Spika
wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amefunguka na kudai matibabu ya Mbunge
wa Singida Mashariki Tundu Lissu hayawezi kufanyika kwa kuchangishana
michango kwa kuwa ana bima yake na haki zake ndani ya Bunge.
Spika
Ndugai amebainisha hayo leo asubuhi wakati akizungumza kwenye kipindi
cha East Africa Breakfast kutoka East Africa Radio baada ya kuulizwa
swali kwamba kuna utaratibu gani endapo mbunge akiumia ama akiumwa akiwa
kazini.
"Utaratibu
ni kwamba wabunge wote wana bima pamoja na mimi mwenyewe, Mawaziri wote
wana bima ndani ya bunge kwa sababu ni wabunge kwanza kabla ya kuwa
Mawaziri. Kwa hiyo bima zao ndiyo zinazowahudumia na tunahudumiwa
kupitia hospitali zote za serikali, tunalazwa kama watanzania wengine
wowote wale. Ikitokea yanahitajika matibabu ya nje ya nchi, yatatoka
mapendekezo katika hospitali ya Muhimbili kwamba matibabu ya huyo mtu
yanapaswa yakafanyikie nje ya nchi kutokana na upungufu wa jambo fulani
hapa nchini", amesema Spika Ndugai.
Pamoja
na hayo, Spika Ndugai aliendelea kwa kusema "Tukirudi kwa Mhe. Lissu ni
kwamba tulikuwa wote hapa Dodoma, baada ya kuombwa na familia pamoja na
Mhe. Mbowe kwamba ni vyema apelekwe kutibiwa katika hospitali ya
Nairobi nchini Kenya tulikubaliana kwa pamoja kuwa ni vizuri aende huko.
Lakini alienda huko kama vile ni hospitali binafsi ambayo ipo nje
kidogo ya mkondo wetu wa kawaida. Kwa hiyo bado bima yake ipo hapa
bungeni na utaratibu wa kumtibu upo".
Aidha, Spika Ndugai amesema bunge kwa ujumla haliwezi kumtupa Mhe. Lissu hata kidogo kuhusiana na masuala ya matibabu yake.
"Sisi
kama bunge hatujamtupa mwenzetu na bahati nzuri serikali imetoa tamko
lake kuwa halijamtupa, ni suala la kuwekana sawa tu badala ya matamko
kwenye vyombo vya habari, magazeti ambayo yamekuwa yakipotosha tu na
kuleta malumbano ambayo hayana sababu. Kwa hiyo wito wangu kwa wahusika
wote ikiwa ni pamoja na familia ya Lissu, CHADEMA, uongozi wa bunge na
serikali endapo tukikaa pamoja hakuna ambacho kitashindwa kuzungumzika,
hatuwezi kumtibu mwenzetu kwa michango ya kuchangishana wakati ana bima
yake na haki zake", amesisitiza Spika Ndugai.
No comments:
Post a Comment