METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, August 28, 2017

SIMBACHAWENE AAGIZA BARABARA YA LUMUMA-MBUGA MPWAPWA KUNGENEZWA KWA KIWANGO KINACHOTAKIWA


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. George B. Simbachawene (Mb) akitoa maelekezo kwa Mhandisi Geophrey Mwamkinga na Wataalam wengine juu ya marekebisho ya barabara ya Lumuma hadi Mbuga yenye urefu wa kilomita 21 ambapo alimtaka kuchukua hatua kwa mkandarasi kampuni ya M/S Besta Holding Co Ltd ya Jijini Dar es Salaam kufanya marekebisho ya upanuzi wa barabara, kumwaga kifusi kisicho tereza, kujenga kingo imara za barabara na marekebisho maalum sehemu korofi kabla ya msimu wa mvua.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. George B. Simbachawene (Mb) akitoa maelekezo kwa Mhandisi Geophrey Mwamkinga na Wataalam wengine juu ya marekebisho ya barabara ya Lumuma hadi Mbuga yenye urefu wa kilomita 21 ambapo alimtaka kuchukua hatua kwa mkandarasi kampuni ya M/S Besta Holding Co Ltd ya Jijini Dar es Salaam kufanya marekebisho ya upanuzi wa barabara, kumwaga kifusi kisicho tereza, kujenga kingo imara za barabara na marekebisho maalum sehemu korofi kabla ya msimu wa mvua.


Na Fred  Kibano, Mpwapwa 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. George B. Simbachawene (Mb) amemwagiza Msimamizi wa Wakala wa barabara za Vijijini (TARURA) Mhandisi Geophrey Mwamkinga kuhakikisha barabara ya Lumuma hadi Mbuga wilayani Mpwapwa inatengenezwa kwa kiwango kinachotakiwa na kwa thamani halisi ya fedha za Serikali.

Mheshimiwa Simbachawene ameyasema hayo akiwa katika ziara ya kutembelea Mamlaka za Serikali za Mitaa ngazi ya vijiji kujionea maendeleo ya vijiji katika sekta za Afya, Elimu, Maji, Ardhi na eneo la Utawala bora ngazi ya vijiji. 

Amesema Mkandarasi anayejenga barabara hiyo kampuni ya M/S Besta Holding Co Ltd ya Jijini Dar es Salaam bado haijafanya kazi nzuri ijapokuwa ujenzi wake umefikia asilimia 70 kwani wembamba wa barabara hiyo ambao hauruhusu magari kupishana, kuwa na mitaro midogo ya kutupa maji, uvunjaji wa miamba kwa mita chache pembeni mwa barabara hiyo ya milima ya Kizi haujafanyika ipasavyo, ikiwa ni pamoja na mitaro ya kinga mita kwa pembeni na kujaza kifusi ambacho hakitelezi.

“Kwa hiyo, barabara lazima itanuliwe, mlima huu hapa hakati, huyu jamaa (Mkandarasi), anagusagusa tu lakini hakati, Yule mwenzake wa kule Wotta (kata nyingine wilayani Mpwapwa) anakata, tena ni jiwe tu kutoka chini, yeye huyu ni udongo anafanya hivi, lakini hakati (mlima kwa upande wa pembeni), hivi vifereji ni utapeli mtupu, hivi vifereji wakati wa mvua vitaondoka vyote kwa sababu hujaandaa vizuri njia yenyewe, ukijenga mfereji unacheza (ni kama utani)”  

Barabara ya kata za Lumuma na Mbuga yenye urefu wa kilomita 21 inahusisha matengenenezo makubwa, ni barabara ya siku nyingi ambayo haikuwahi kuwa chini ya Halmashauri  ambapo ni wananchi pekee na Wamisionari wa Kanisa katoliki ndio walioianzisha na kuikarabati kuweza kupita kwa shughuli zao.

Mradi huo mkubwa wa ukarabati wa barabara ulianza mapema mwezi Februari, 2017 na kutarajiwa kwisha katikati ya mwezi Agosti, 2017 na jumla ya gharama zitakazotumika ni shilingi 641,912,684 na mpaka sasa amekwishalipwa asilimia 33 ya fedha zote. 

Kwa mujibu wa Bw. Mwamkinga mpaka sasa mkandarasi huyo amekwishalipwa kiasi cha shilingi 209,175,882 na bado shilingi 432,736,802. Pia mkandarasi ameongezewa muda  wa siku 60 kutokana na changamoto za kijiografia zinazosababisha vifaa kutofika kwa wakati na kufanya ufuatiliaji kwa kuweka vikao kazi kwa kila wiki kuona maendeleo na ubora wa kazi na kutoruhusu ucheleweshaji mwingine wa kazi kabla ya msimu ujao wa mvua. 

Mheshimiwa Simbachawene anafanya ziara katika Mamlaka za Serikali za Mitaa hasa maeneo ya vijijini ili kujionea hali halisi ya utendaji, migogoro ya ardhi, utunzaji wa mazingira, huduma kwa wananchi na ukamilishaji wa miradi ya maendeleo ambapo mwishoni mwa wiki ametembelea kata za Mbuga, Kibakwe na Ipera zenye vijiji kadhaa wilayani Mpwapwa kama sehemu ya kazi zake za kujionea maendeleo ya wananchi na kero zao.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com