METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, July 31, 2017

DC MTATURU AWEZESHA UPATIKANAJI WA ZAIDI YA MILIONI 5 KWA AJILI YA KWAYA YA JERUSALEM

Na Mwandishi Wetu, Ikungi

MKUU wa wilaya ya Ikungi mkoani Singida Miraji Mtaturu ameendesha harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia kwaya ya Jerusalem ya kanisa la EPCT Kimbwi lililopo wilayani humo na kuvuka lengo la ukusanyaji lililowekwa.

Kwaya hiyo inahitaji jumla ya shilingi milioni 7,400,000 kwa ajili ya kurekodi video  ambapo kabla ya harambee hiyo wanakwaya hao walifanikiwa kuchanga shilingi milioni 3  ambapo lengo la kufanya harambee hiyo ni ili wakusanye  shilingi milioni 4,400,000 lakini wamefanikiwa kuchangisha shilingi milioni 5,169,500 kati ya hizo shilingi milioni 3 ikiwa ni ahadi ya mkuu wa wilaya Mtaturu.

Akizungumza katika harambee hiyo Mtaturu aliwapongeza kwa kuanza kuchanga wenyewe kiasi hicho kwa kuwa kimeonyesha dhamira njema waliyonayo na kuwaasa waumini hao kushirikiana kwa pamoja katika kuilinda amani iliyopo kwa kutokubali kugombanishwa au kugawanywa na watu wasio na dhamira njema.

“Ndugu zangu tofauti zetu za vyama isituondoe kwenye tabia yetu ya asili ya kushirikiana kwenye maendeleo,tumuunge mkono rais wetu dokta John magufuli kwa kuwa ameonyesha nia njema aliyonayo ya kuwaondoa watanzania kwenye umaskini kwa kusimamia rasilimali za nchi na hiyo itasaidia uboreshaji wa huduma katika jamii,”alisema Mtaturu.

Alisema katika kumuunga mkono rais Magufuli wilaya imeamua kuja na kampeni ya kulima korosho ili kukuza uchumi wa wananchi ambapo watagawa bure miche ya mikorosho ili wananchi waandae mashamba mapema na kuahidi uwepo wa soko la zao hilo kwa bei nzuri.
 

Alilipongeza kanisa kwa kuendelea kuwaandaa waumini wake kiroho na kuboresha huduma za kijamii,elimu,afya na maji kwa kushirikiana na serikali na kuwashukuru wote waliomuunga mkono katika harambee hiyo kwa kuwa wamemkopesha Mungu na yeye ndio atakayewalipa kwa moyo wao huo.

Katika harambee hiyo kiasi cha shilingi milioni 1,454,500 kilitolewa taslimu na ahadi ni shilingi milioni 3,715,00 ambapo mkuu wa wilaya huyo aliwataka wote waliotoa ahadi kuhakikisha hadi agosti 30 wawe wamekamilisha ahadi zao ili septemba mosi vijana hao wa kwaya waende kurekodi video yao na septemba 15 waizindue.

Akisoma risala kwa mgeni rasmi Easter Richard alimshukuru mkuu huyo kwa kukubali mwaliko na kumpongeza kwa kazi nzuri za kuhamasisha na kusimamia maendeleo katika wilaya ya Ikungi kwa muda mfupi alipoteuliwa kuwa mkuu wa wilaya.

 
“mkuu wetu wa wilaya unafanya kazi nzuri,ushahidi ni huu miezi miwili iliyopita ulitembelea Zahanati ya kijiji cha Kimbwi na kukuta nyumba ya mganga wa zahanati haijakamilika ambayo ilitakiwa ipewe milioni 20 lakini ilikuwa imetoka milioni 10 na ukaagiza pesa yote iletwe na ikaletwa na sasa nyumba imekamilika na watumishi wameshahamia,ahsante sana mkuu,”alishukuru Easter.

Naye mwenyekiti wa kijiji cha Kimbwi Julius Iyunde akizungumza katika harambee hiyo alimshukuru mkuu huyo kwa kuwapelekea Solar wakati alipoenda kutembelea Zahanati na kumpa kero hiyo na kusema kwa sasa tayari wameshafunga na huduma zinaendelea kutolewa vizuri.

Akitoa neno la shukrani mama mchungaji Basilisa Mathayo alisema kupitia harambee hiyo wameona muujiza kwa mtumishi ambaye ni mkuu wa wilaya kwak uwa harambee imekwenda vizuri na kumuombea yeye pamoja na  rais Magufuli ili Mungu amuongoze katika kuwatumikia watanzania.

Kwaya ya Jerusalem ilianzishwa mwaka 1998 ikiwa ni miongoni mwa kwaya tatu zilizopo katika kanisa hilo ikiwa inafanya kazi ya kupeleka injili kwa njia ya uimbaji ambapo mpaka sasa wamesharekodi CD za Audio 3 na malengo ya baadae mwaka huu ni kutoa video.

Mwisho.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com