MKUU wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida,
Miraji Mtaturu ameyashauri mabenki ikiwemo NMB kubuni bidhaa
zitakazowanufaisha Watanzania maskini ili kuondoa dhana inayowabaguzi ya
kuwa “‘maskini sio rafiki wa taasisi za kifedha”. Mtaturu ametoa wito
huo juzi wakati akifungua rasmi Tawi la Benki ya NMB Ikungi. Alisema
kuendelea kuamini kwamba maskini sio rafiki wa mabenki, kundi hilo la
Watanzania litaendelea kudidimia ndani ya lindi la umaskini.
“Kaeni muangalie kundi hili la watu
maskini litanufaikaje na huduma zinazotolewa na mabenki ikiwemo ninyi
NMB. Kundi hili la Watanzania maskini ili liweze kujikomboa kiuchumi,
basi mabenki badala ya kutoa mikopo ya fedha taslimu, toeni mikopo ya
mizinga ya nyuki, mabwawa ya kufungia samaki au kuku kwa ajili ya
kufunga kibiashara”, alishauri Mtaturu.
Akisisitiza,mkuu huyo wa wilaya, alisema
ili Mtanzania akiwemo maskini aweze kupata maendekeo ya kweli ni lazima
ajiongeze kwa kupata mikopo kutoka kwenye taasisi za kifedha.
“NMB ninyi mnakwenda vizuri na mnakwenda
na wakati. Mmeendelea kubuni bidhaa/huduma mbalimbali ambazo
zimepelekea kuvutia Watanzania zaidi ya milioni mbili kufungua akaunti
kwenye matawi yenu nchini kote”, alisema na kuongeza; “Sasa mmebuni
akaunti ya FANIKIWA, ambayo inawalenga wajasiriamali wadogo wakiwemo
baba/mama lishe na wauza chips. Hongereni sana”.
Mtaturu alisema sasa umefika wakati wa
kuliangalia upya kundi la Watanzania maskini,ili na lenyewe liweze
kushiriki kikamilifu kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa kati. Aidha,
Mtaturu ametumia fursa hiyo kuwaalika wakazi wa wilaya ya Ikungi
wahakikishe wananufaika kikamilifu na huduma mbalimbali zinazotolewa na
tawi la NMB Ikungi.
“Najua wazi wakazi wengi wa wilaya yetu
wameshindwa kunufaika na huduma za kibenki ikiwemo mikopo, kutokana na
benki zote kuwa Singida mjini umbali wa kilometa 45. Sasa NMB imesongeza
huduma karibu, tuitumie fursa hii kwa kupata mikopo kwa ajili ya kukuza
mitaji na kupanua kilimo kikiwemo cha alizeti”, alisema.
Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa
wilaya huyo,ametumia nafasi hiyo kuipongeza na kuishukuru benki ya NMB,
kwa msaada wake wa vifaa tiba kwa kituo cha afya Ikungi vyenye thamani
ya shilingi milioni tano.
“Naagiza vitanda hivi vitatu vya
kujifungulia, vifaa vya kujifungulia, vitanda na magodoro mawili ya
kupumzikia wagonjwa na mizani mbili, vitunzwe vizuri viweze kutumika kwa
kipindi kirefu”, alisema.
Awali meneja NMB kanda ya kati, Straton
Chilongola, alisema msaada huo wa vifaa tiba, ni mwendelezo wa NMB
kuunga mkono serikali ya awamu ya tano katika kuboresha sekta ya afya.
Alisema benki hiyo imeendelea kubuni bidhaa mbalimbali na zenye
kuzingatia mahitaji halisi ya soko kwa wakati husika.
“Moja ya bidhaa hizo ni kampeni ya
‘FANIKIWA’ akaunti ambayo ni mahususi kabisa kwa wajasiriamali wadogo
wadogo.Wajasiriamali hao ni pamoja na baba/mama lishe, wauza chipis,
wenye maduka ya biashara yakiwemo ya nguo”, alifafanua Chilongola.
Akifafanua zaidi, alisema akaunti hiyo
inampa fursa mteja kupata mkopo wa shilingi laki tano hadi shilingi 30
milioni. Pia meneja huyo, alisema wanayo akaunti nyingine ya ‘Wajibu’
ambayo ni mahususi kwa ajili ya watoto wenye umri wa miaka 0-18.
“Kwa upande wa teknolojia tuna akaunti
ya ‘Chap Chap’. Akaunti hii mteja anaweza kufungua akaunti kwa muda
mfupi na papo hapo kupata kadi yake ya ATM, na kuanza kufanya miamala wo
wote”, alisema Chilongola.
Benki ya NMB, ina matawi zaidi ya 200 na
mashine za kutolea fedha zaidi ya 700 nchi nzima. Ina wateja zaidi ya
milioni mbili jambo linaloifanya kuwa benki pekee nchini yenye hazina ya
wateja wengi kuliko benki zingine zilizopo nchini.
0 comments:
Post a Comment