WAZIRI Mkuu Kassim
Majaliwa amefanya ziara katika hospitali ya wilaya ya Ruangwa na amekabidhi
magari mawili ya kubebea wagonjwa.
Amesema kati ya
magari hayo moja ni kwa ajili ya hospitali hiyo ya wilaya na la pili
litapelekwa katika kituo cha afya cha Mandawa.
Waziri Mkuu
amekabidhi magari hayo leo (Jumatano, Julai 12, 2017), alipotembelea hospitali
hiyo, ikiwa ni siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi Mkoani Lindi.
Amesema magari hayo
ni muendelezo wa mkakati wa Serikali ya awamu ya tano wa kuboresha huduma za
afya kwa wananchi wake.
“Rais wetu Dkt.
John Magufuli amedhamiria kuwaondolea wananchi kero mbalimbali zinazowakabili
zikiwemo za huduma za afya, hivyo tuendelee kumuunga mkono.”
Waziri Mkuu amesema
magari hayo ya kisasa yatasaidia kurahisisha usafiri kwa wagonjwa
wanaohitaji matibabu ya dharura katika hospitali kubwa.
Kabla ya
kukabidhi magari hayo, Waziri Mkuu alitembelea wodi ya akina mama
na ya watoto waliolazwa katika hospitali hiyo na amesema kwamba
ameridhishwa na hali ya utoaji huduma.
Kwa upande wake,
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Mheshimiwa Rashid Nakumbya
amesema magari hayo ni faraja kwao kwa kuwa walikuwa na changamoto ya usafiri
kwa wagonjwa wa dharura.
“Tunatambua na
kuthamini jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano katika
halmashauri yetu na Taifa kwa ujumla, nasi tutayatumia magari haya kama
ilivyokusudiwa.”
Awali, Mganga Mfawidhi
wa Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa, Dkt. Regan Rajuu amesema hali ya upatikanaji
wa dawa na vifaa tiba katika hospitali hiyo umeongezeka kutoka asilimia 80
Desemba, 2016 na kufikia asilimia 90 Juni 2017.
Pia Waziri Mkuu
alitembelea shule ya Sekondari ya Kassim Majaliwa iliyoanza kujengwa Desemba,
23, 2016 kwa michango ya Halmashauri, fedha za mfuko wa jimbo pamoja na wadau
mbalimbali wa maendeleo.
Kaimu Mkuu wa shule
hiyo, Mwalimu Emmanuel Sechawe alisema msingi wa kuanzisha shule hiyo ulitokana
na uwepo wa wanafunzi 319 waliofaulu darasa la saba mwaka 2016 kukosa nafasi ya
kujiunga na kidato cha kwanza katika shule zilizopo.
0 comments:
Post a Comment