METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, July 13, 2017

MWAKA MMOJA WA MKURUGENZI WA MANISPAA YA UBUNGO NDG JOHN LIPESI KAYOMBO MADARAKANI NA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU

 
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo (Pichani) akiwa ametimiza mwaka mmoja tangu alipopewa dhamana ya kuwatumikia wananchi wa Ubungo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli akiongea na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri, Miji, Manidpaa na Majiji 185 kabla ya hawajala kiapo cha maadili ya viongozi leo Ikulu jijini Dar es salaam.(Picha na Makataba-Ikulu) 


Imeandaliwa na Mathias Canal

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo pamoja na wakurugenzi  watendaji  185 wa Majiji, Manispaa, Miji na Halmashauri za Wilaya, leo Julai 13, 2017 wamefikisha mwaka mmoja wakiwa madarakani kutekeleza dhima ya serikali ya awamu ya tano kupitia ilani ya ushindi ya Chama cha Mapinduzi CCM ya Mwaka 2015.
 
Hafla ya Kiapo cha Uadilifu wa Utumishi wa umma kwa Wakurugenzi Watendaji wa Majiji, Manispaa, Miji na Halmashauri nchini, iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Wakurugenzi watendaji wote waliaswa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kufanya kazi kwenye maeneo yao mapya waliyopangiwa kwa kuzingatia uadilifu, uwajibikaji na uaminifu.

Katika utekelezaji na kuondoa kero ya wananchi Manispaa ya Ubungo inayoongozwa na Mkurugenzi Ndg john lipesi kayombo  ameanzisha Programu maalumu ya kusikiliza kero  mbalimbali za wananchi na kuzitatua ikiwemo Migogoro inayohusu kadhia ya Ardhi ambayo kwa kiasi kikubwa imesikilizwa na kutatuliwa.

kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya wananchi kwani wamechoshwa na kero hasa kwenye ushuru na kodi zisizo za lazima, akitolea mfano mkulima wa mchicha na mpunga kutozwa kodi wakati amelima kwa ajili ya chakula chake ya kwamba hili jambo halikubaliki.

“Katika Mwaka mmoja huu tumefanya kazi kubwa katika Manispaa ya Ubungo ili kuitafsiiri kwa vitendo dhima na Imani kubwa kwa Rais aliyotupatia kwa kututeua kwani tunaamini uteuzi ulifanywa kwa umakini mkubwa vivyo hivyo nasi tunafanya kazi kwa umakini mkubwa ili na kuongeza ufanisi wa utatuzi wa kero za wananchi” Alisema Mkurugenzi Kayombo

“Katika kipindi hiki cha mwaka mmoja kwa kushirikiana na wakuu wa idara na vitengo tumehakikisha tunakuwa watumishi wa watu na si watawala wa watu kwa kuzingatia uwajibikaji, uadilifu na uaminifu” Alisisitiza Mkurugenzi Kayombo

TAZAMA UTEKELEZAJI WA UTENDAJI KAZI NA BAADHI YA MIRADI YA MAENDELEO KATIKA HALMASHAURI YA MANISPAA YA UBUNGO ULIOFANYIKA KATIKA KIPINDI CHA MWAKA MMOJA WA UONGOZI WA MKURUGENZI KAYOMBO

1.  KITUO CHA AFYA MBEZI

Mradi wa jengo la kituo cha huduma kwa wanaoishi na virusi vya Ukimwi(CTC). Jengo hilo lina vyumba 8 na vyoo 2 ambapo mchanganuo wake ni chumba 1 cha Daktari, chumba cha taarifa(data room),chumba cha kuchukulia sampuli (Phlebotomy),chumba cha Stoo,chumba cha Dawa(pharmacy),chumba cha Ushauri Nasaha (counseling room),chumba cha Daktari Mfawidhi na chumba cha Muuguzi. Jengo hili limegharimu kiasi cha Tshs 125 milioni ambazo zimetolewa na wafadhili ambao ni MDH (Management and Development for Health) 

2.  KITUO CHA POLISI CHA KATI – GOGONI KATA YA KIBAMBA 

Ujenzi wa kituo cha polisi cha kati  kwa nguvu za wananchi na wadau mbalimbali waliopo nje ya mtaa wa Golani kutokana na kukithiri kwa uhalifu katika mtaa. Michango ya wananchi ni Tsh.53,000,000/= na NSSF imechangia Tsh. 50,000,000/= sawa na jumla ya Tsh. 103,000,000/=. Eneo la ujenzi kituo cha polisi linaukubwa wa ekari  moja (o1) ambapo Jengo la kituo cha polisi linakusudiwa kuwa na vyumba 13, vyumba vitatu ni kwa ajili ya maabusu ya wanaume, wanawake na watoto zenye vyoo vya ndani, vyumba vya ofisi na vyoo 4.

Matarajio ni kuwa kituo hicho cha polisi Gogoni kikimalizika na kufunguliwa kitapunguza uhalifu kwa kiasi kikubwa katika mtaa, kata na Wilaya ya Ubungo kwa ujumla. 

3.   MADARASA NANE  SHULE YA MSINGI MALAMBAMAWILI
 

Ujenzi wa Jengo lenye madarasa nane (8) ambayo yamejengwa kwa fedha kutoka Serikali kuu kwa  gharama ya Shilingi Milioni mia moja na thelethini na sita (Tshs 136,000,000/=). Na kuifanya shule hiyo kuwa na vyumba vya madarasa 24. Dhumuni kubwa la mradi huo ni kupunguza msongamano mkubwa wa wanafunzi katika darasa moja kutoka uwiano wa darasa moja kwa wanafunzi 234 (1:234) uliokuwepo awali  na kuwa uwiano wa darasa moja kwa wanafunzi 156 (1:156). Vile vile utaratibu wa wanafunzi kusoma kwa kupishana asubuhi na wengine jioni (double session) utakuwa umepungua na kubaki kwa darasa la I & II tu.

4.   KITUO CHA MABASI SIMU 2000 (SINZA)
  

Mradi wa kituo cha mabasi SIMU 2000 uliopo kata ya Sinza. Ujenzi wa mradi huo ulijumuisha ujenzi wa kituo cha kuegesha magari (kituo cha daladala), ujenzi wa kituo cha polisi na ujenzi wa choo. Lengo kuu la kuanziasha mradi huo lilikuwa ni  kurahisisha upatikanaji wa usafiri kwa wananchi kuelekea sehemu mbalimbali za jiji la Dar es salaam na nje ya mkoa.  Ujenzi huu wa mradi wa  simu 2000 ulianza kufanya kazi  tarehe 23 /10/2014 kikiwa na mabasi (daladala)  

5.   UJENZI WA JENGO LA ZAHANATI YA MBURAHATI

Uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa jengo la zahanati ya mburahati katika eneo la mtaa wa NHC  Kata ya mburahati. Mradi huo unatarajiwa kuhudumia zaidi ya wananchi elfu 30,000 walioko katika Kata ya Mburahati na mitaa yake Barafu, Kisiwani na NHC na kata zinazozunguka eneo hilo kama Kata za Mabibo,Makurumla na Kigogo. Mradi huu wa ujenzi wa zahanati  ulianza kutekelezwa tangu Juni 2014 na kukamilika mnamo Oktoba 2016 chini ya Manispaa ya Ubungo, kwa gharama ya kiasi cha Tshs 84,000,000.00.  

6.   KUANZA UJENZI WA BARABARA YA KWENDA SHULE KUU YA SHERIA TANZANIA
 
Kuanza Ujenzi wa barabara inayotoka Mawasiliano kuelekea Shule kuu ya Sheria (Law school Of Tanzania) iliyopo katika Kata ya Sinza Jijini Dar es salaam. Matengenezo hayo yataanza hivi karibuni ili kurahisha huduma za kijamii kwa watumiaji wa barabara hiyo wakiwemo wananchi wa Mtaa wa Mawasiliano na Kata ya Sinza sambamba na wanafunzi wa Shule ya Sheria.

7.   KUANZISHWA KWA REJESTA YA WAKAZI KWA KILA MTAA 
 
Kuanzishwa kwa Daftari la Rejesta ya Wakazi wa Mtaa ambapo pamoja na kuanzishwa kwa Daftari la Rejesta ya wakazi wa Mtaa pia kutakuwa na Fomu ya Rufaa ya Malalamiko katika kila Mtaa sambamba na kitabu cha kutunza kumbukumbu za kusikiliza malalamiko ya wananchi katika Ofisi za serikali.

Tayari vitabu hivyo vyote vimepelekwa katika kila Mtaa ili kuanza utekelezaji wa zoezi hilo haraka iwezekanavyo.

8.   UJENZI WA DARAJA LA MBEZI MSUMI 
 
Kuanza kujengwa kwa daraja  jipya kutokana na kuharibika kwa daraja la awali katika eneo la Msumi Kata ya Mbezi Jijini Dar es salaam. Draja hilo litaondoa adha iliyopo katika daraja hilo ambapo sio ubovu wa miundombinu pekee bali pia ni swala la usalama hasa kwa watoto wanaopita katika daraja hilo waendapo shuleni na sehemu mbalimbali.

Daraja lililokuwa limejengwa awali lilikuwa Dogo ukilinganisha Na wingi wa Maji Jambo lililopelekea kuharibika haraka kwa daraja hilo. Ungenezaji wa daraja hilo utaanza hivi karibuni na matarajio ni kufikia mwaka 2018 liwe limeanza kutumiwa Na wananchi hao ambao wamepata adha kubwa kwa muda mrefu.

9.   UJENZI WA MADARASA MATANO MAPYA SHULE YA MSINGI HONDOGO KATA YA KIBAMBA 

Kuanza ujenzi wa madarasa matano katika shule ya Msingi Hondogo iliyopo katika Kata ya Kibamba Jijini Dar es salaam, Ujenzi huo unaanza kutokana na kuwapo na ubovu wa madarasa hivyo kuamua kujenga madarasa mengine mapya matano kwa ajili ya wanafunzi kujisomea kwa uhuru na amani shuleni hapo. Ujenzi huo utagarimu shilingi milioni 85

Ujenzi huo utakaoanza hivi karibuni wa vyumba vitano vya madarasa utaakisi pia ujenzi wa vyumba vya madarasa nane na matundu ya vyoo katika Shule ya Msingi Ubungo Plaza, vivyo hivyo katika Shule ya Msingi Kawawa na Shule ya Sekondari Mburahati ambapo kote huko ameelekeza kuanza haraka ujenzi wa Madarasa sambamba na Vyoo kwa ajili ya wanafunzi na walimu.

Mara baada ya kukamilika kwa madarasa hayo yatapunguza kadhia ya mbanano wa wanafunzi darasani ambapo pia amesema ujenzi wa madarasa hayo utakuwa wa kisasa ili kukidhi mahitaji ya ubora wa majengo ya serikali.

10.   UJENZI WA MADARASA MANNE NA VYOO VYA SHULE YA SEKONDARI MBURAHATI

Mchakato wa ukamilisho wa ujenzi wa Madarasa manne katika shule ya Sekondari Mburahati iliyopo Katika Mtaa wa Barafu, Kata ya Mburahati Jijini Dar es salaam kuanza hivi karibuni. Sambamba na kujengwa vyoo vya wanafunzi kutokana na uchache wa vyoo vilivyopo ili kukabiliana na wingi wa wanafunzi.

Shule ya Sekondari Mburahati ni shule ya kutwa iliyoanzishwa mwaka 2010 ambapo pamoja na kuwa na wanafunzi wengi ina jumla ya vyumba vya madarasa 9 huku mahitaji yakiwa ni vyumba 25 hivyo kupelekea kuwa na upungufu wa madarasa 16.

11.   KUTEKELEZA KAMPENI YA MTI WANGU
 

Kampeni ya MTI WANGU imeendelea kutekelezwa kwa kupanda miti 156 katika shule ya Sekondari Kibwegere iliyopo eneo la Kibwegere Kata ya Kibamba.
Kampeni hiyo yenye  kauli mbiu ya panda miti tunza miti tupate nishati (MTI WANGU) ina lengo la kuhifadhi mazingira,  kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi pamoja na majanga asilia kama upepo mkali, mmomonyoko wa udongo, maporomoko ya  ardhi na mafuriko.

12.   OPERESHENI YA KUSHUSHA MABANGO AMBAYO HAYAJALIPIWA KODI

Kuanza Operesheni ya kusimamia zoezi la ushushaji wa Mabango ambayo hayajalipiwa katika maeneo mbalimbali ndani ya Manispaa lengo ikiwa ni kuwakumbusha kwa njia ya vitendo wadaiwa hao ambao wamefunga masikio kwa kipindi kirefu.

Zaidi ya mabango 25 yatashushwa ambapo tayari mabango Tisa yameshushwa ambayo yapo chini ya kampuni tatu ambazo ni Kampuni ya A1 Outdoor, Masoko Agency na kampuni ya Apple Media.
Kampuni zingine zinazodaiwa Kodi ni pamoja na M1 Outdoor, SkyOutdoor, Brooklyn Media, Loft Media, Lable Promotion, EF Outdoor, Milestone International, JCD Decaux, Spark Venture, Brand Active, Global System, na TBL Tanzania Ltd.

Kampuni zingine ni Goba Petrol Station, Oil Link, Lake Oil, Camel Oil, CRDB Bank PLC, Access Bank, Tanzania Distillers, Sadoline, UDART, na Equity Bank Tanzania LTD.

Ambapo Jumla ya Shilingi 644.428.994.00 zinadaiwa kutoka katika kampuni hizo huku mdaiwa wa Deni kubwa ikiwa ni kampuni ya A1 Outdoor inayodaiwa Jumla ya Shilingi 273,000,000.00

13.   USIMAMIZI WA ULIPAJI KODI KATIKA KITUO CHA DALADALA CHA SIMU 2000

Kusimamia uwajibikaji na ukusanyaji mahususi wa mapato katika Kituo Cha Mabasi Simu 2000 kilichopo Kata ya Sinza. Awali kulibainika kutotolewa risiti ambapo Jambo Hilo limetajwa kuwa ni moja ya sababu ya kupatikana mapato kiduchu ukilinganisha na huduma zinazotolewa Kwa wananchi.


Mara baada ya kuwa na usimamizi madhubuti mapato yameongezeka kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na awali

14.   KUSAINI MIKATABA YA KAZI MBALI MBALI YENYE JUMLA YA SHILINGI BILIONI 4 NA MAKAMPUNI YA UJENZI, BARABARA NA WAZABUNI 29




Kusainiwa mikataba ya kazi mbali mbali na makampuni ya Ujenzi, Barabara na Wazabuni 29 Ambapo kati ya makampuni mengi yaliyoomba kazi ni Makampuni 14 pekee ndio yaliyokidhi vigezo na kupewa kazi za Billioni 3.2 kwa kazi ya kusafisha barabara na mazingira yote ya Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo ili kuifanya Halmashauri ya Ubungo kuwa katika Hali ya usafi.Mikataba kazi hiyo ipo katika makundi matatu ambayo ni miradi ya Maji, Barabara na usafi.

Katika makubaliano hayo jumla ya Shillingi Millioni 400 zimesainiwa kwa ajili ya uchongaji wa barabara za Mitaa mbalimbali ya Halmashauri na Shilingi Millioni 200 Ni kwa ajili ya Miradi ya upelekaji wa maji katika kata za Mbezi na Mabibo.

Kiasi kingine cha shillingi Millioni 200 ni kwa ajili ya Ukarabati mfumo wa maji Hospitali ya Sinza na ujenzi wa madarasa ya shule ya Sekondari ya Matosa sambamba na Nyumba sita za walimu zilizopo Kata ya GOBA.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo amefanya ukaguzi wa eneo kwa ajili ya Maonesho ya Kilimo (Nane Nane) ili kujiridhisha na kutoa maelekezo ya maandalizi kwa kufyeka majani yaliyopo katika eneo la JKT Mtaa wa Nanenane ikiwa ni hatua za ufanisi kwa ajili ya kuelekea Maonesho ya Nane Nane mwanzoni kwa mwezi Agosti.

15.   KUNUNUA SHAMBA MKOANI MOROGORO LITAKALOKUWA LINATUMIKA KWA AJILI YA MAONESHO YA NANENANE

Manispaa ya Ubungo imenunua shamba Mkoani Mororgoro lenye ukubwa wa Mita za Mraba 3600 ambalo limegharimu shilingi Milioni 8.25 litakalotumika kwa ajili ya Maonesho ya Sikukuu ya Wakulima (Nanenane)

Tayari Afisa Kilimo na Afisa Mifugo na Uvuvi wa Manispaa ya Ubungo wamemaliza usafishaji wa shamba hilo ambapo tayari mazao mbalimbali yamepandwaa kwa ajili ya Maonesho ya Kilimo Nane Nane.

Pia vimenunuliwa viuatilifu kwa ajili ya kuua wadudu waharibifu na magonjwa, kuandaa mabango na kuainisha aina mbalimbali za malisho iliyooteshwa na kujenga bwawa la samaki. Na kuanza kukusanya bidhaa za mazao mbalimbali ya wafugaji, wakulima na wavuvi watakaoshiriki Maonesho hayo ya Kilimo Nane Nane kwa ajili ya kuyapeleka Morogoro.

16.  KUANZISHWA KWA KITUO CHA UKUSANYAJI KODI NA TOZO MBALIMBALI KATIKA KITUO CHA DALADALA SIMU 2000

Katika kuhakikisha ukusanyaji wa mapato Unaongezeka, Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo imesogeza huduma karibu ya ulipaji ushuru na tozo mbalimbali zinazotozwa na Manispaa ya Ubungo.

Uanzishwaji wa kituo hicho utarahisisha kata ambazo zipo karibu na eneo hilo la Mawasiliano kupata huduma za kulipa ushuru na tozo mbalimbali katika kituo hicho pasipo kwenda makao makuu ya Manispaa hiyo Kibamba CCM.

Kata ambazo zitanufaika ni Sinza , Manzese, Mabibo , Mburahati Ubungo , Kimara na Makuburi ambazo awali wakazi wake walilazimika kufunga safari hadi Kibamba CCM kufuata huduma hizo.
Mstahiki Meya pia baada ya kukagua ofisi amehaidi kuwa ameona changamoto ya ofisi ni ndogo hivyo bajeti ijayo itajengwa ofisi mpya ili kuwezesha watumishi kupata sehemu nzuri ya kutoa huduma kwa wananchi wa ubungo.

Kituo hicho kinatumia mfumo wa kielektronic ujulikanao ‘ Local Government Revenue Collection Information System’ambao unawezesha kutoa huduma za ukusanyaji wa kodi na tozo mbalimbli kwa haraka pasipo kupoteza mapato hivyo kutokana na uwepo wa kituo hicho ambacho ofisi yake imefunguliwa kitawezesha kuongeza Mapato ya Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.

IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA HABARI NA UHUSIANO 
HALMASHAURI YA MANISPAA YA UBUNGO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com