Na: Judith Mhina – MAELEZO
Hakika historia imejirudia, mkoa wa
Tanga ni kati ya mikoa mashuhuri nchini Tanzania kabla ya uhuru wa
Tanganyika katika kupigania uhuru, kwa kuwa ni mkoa uliokuwa na wasomi
wengi kuliko mikoa mingine wakati huo.
Hii ilitokana na uwepo wa shule za
wamisionari wa kanisa la Anglikana (UMCA) ambalo ni la kwanza kuingia
katika Pwani ya Afrika Mashariki mwaka 1878 na waliojenga shule za
Magila na Kiwanda Muheza, Korogwe misheni, Kideleko Handeni (Shule za
Kati) na Saint Andrew Minaki Pwani (shule ya Sekondari).
Hata baada ya uhuru chini ya Serikali ya
Awamu ya Kwanza na ya Pili ya uongozi wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu
Julius K. Nyerere na Rais Msataafu Ali Hassan Mwinyi, mkoa wa Tanga
ulikuwa maarufu kutokana na uwepo wa viwanda vingi, njia za reli na
Bandari yenye kina kirefu yenye uwezo wa kuingiza meli kubwa za mizigo
za Kitaifa na Kimataifa.
Viwanda ambavyo vilijengwa katika mkoa
wa Tanga ni pamoja na vya chuma, mbolea, saruji, maziwa, kamba za
katani na mazulia, amboni plastic, mbao, sabuni maarufu ya mbuni,
gardenia, foma na mafuta ya nazi.
Historia hii sasa inajirudia katika mkoa
wa Tanga baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, John
Pombe Magufuli, kupigania kwa nguvu zote Mradi wa ujenzi wa bomba la
mafuta kutoka Uganda kuja nchini Tanzania ambalo litaishia katika kijiji
cha Chongoleani.
Wananchi wote wa Tanzania wana kila
sababu ya kujivunia ujenzi wa bomba hilo la mafuta ambalo litawapatia
ajira Watanzania hususan wananchi wa mkoa wa Tanga. Pongezi kubwa ziende
kwa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa juhudi zake za
kuhakikisha kwamba Mradi huu unakuja Tanzania. Wananchi wa mkoa wa Tanga
na Tanzania kwa ujumla wana kila sababu ya kulinda heshima ya nchi yetu
kwa kuhakikisha kuwa kunakuwepo na ulinzi mkali wa Bomba hilo kila
mahali lilikopita.
Kurejea kwa mkoa wa tanga katika ramani
ya Tanzania ya viwanda umedhihirishwa na Wananchi wa Chongoleani ambao
siku ya uwekaji jiwe la msingi walikuwa wawakilishi wa Watanzania ambao
hawakupata fursa ya kwenda Tanga kumshuhudia Mheshimiwa Rais na na mgeni
wake Rais wa Jamhuri ya Uganda Yoweri Kaguta Museveni wakifungua pazia
la jiwe la msingi kuashiria uzinduzi wa Mradi huo.
Kutokana na tukio hilo la uwekaji wa
jiwe la msingi wana Chongoleani walitoa ya moyoni kwa kuonyesha furaha
yao isiyo na kifani kupitia kwa Mwenyekiti wao wa kijiji Ndugu Mbwana
Nondo wakisema; “Kwa moyo wa dhati kabisa tunamshukuru sana Rais wetu
Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutujali Wananchi wake kwa kutuletea neema
ya mradi huu wa bomba la mafuta”.
Aidha, Mwenyekiti huyo aliongeza kwa
kusema kwamba, katika maisha yetu Wananchi wa Chongoleani hatutaweza
kumsahau Mheshimiwa Rais kwa mambo mengi anayowafanyia Watanzania na
Taifa kwa ujumla na itakuwa ni kumbukumbu kwa kizazi kijacho.
“Napenda kusisitiza kwamba tunamuahidi
Rais, kuwa wote watakaopata fursa kwenye Mradi huu wa Bomba la Mafuta,
watafanyakazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo ya mtu mmoja mmoja na
Taifa kwa ujumla”. Alihitimisha Bw Nondo.
Naye Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii
Jinsia Wazee na Watoto, Bibi Ummy Mwalimu, amewaomba wanawake wa Mkoa wa
Tanga kuchangamkia fursa zinazojitokeza, kutokana na uwepo wa mradi wa
bomba la mafuta.
Akisisitiza kuhusu ajira hizo amesema;
“Kwa wale wenye ujuzi wanaweza kupata ajira za kudumu katika mradi, ila
kwa wale ambao hawana ujuzi wachangamkie fursa nyingine kama mama lishe
ambapo mkoa unjulikana kwa kujua kupika mapishi yanayovutia walaji
wengi”
Aidha, amewaasa wakulima kuona fursa ya
kulima mazao ambayo yataliwa kwa wingi kwa watumishi watakaoajiriwa
Tanga katika mradi wa bomba la mafuta. Mfano matunda na mbogamboga
ambavyo ni sehemu ya kuimarisha lishe za watumishi hao watakao kaa
Tanga.
Mradi wa Bomba la Mafuta ni ishara njema
kwa Watanzania, Serikali na Taifa kwa ujumla maana inaonyesha dhahiri
kukosekana kwa fursa kama hii kwa miaka mingi katika mkoa wa Tanga ni
fundisho kwa Watanzania hususan Wananchi wa mkoa wa Tanga kama
waswahili wasemavyo “usichezee shilingi chooni” ikiwa na maana shilingi
ikitumbukia kuipata sio rahisi.
Kila jambo jema lina fursa zake, nalo
bomba la mafuta limekuja na neema zake, mfano wana Chongoleani kupata
barabara ya kilometa 8 inayowaunganisha na barabara kuu ya kutoka Tanga
kwenda Horohoro. Hii ina maana kubwa kwa wana chongoleani kiuchumi,
maana watakuwa na wepesi wa usafiri wa mabasi na malori. Hivyo, bidhaa
zitokazo chongoleani sasa zitaenda Tanga na nje ya mkoa wa Tanga kwa
urahisi. Mfano samaki, mazao ya chakula na mengineyo.
Wafanyabiashara wetu wachangamkie fursa
iliyojitokeza watembelee eneo husika na kudadisi kipi wanachoweza
kufanya biashara kwa ajili ya kuinua kipato chao binafsi na Taifa kwa
ujumla.
Kama tujuavyo Taifa letu liko kwenye
harakati za kuelekea katika uchumi wa viwanda, na kama ujuavyo Tanga ni
Mkoa wenye kuzalisha matunda ya aina mbalimbali na mbogamboga kwa wingi,
nazi, katani, mahindi, viazi, maharagwe, samaki, viungo kama tangawizi,
iliki, pilipili manga, mdalasini, chai na mifugo kama ngombe mbuzi na
kondoo wapo kwa makundi katika ranchi zinazotambulika na wale wanaofugwa
kiasili.
Katika suala zima la bomba la mafuta ni
muhimu mikoa yote ambapo bomba linapita kutambua na kujiandaa kuitumia
fursa zilizopo na zitakazo jitokeza katika mikoa ya; Kagera, Geita,
Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma Morogoro na Tanga. Wilaya
zitakazopitiwa na bomba hilo zipo 24 na vijiji zaidi ya 180,
vitafahamishwa kwa usahihi hapo baadaye.
Kwa kuwa Wizara ya Nishati na Madini
inahamasisha kwa pamoja na wadau mbalimbali ni vema kutumia mafunzo
hayo, kujiimarisha na kuwa sehemu ya matokeo mazuri ya bomba husika.
Bomba la Mafuta la kutoka Hoima Uganda
mpaka Tanga Chongoleani lina urefu wa Kilometa 1445 ambapo kwa upande wa
Tanzania itakuwa na jumla ya kilometa 1115 na Uganda 330. Aidha, Mradi
utatarajia kusafirisha mapipa laki mbili na kumi na sita elfu
(216,000) kwa siku .
Kijiji cha Chongoleani ndio kituo cha
mwisho ambapo mitambo mikubwa itasimikwa katika eneo hili kwa ajili ya
kusukuma mafuta eneo la baharini ili, kuweka kwenye vyombo vya
usafirishaji kusafirisha maeneo mbalimbali duniani ambayo Uganda
watakuwa wamepata soko.
Tanzania itafaidika na mradi huu
kutokana na kodi, tozo na mrahaba wa bomba la mafuta, itakayofanywa
moja kwa moja na mradi huo. Faida nyingine ambazo, sio za moja kwa moja
ni ajira, fursa za kufanya biashara katika mikoa 8 ambayo ni Kagera,
Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Morogoro na Tanga.
Tusisahau unapopata fursa moja, ni vema
kuitumia kwa kuimarisha na kuitangaza Tanga kimataifa kwa upande wa
utalii katika machimbo ya Amboni, utalii wa samaki adimu duniani
Silikanti eneo la ufukwe wa Kigombe. Samaki huyu alikuwepo duniani miaka
6000 iliyopita, ambapo alitoweka na kugundulika kuwa yupo katika pwani
ya bahari ya hindi eneo la Kigombe Muheza Tanga.
Aidha, utalii wa milima ya Usanbara na
Nnguu Kilindi, misitu ya asili ambayo kama vile miti ya miwati
inayotengeneza nta au gundi, Tao la Mashariki misitu ya asili ya Nguu na
maporomoko ya maji katika Tao la mashariki ikiwa ni pamoja na milima ya
usambara, amani, maghamba, na nguu.
Uoto wa asili na baridi ambayo
isingedhaniwa kabisa kuwepo katika milima inayoelekea bahari ya Hindi.
Pia Hifadhi ya Taifa ya wanyamapori ya
Saadani yenye kivutio cha ngiri wanaoishi katika makazi ya binadamu
ambayo ni mbuga pekee iyopo pembezoni mwa bahari katika Afirka
mashariki, pia mbuga ya Mkomazi na mbuga ya uwindaji wanyapori ya Nnguu,
madini ya aina mbalimbali, Kasa wa pembezoni mwa ufukwe wa bahari ya
Hindi na vipepeo adimu duniani wa milima ya usambara Amani. Ni vema
kuwakarimu wageni kwa utamaduni wa asili wa Tanga kwa kuwaonyesha
mapishi na ukarimu uliotukuka wa Watanzania wapatapo wageni.
Mungu Ibariki Tanzania na watu wake.
0 comments:
Post a Comment