METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, September 11, 2017

Mfumo wa EFDs Waongeza Mapato ya Halmashauri

IMG_6432
Naibu Waziri-TAMISEMI Mhe.Selemani Jafo akizungumza jambo na Naibu Katibu Mkuu-TAMISEMI Mhe.Dkt Zainabu Chaula wakati wa mafunzo ya Uongozi  kwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Manispaa,Majiji na Halmshauri yanayofanyika Mjini Dodoma na kuendeshwa na Taasisi ya Uongozi.
…………………………………………………………………..
Na: Lilian Lundo – MAELEZO – DODOMA

Matumizi ya mfumo wa ukusanyaji mapato kwa njia ya kielekroniki (EFDs) umeongeza mapato ya kodi za Serikali kwa Majiji, Manispaa na Halmashauri hapa nchini.

Hayo yameelezwa leo, Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo alipokuwa akifungua mafunzo ya uongozi kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa majiji, manispaa na halmashauri Tanzania Bara.

“Kabla ya matumizi ya mashine za EFDs baadhi ya halmashauri zilikuwa zikikusanya kati ya shilingi milioni 3 hadi 4 kwa mwezi lakini mara baada ya kuanza kutumika kwa mashine hizo mapato yamepanda mpaka kufikia shilingi milioni 24,” alifafanua Jafo.

Aliendelea kwa kusema kuwa kumekuwepo na udanganyifu mkubwa katika makusanyo ya mapato ya Serikali hapo nyuma. 

Hivyo amewataka viongozi hao kusimamia kwa umakini sekta hiyo na kuhakikisha fedha zote zinazokusanywa zinaingizwa katika mfuko mkuu wa Serikali ili ziweze kuwahudumia wananchi.

Vile vile Jafo amewataka viongozi hao kusimamia kwa umakini sekta za kilimo, maji, mifugo, elimu na afya kutokana na sekta hizo kuwa ndio  sekta pekee ambazo zinategemewa na wananchi wa hali ya chini katika kuwaingizia kipato chao cha kila siku.

Pia amewaambia viongozi hao kuwa matarajio ya wananchi juu ya mabadiliko katika maeneo yao ya kazi yako mikononi mwa mwao. Hivyo wana wajibu wa kufanya kazi kwa bidii huku wakiacha alama katika maeneo yao ya kazi ambayo haitaweza kufutwa na mtu yoyote hapo baadae.

Mafunzo hayo ya siku Tano yameandaliwa na Taasisi ya Uongozi ikiwa ni awamu ya tatu kati ya awamu nne zinazotarajiwa kufundishwa kufikia Novemba mwaka huu. Aidha katika awamu hii ya mafunzo imehusisha wakuu wa wilaya na wakurugenzi wapatao 89 kutoka mikoa ya Mbeya, Iringa, Rukwa, Njombe, Ruvuma, Songwe, Shinyanga na Dar es Salaam.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com