Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA kutoka
Wizara ya Ardhi akitoa ufanunuzi juu ya ujenzi wa Mfumo unganishi wa
taarifa za sekta ya Ardhi (ILMIS).
Wadau wa Sekta ya Ardhi wakisiliza
taarifa kuhusu mfumo unganishi wa taarifa za sekta ya Ardhi nchini
kutoka kwa mtaalamu (hayuko pichani).
……………….
Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi imeendesha warsha ya kuwajengea uwezo wadau wa
masuala ya sekta ya ardhi nchini kuhusu mifumo mbalilmbali inavyotumika
katika kutoa huduma kwa wananchi.
Akifungua warsha hiyo Kaimu Katibu
Mkuu Wizara ya Ardhi Dkt. Moses Kusiluka alisema, hadi sasa wizara
inatumia mfumo zaidi ya mmoja kutoa huduma za kila siku kwa mwananchi.
Uwepo wa mifumo hiyo katika utoaji huduma za sekta ya ardhi ni muhimu
kwa ajili ya kurahisisha huduma. Ili kufikia malengo, ni lazima kuwepo
na mfumo mmoja utakaounganisha mifumo yote hiyo kwa lengo la kuongeza
ufanishi na kuboresha huduma.
Uundaji wa mfumo unganishi wa taarifa za sekta ya ardhi (Intergrated Land Management Information System, ILMIS)
unatekelezwa na Wizara ya Ardhi, nyumba na Maendeleo ya Makazi
ikishiriana na wataalamu kutoka kampuni ya IGN FI kwa udhamini wa Benki
ya Dunia. Uundaji huu ulishaanza na kwa sasa mfumo uko katika hatua ya
majaribio.
Dhumuni kuu la uundaji mfumo
unganishi wa taarifa za sekta ya ardhi ni kuimarisha usalama katika
umiliki wa ardhi kwa kuboresha usahihi katika taarifa za ununuzi ardhi,
usajili, upimaji na pia katika kusimamia ardhi kwa ujumla wake.
Utekelezaji wa Mfumo unganishi wa
taarifa za sekta ya ardhi (ILMIS), utahusisha mambo mbalimbali kama vile
njia rahisi na rafiki ya kusimamia uundaji na uendelezaji wa mfumo
wenyewe, majaribio ya mfumo katika utekelezaji, ubadilishaji wa taarifa
za ardhi zilizopo mfano taarifa za upimaji na ramani, hatimilki na
kuziweka katika mfumo.
Naye Msajili Msaidizi wa Hati,
Appolo Laizer alisisitizia umuhimu wa utumiaji mfumo unganishi wa
taarifa za sekta ya ardhi (ILMIS) kwa wadau wa sekta ya ardhi alipokuwa
akielezea jinsi hatimilki zitakavyotolewa na mfumo huo.
Alisema, utoaji wa hati kupitia
mfumo utaongeza usalama katika nyaraka za umiliki, huduma sahihi, salama
na kwa unafuu zaidi.
Mfumo utapunguza muda wa kuhakiki taarifa katika
uhamisho wa milki kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine, kuongeza
ulinzi kwenye maeneo yaliyotengwa kama hifadhi ya barabara, misitu au
maeneo ya wazi.
Utoaji wa hatimilki kwa kutumia
mfumo utasaidia sana kupunguza kama sio kumaliza kabisa migogoro ya
ardhi kwa kulinda umiliki wa mwananchi. Pia mfumo utaondoa migogoro ya
umilikishaji wa hati kwa mtu zaidi ya mmoja pamoja na kuongeza ulinzi wa
hatimilki katika taasisi za kifedha.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI
0 comments:
Post a Comment