kuwekana sawa tu badala ya matamko kwenye vyombo vya habari, magazeti ambayo yamekuwa yakipotosha tu na kuleta malumbano ambayo hayana sababu. Kwa hiyo wito wangu kwa wahusika wote ikiwa ni pamoja na familia ya Lissu, CHADEMA, uongozi wa bunge na serikali endapo tukikaa pamoja hakuna ambacho kitashindwa kuzungumzika, hatuwezi kumtibu mwenzetu kwa michango ya kuchangishana wakati ana bima yake na haki zake", amesisitiza Spika Ndugai.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com