1.0 UTANGULIZI
Serikali iliamua kuanzisha
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kuweza kuwezesha
upatikanaji wa mikopo katika sekta ya kilimo na kuhamasisha taasisi
zingine za fedha nchini kutoa
mikopo zaidi kwa wakulima.
TADB imeanzishwa kwa madhumuni makubwa mawili ambayo ni:
- Kusaidia upatikanaji wa utoshelezi na usalama wa chakula ambao ni endelevu nchini Tanzania;
- Kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.
Benki ya Maendeleo ya Kilimo
Tanzania ilizinduliwa Rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete siku ya Kilele cha Maadhimisho ya
Siku ya Wakulima
nchini, mnamo tarehe 8 Agosti, 2015 mjini Lindi.
Benki ilizindua utoaji wa mikopo tarehe 30 Disemba 2015 mkoani Iringa.
Tarehe tarehe 8 Agosti, 2017
ilitimiza miaka miwili (2) tangu izunduliwe na takribani mwaka mmoja na
nusu wa kutoa huduma kwa wakulima wadogo wa Watanzania ikiwa
imefanikiwa kufanya yafuatayo:
1.2 MAFANIKIO YALIYOPATIKANA TANGU JANUARI 01, 2017 MPAKA KUFIKIA AGOSTI 31, 2017
- Benki imeongeza kiasi cha mikopo kwa wakulima wadogo wadogo kutoka Shilingi 1.0 Bilioni hadi Shilingi 8.917 Bilioni;
- Benki imeweza kukopesha kutoka vikundi 8 hadi kufikia vikundi 21, Taasisi moja ya Umma na Kampuni moja ya Maziwa;
- Benki imekopesha wakulima 2610 kutoka wakulima 857; wanawake 910 na wanaume 1699;
- Benki inaendelea kufanya uchambuzi wa miradi 17 yenye thamani ya zaidi ya Shilingi 35.473 Bilioni;
- Benki imeweza kuvijengea uwezo vikundi 672 vya wakulima wadogo wadogo vyenye jumla wa wanachama 91,684 kutoka vikundi 336 vilivyokuwa vinajumuisha wakulima wadogo wadogo 44,000 katika mikoa ya Iringa, Morogoro na Tanga. Hivyo kuwezesha jumla ya vikundi 19 kutimiza masharti na maandalizi ya msingi ya kuweza kukopa; Vikundi vingine vilivyobaki vinaendelea kupatiwa mafunzo ili viweze kufikia hali ya kuweza kukopesheka;
- Kuwaunganisha wakulima wadogo 2,328 na wanunuzi kwenye mnyororo wa thamani wa mazao ya mahindi, mpunga, mboga mboga na miwa;
- Kutoa mafunzo ya Kanuni za Ukopeshaji katika Kilimo kwa wafanyakazi ya zaidi ya 60 kutoka mabenki ya biashara na taasisi za kifedha nchini ili kuwaandaa kukopesha kwa ufanisi shughuli za kilimo. Mafunzo haya yaliendeshwa kwa ushirikiano wa pamoja kati ya TADB, Benki ya Taifa ya Kilimo na Maendeleo Vijijini India (NABARD) na Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani Mazao na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF);
- Benki imeweza kupata fedha zaidi za kukopesha toka Serikalini kiasi cha Shilingi 209.5 Bilioni na nusu yake tayari zimeshapatikana kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika;
- Kuongeza wigo wa mikoa kwenye huduma kutoka mikoa sita (6) kwenda kwenye Kanda Nane (8) kwa utaratibu wa Kongani, na pia idadi ya mazao ya kipaumbele toka 14 kwenda 20 kulingana vipaumbele vya mikoa;
- Kupanua wigo wa wateja toka vikundi vya wakulima wadogo wadogo pekee hadi makampuni binafsi na ya umma, miradi ya halmashauri za wilaya inayojiendesha kibiashara;
- Kujumuisha viwanda vidogo vidogo na vya kati vya uchakataji na usindikaji wa mazao ya kilimo vyenye kuongeza thamani ya mazao;
- Kuhuisha
utaratibu wa kutoa mikopo na kusimamia utekelezaji kwa kuhusisha
uongozi wa Serikali za Mikoa na Wilaya, Kata na Vijiji moja kwa moja na
wadau wengine.
2.0 MIKAKATI WA KUJITANUA KUPITIA KONGANI
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imedhamiria na kujizatiti kuhakikisha inachangia kwa kiasi kikubwa katika kuleta Mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo nchini kwa kusaidia upatikanaji wa fedha na sera nzuri zitakazosaidia maendeleo ya kilimo nchini. Hivyo, katika kutekeleza mkakati wa kuwafikia wakulima wengi zaidi nchini Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imejipanga kutoa huduma kupitia Kongani nane (8) ili kuongeza tija kwa wakulima nchini.
2.1DHANA YA KONGANI NA MINYORORO YA ONGEZEKO LA THAMANI
Tanzania ni nchi kubwa na yenye maeneo tofauti ya kimazingira/kilimo (Makundi) ambayo yana faida linganifu kwa ajili ya kuzalisha mazao maalum au seti ya bidhaa (mazao, mifugo, uvuvi). Kongani ni njia ya kimkakati ya kijiografia yenye kujikita katika shughuli za kilimo zinazohusiana, wasambazaji, na taasisi zinazohusishwa katika kujenga usawa wa moja kwa moja miongoni mwa wadau. Ni njia yenye kujenga fursa ya ushindani kwa njia endelevu.
Upekee wa njia hii ni kuwepo kwa uhusiano na ushirikiano miongoni kwa mlolongo wa uongezaji wa thamani hasa katika makundi mbalimbali ya minyororo ya thamani, pamoja na taasisi na mamlaka za udhibiti zinazosaidia sekta ya kilimo. Ukaribu wa kitaasisi uchagiza uwezekano wa kurahisisha ushiriki na usambazaji wa maarifa na ujuzi ulio wazi na ule ujuzi usio wazi.
3.0 HITIMISHO
Kama ilivyo ada, Benki inatoa wito kwa
wananchi hususan wakulima kuunga mkono kwa vitendo nia ya dhati ya Mhe.
Rais Dkt. John Magufuli na Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwawezesha
wakulima nchini kwa
kuwapatia mikopo ya gharama nafuu inayotolewa na Benki ya Maendeleo ya
Kilimo Tanzania.
Pia, wakulima wanaombwa kuwasiliana na
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania kwa anuani na njia nyingine
zilizoainishwa hapa chini ili kuweza kupatiwa maelezo ya kina kuhusu
huduma zinazotolewa na
jinsi ya kunufaika na fursa zilizopo. Vile vile, TADB inayakaribisha
mabenki mengine na wadau mbali mbali wa Kilimo kuchangamkia fursa
zinazotolewa na TADB.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya
Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Francis Assenga (katikati)
akisisitiza jambo wakati akiongea na wanahabari kuhusu
kutimiza miaka miwili ya kutoa
huduma kwa wakulima wa Tanzania na mkakati wa TADB wa kujitanua kupitia
kongani. Wengine pichani ni
Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara
wa Benki, Bw. Augustino Matutu Chacha (kushoto) na Meneja wa Maendeleo
ya Wakulima Wadogo wa TADB, Bw. Joseph Mabula (kulia).
Meneja wa Maendeleo ya Wakulima Wadogo wa TADB, Bw. Joseph Mabula (kulia)akizungumzia nafasi ya Benki hiyo katika kuwawezesha wakulima wadogo kulima kibiashara. Wanaomsikiliza ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Francis Assenga (katikati) na Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara wa Benki, Bw. Augustino Matutu Chacha (wapili kushoto) kwa mbali kushoto ni Afisa habari Mwandamizi wa Idara ya Habari, Bw. Jonas Kamaleki.
Mmoja wa wanahabari waliohudhuria Mkutano kuhusu
kutimiza miaka miwili ya kutoa huduma kwa wakulima wa Tanzania na mkakati wa TADB wa kujitanua kupitia kongani akiuliza swali.
Wanahabari wakifuatilia kwa makini Mkutano kuhusu
kutimiza miaka miwili ya kutoa huduma kwa wakulima wa Tanzania na mkakati wa TADB wa kujitanua kupitia kongani.
0 comments:
Post a Comment