Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwigulu Nchemba (Katikati), akisaini
hati ya makubaliano ya kuwarejesha makwao wakimbizi wa Burundi waishio
Tanzania wakati wa mkutano wa siku moja uliofanyika leo Jijini Dar es
Salaa. Kutoka kushoto ni Waziri wa Mambo ya Ndani wa Burundi Bw. Pascal
Barandagiye, Mkurugenzi wa Huduma za Wakimbizi Tanzania Bw. Harrison
Mseke, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi
nchini Tanzania (UNHCR), Bi. Chansa Ruth Kapaya na Mwakilishi wa
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi nchini Burundi Bw.
Abel Mbilinyi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwigulu Nchemba akibadilisha hati ya
makubaliano ya kuwarejesha makwao Wakimbizi kutoka Burundi waishio
Tanzania na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia
Wakimbizi nchini Tanzania (UNHCR), Bi. Chansa Ruth Kapaya katika mkutano
wa siku moja uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwigulu Nchemba akimsikiliza Mkurugenzi
wa Huduma za Wakimbizi Tanzania Bw. Harrison Mseke baada ya kusaini hati
za makubaliano ya kuwarejesha makwao wakimbizi wa Burundi waishio
nchini Tanzania katika mkutano wa siku moja majadiliano kuhusu
urejeshwaji wa wakimbizi hao uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwigulu Nchemba (katikati) akiteta
jambo na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia
Wakimbizi nchini Tanzania (UNHCR) Bi. Chansa Ruth Kapaya, kulia ni
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi nchini
Burundi (UNHCR) Bw. Abel Mbilinyi na kushoto ni Waziri wa Mambo ya
Ndani wa Burundi Bw. Pascal Barandagiye na Mkurugenzi wa Huduma za
Wakimbizi Tanzania Bw. Harrison Mseke (wapili kushoto) wakati wa mkutano
wa siku moja wa kusaini makubaliano ya kuwarejesha makwao wakimbizi
kutoka Burundi waishio nchini Tanzania leo Jijini Dar es Salaam. (Picha zote na: Thobias Robert – MAELEZO)
Tanzania, Burundi na Shirika la
Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wakimbizi (UNHCR) wamepitisha
mpangokazi wa kuwarejesha nyumbani wakimbizi raia wa Burundi ambao
tayari wamejiandikisha kwa hiari kurejea nyumbani.
Mpangokazi huo ni sehemu ya
makubaliano yaliyotiwa saini kufuatia Kikao cha 19 cha Kamisheni ya
Pande Tatu kilichofanyika jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na
mawaziri wanaoshughulikia wakimbizi wa Tanzania, Burundi na mwakilishi
wa UNHCR.
Chini ya Mpangokazi huo wa kipindi
cha karibu miezi minne (07 Septemba hadi 31 Disemba, 2017) wakimbizi
12,000 ambao tayari wamejiandikisha kwa hiari watarejeshwa nyumbani huku
ukitoa nafasi kwa wengine zaidi watakaojiandikisha kujumishwa.
Makubaliano hayo yalitiwa saini na
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba, Waziri wa Mambo ya
Ndani na Elimu ya Uzalendo wa Burundi Pascal Barandagiye na Mwakilishi
wa UNHCR nchini Bibi Chansa Ruth Kapaya.
Chini ya Makubaliano hayo shirika
la UNHCR na washirika wake wataweza kutembelea maeneo ya mipakani ya
Tanzania na Burundi kwa lengo la kusaidia mchakato wa urejeshaji wa
hiari wa wakimbizi hao na masuala mengine yanayohusu hifadhi ya
wakimbizi na raia wengine wanaohitaji hifadhi.
Pande hizo za makubaliano zimetoa
wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoa ushirikiano katika kutekeleza zoezi
la kuwarejesha nyumbani wakimbizi hao na kulitaka shirika la Mpango wa
Chakula Duniani (WFP) kutoa chakula kwa wakimbizi wanaorejea kwa kipindi
cha miezi mitatu.
Kikao hicho cha 19 cha Kamisheni
ya Pande Tatu kimeeleza kutumbua na kuthamini ukarimu wa watanzania
ambao umewezesha mamilioni ya wakimbizi kuishi Tanzania tangu nchi hiyo
ilipopata uhuru mwaka 1961 na zaidi kuendelea kuwakarimu wakimbizi
wapatao 350,000 miongoni mwao 256,850 wakiwa raia wa Burundi.
0 comments:
Post a Comment