Naibu Waziri-TAMISEMI
Mhe.Selemani Jafo akizungumza jambo na Naibu Katibu Mkuu-TAMISEMI
Mhe.Dkt Zainabu Chaula wakati wa mafunzo ya Uongozi kwa Wakuu wa Wilaya
na Wakurugenzi wa Manispaa,Majiji na Halmshauri yanayofanyika Mjini
Dodoma na kuendeshwa na Taasisi ya Uongozi.
…………………………………………………………………..
Na: Lilian Lundo – MAELEZO – DODOMA
Matumizi ya mfumo wa ukusanyaji
mapato kwa njia ya kielekroniki (EFDs) umeongeza mapato ya kodi za
Serikali kwa Majiji, Manispaa na Halmashauri hapa nchini.
Hayo yameelezwa leo, Mjini Dodoma
na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) Selemani Jafo alipokuwa akifungua mafunzo ya uongozi kwa
wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa majiji, manispaa na halmashauri
Tanzania Bara.
“Kabla ya matumizi ya mashine za
EFDs baadhi ya halmashauri zilikuwa zikikusanya kati ya shilingi milioni
3 hadi 4 kwa mwezi lakini mara baada ya kuanza kutumika kwa mashine
hizo mapato yamepanda mpaka kufikia shilingi milioni 24,” alifafanua
Jafo.
Aliendelea kwa kusema kuwa
kumekuwepo na udanganyifu mkubwa katika makusanyo ya mapato ya Serikali
hapo nyuma.
Hivyo amewataka viongozi hao kusimamia kwa umakini sekta
hiyo na kuhakikisha fedha zote zinazokusanywa zinaingizwa katika mfuko
mkuu wa Serikali ili ziweze kuwahudumia wananchi.
Vile vile Jafo amewataka viongozi
hao kusimamia kwa umakini sekta za kilimo, maji, mifugo, elimu na afya
kutokana na sekta hizo kuwa ndio sekta pekee ambazo zinategemewa na
wananchi wa hali ya chini katika kuwaingizia kipato chao cha kila siku.
Pia amewaambia viongozi hao kuwa
matarajio ya wananchi juu ya mabadiliko katika maeneo yao ya kazi yako
mikononi mwa mwao. Hivyo wana wajibu wa kufanya kazi kwa bidii huku
wakiacha alama katika maeneo yao ya kazi ambayo haitaweza kufutwa na mtu
yoyote hapo baadae.
Mafunzo hayo ya siku Tano
yameandaliwa na Taasisi ya Uongozi ikiwa ni awamu ya tatu kati ya awamu
nne zinazotarajiwa kufundishwa kufikia Novemba mwaka huu. Aidha katika
awamu hii ya mafunzo imehusisha wakuu wa wilaya na wakurugenzi wapatao
89 kutoka mikoa ya Mbeya, Iringa, Rukwa, Njombe, Ruvuma, Songwe,
Shinyanga na Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment