Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha
nne Mkoani Simiyu wakiwa katika picha ya pamoja na Naibu Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu,
Mhe. Stella Ikupa, mara baada ya kambi ya kitaaluma ya siku 60 kwa
wanafunzi hao kuhitimishwa Oktoba 30, 2019 Mjini Bariadi.
Baadhi ya viongozi wakifuatilia
kitu wakati wa kufunga kambi ya kitaaluma ya siku 60 kwa wanafunzi wa
kidato cha nne Oktoba 30, 2019 Mjini Bariadi , kutoka kulia walioketi
mbele, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt Hassan Abbas, Katibu wa CWT Taifa,
Mwl. Deus Seif na Mbunge la Afrika Mashariki, Mhe. Happyness Lugiko.
Baadhi ya wanafunzi wa Kidato cha
nne kutoka shule mbalimbali mkoani Simiyu, wakimsikiliza Naibu Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia masuala ya watu wenye
ulemavu, Mhe. Stella Ikupa, wakati wa kufunga kambi yao ya kitaaluma ya
siku 60 Oktoba 30, 2019 Mjini Bariadi.
***************************
Na Stella Kalinga, Simiyu RS
Naibu Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia masuala ya watu wenye
ulemavu, Mhe. Stella Ikupa, amefunga rasmi kambi ya kitaaluma kwa
wanafunzi wa kidato cha nne Mkoani Simiyu, ambapo amewapongeza viongozi
wa mkoa wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka kwa ubunifu
huo ambao utawasaidia wanafunzi hao kufanya vizuri katika mitihani yao.
Naibu Waziri
Ikupa ameyasema hayo Oktoba 30, 2019 wakati wa kuhitimisha kambi ya
kitaaluma ya wanafunzi wa kidato cha nne ambayo imefanyika kwa muda wa
siku 60 katika Shule ya sekondari Simiyu na Chuo cha Ualimu Bariadi
Mjini Bariadi, kwa lengo la kuwaandaa na mtihani wa Taifa unaotarajia
kufanyika kuanzia Novemba 04, 2014.
“Nampongeza
Mkuu wa Mkoa kwa ubunifu mkubwa wa kuandaa kambi hizi kwani,
naamini wanafunzi mmejifunza mambo mengi na mtafanya vizuri katika
mtihani wenu, ningeshauri watu wengine waige jambo hili, niwakumbushe
wanafunzi mtakaoanza mtihani wenu Novemba 4, 2019, kumuomba Mungu ili
awaongoze kipindi chote cha mitihani,” alisema Ikupa.
Aidha, Ikupa
amesema Serikali imeendelea kuboresha sekta ya elimu nchi kwa kuongeza
bajeti katika shule, kujenga madarasa, na anaamini kuwa itaendelea
kutatua changamoto ya walimu katika mkoa wa Simiyu, na nchini kwa
ujumla.
Mkuu wa Mkoa
Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema uongozi wa Mkoa, walimu, wazazi na
wadau wote wa elimu mkoani humo wamefanya uwekezaji mkubwa kwa wanafunzi
wote waliokuwa katika kambi za kitaaluma na kupitia kazi nzuri
iliyofanywa na walimu anaamini kwamba watafanya vizuri katika mtihani wa
Taifa utakaoanza Novemba 4, 2019.
Ameongeza
Serikali mkoani Simiyu itaendelea kuwapa motisha walimu, wanafunzi na
shule zote zitakazofanya vizuri katika mitihani ya Kitaifa, huku
akiahidi kuwalinda walimu wote, ambapo ameahidi kuwa kuanzia Desemba
Mosi, 2019 viongozi wa mkoa watawatembelea walimu katika Halmashauri
zote na kuzungumza nao.
Mkurugenzi wa
Idara ya Habari- MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas
amewaomba wadau kuendelea kuunga mkono kambi hizi ili waweze kutimiza
ndoto zao huku akibainisha kuwa kupitia kambi hizo watapatikana viongozi
mahiri wa baadaye.
Katibu Mkuu,
Chama cha Walimu Tanzania, Deus Seif amesema walimu wana imani na
Serikali na wameamua kufanya kazi yao kwa bidii na wanaiomba Serikali
kuendelea kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo
kupandishwa madaraja na mishahara kwa wakati na malipo ya fedha za
likizo na malimbikizo ya mishahara.
Naye Afisa
Elimu wa Mkoa, Mwl. Ernest Hinju amesema tangu kambi hizi zianze mwaka
2016 zimesaidia kuongeza kiwango cha ufaulu katika matokeo ya darasa la
saba, kidato cha nne na kidato cha sita, ambapo kwa kidato cha nne
mwaka 2017 ufaulu ulikuwa 70.68% na mwaka 2019, ufaulu umekuwa 86.46%.
Naye Diana
Boniphace mwanafunzi kutoka Shule ya sekondari Kidinda amesema, “kupitia
kambi hii wanafunzi tumejifunza mambo mengi kupitia kwa walimu mahiri
na kiwango cha ufaulu kimeongezeka tofauti na tulivyoingia hivyo
tunaahidi kuwa tutafanya vizuri katika mtihani wa Taifa tutakaoanza
Novemba 04, 2019.”
Kambi ya
Kitaaluma iliyohitimishwa Oktoba 30, 2019 ilihusisha wanafunzi 1512
ambao walikuwa na ufaulu hafifu(daraja sifuri), wanafunzi waliofanya
vizuri katika mtihani wa Mkoa(Mock) na wanafunzi kutoka shule zenye
wanafunzi chini ya 30 na wamekaa kambini siku 60.
0 comments:
Post a Comment