Watumishi wa Hospitali ya sinza wakimsikiliza kwa makini Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Jijini Dar es salaam Mhe Kisare Makori alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wote wa Hospitali hiyo
Mkurugenzi wa
Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo akisalimiana na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Dkt Grace Magembe mara baada ya kuwasili katika Hospitali ya Sinza
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Jijini Dar es salaam Mhe Kisare Makori amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo kumchukulia hatua za kinidhamu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Sinza Dkt Christin Kayola kwa kushindwa kutekeleza vyema majukumu yake sambamba na kutosimamia vyema nidhamu kwa watumishi wengine ya huduma kwa wagonjwa wanaofika kutibiwa Hospitalini hapo.
Agizo Hilo limetolewa na Mheshimiwa Makori wakati wa ziara ya kushtukiza katika Hospitali hiyo ikiwemo kujionea hali ya utoaji huduma kwa wagonjwa.
Wengine waliotakiwa kuchukuliwa hatua kwa kushindwa kuwajibika ipasavyo ni pamoja na wauguzi wanne akiwemo Ndg Celestina Issango, Theopister Kipanga, Felix Lucas na Elinaza Sendoro.
Akizungumza kabla ya kutoa agizo hilo Mhe Makori alisema kuwa watumishi wa Umma wanapaswa kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia miiko na maadili ya utu na kazi.
Alisema dhima ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli ni kuwahudumia wananchi kwa ufanisi na weledi mkubwa pasina kubagua makabila yao, Jinsia zao Wala dini zao.
Mhe Makori alisema kuwa Watumishi wote katika ngazi yoyote ile kushindwa kuwajibika ni kuitafsiri na kuirudisha nyuma dhima ya Rais Magufuli ya kuwahudumia wanachi wanyonge.
Amesema kuwa taaluma ya afya inahusu huduma ya maisha ya watu hivyo katika kuwahudumia ni lazima kuwa na utu na moyo wa kujitoa kwa maslahi ya serikali na nchi kwa ujumla wake.
Mhe Makori ameagiza pia kufanyiwa uchunguzi wa vifo vya watoto wawili vilivyotokea hivi karibuni katika Hospitali hiyo na kuzua sintofahamu kwa wananchi kutokana na kuandikwa kwenye vyombo vya habari.
Sambamba na hayo pia Mhe Makori aliagiza watumishi wote katika Hospitali hiyo ya Sinza kuwa na kauli nzuri kwa wagonjwa kuanzia wanapofika getini mpaka wanapofika kuwaona wauguzi ama madaktari.
Pia aliagiza uongozi wa Hospitali hiyo kuwa na usimamizi mzuri katika kila eneo na kuwa na mtu mmoja atakayeweza kuzungumzia baadhi ya Mambo yahusuyo taarifa mhalimbali za kituo sio kila mtu kuongea pasina weledi na nakubaliano na uongozi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo ametoa onyo kwa katibu wa afya katika kituo hicho kuacha haraka iwezekanavyo kutoa kauli za kuudhi dhidi ya wagonjwa.
Hata hivyo Mkurugenzi Kayombo tayari amechukua hatua za kinidhamu kwa watumishi wote hao watano waliofikishwa katika Kituo cha Polisi Urafiki kutoa maelezo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA MKUU WA WILAYA YA UBUNGO
0 comments:
Post a Comment