METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, November 3, 2019

KAMATI YA BUNGE YAITAKA SERIKALI KUONGEZA FEDHA ZA SEKTA YA MIFUGO



Mwenyekiti wa Kamati  ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji,Mhe. Mahmoud Mgimwa,(katikati) akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) Tanzania Dkt.Eligy Shirima  upande wa kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa LITA chini ya wizara ya mifugo Dkt.Pius Mwambene,akisoma taarifa kwa Kamati  ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ambayo ilitembelea Kituo cha Utafiti wa Mifugo Mpwapwa(LITA) na Ranchi ya Taifa(NARCO),
 Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel, ,akizungumza katika ziara ya kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ambayo ilifanya ziara katika Kituo cha Utafiti wa Mifugo Mpwapwa(LITA) na Ranchi ya Taifa(NARCO) zilizopo mkoa wa Dodoma.
Mwenyekiti wa Kamati  ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji,Mhe. Mahmoud Mgimwa,akizungumza na wataalamu kutoka wizara ya mifugo wakati walipofanya ziara na kamati yake katika Kituo cha Utafiti wa Mifugo Mpwapwa(LITA) na Ranchi ya Taifa(NARCO) zilizopo mkoa wa Dodoma kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel
 Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel,akiwa kwenye maabara akitoa maelezo kwa kamati Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ambayo ilifanya ziara katika   Kituo cha Utafiti wa Mifugo Mpwapwa(LITA) na Ranchi ya Taifa(NARCO),zilizopo mkoani Dodoma
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) Tanzania Dkt.Eligy Shirima,akitoa maelezo kwa kamati Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ambayo ilifanya ziara katika   Kituo cha Utafiti wa Mifugo Mpwapwa(LITA) na Ranchi ya Taifa(NARCO),zilizopo mkoani Dodoma.

………………………..

Na Alex Sonna,Mpwapwa

KAMATI ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imetembelea Kituo cha Utafiti wa Mifugo Mpwapwa(LITA) na Ranchi ya Taifa(NARCO), huku ikishauri serikali kutoa fedha za kutosha kwa ajili ya tafiti ili ziwe na tija kwa Taifa.

Kamati hiyo imefanya ziara yake leo ikiambatana na Wataalam kutoka Wizara ya Mifugo wakiongozwa na Katibu Mkuu wakikagua utendaji kazi wa kituo hicho na Ranchi ya Kongwa, mkoani Dodoma.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mahmoud Mgimwa, amesema kamati inapenda kuona wizara inazoongoza ziingie na kuwa za kipaumbele kwa kuwa malighafi za viwanda asilimia 85 inapatikana sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.

“Kama serikali inataka tufanikiwe kwenye maeneo haya ifike wakati tujielekeze  kwa nguvu, tuishawishi serikali ione umuhimu wa hizi taasisi, Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazosifika kwa ufugaji wa ng’ombe wengi bara la Afrika sasa tunafaidikaje na hiyo sifa,”amesema.

Amesema hakuna nchi yeyote Duniani iliyoendelea kama haijawekeza vya kutosha kwenye utafiti hivyo imeelekeza uboreshaji zaidi wa wataalamu na vifaa kwenye utafiti.

“Tukichelewa kuwekeza vya kutosha tukawapa fursa watu wa kutoka nje kuwekeza tutafanya utafiti kwa matakwa yao, COSTECH wametoa fedha kidogo, kwenye Baraza la Mawaziri kipindi cha nyuma serikali ilisema lazima itenge asilimia moja kutoka kwenye Bajeti kuu kwenda kwenye utafiti, je, ni kweli inatengwa kwasababu inatakiwa kugawanywa kwenye kilimo na mifugo,”amesema.

Awali, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel , ameahidi kutekeleza ushauri uliotolewa na wabunge huku akiwahamasisha waendelee kuwekeza kwenye ufugaji.

“Mtusaidie sana wabunge kuhamasisha jamii, endeleeni kufuga sana tunatamani muwe na mashamba na sisi tutakuwa tayari kutuma wataalam wetu wawasaidie,”amesema.
Amesema lengo la wizara hiyo ni kuona mageuzi ya kisayansi yanafanyika katika sekta ya mifugo na kwamba haiwezekani kufanya mageuzi bila tafiti za uhakika.

“Ndio maana tunafundisha ili kutoa taaluma hizi ambapo kutoka LITA ambao wanatoa taaluma mbalimbali ili kupata wabobezi wa kwenda kusaidia wafugaji wetu, tungependa tuhame kutoka kwenye uchumi wa uzalishaji twende kwenye uchumi wa kitaaluma, tunaamini hilo litasaidia sana,”amesema.

Amebainisha kuwa bila kuunganisha utaalam na utafiti mambo hayawezi kwenda vizuri.
Katibu huyo amesema Wizara imejipanga kuhakikisha mageuzi ya kisayansi ya mifugo yanafanikiwa.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com