WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa
WAZIRI MKUU, Kassim
Majaliwa amesema Serikali imeweka mikakati mizuri kuhakikisha wananchi hususani
wachimbaji wadogo wadogo wananufaika na uwepo wa rasilimali hiyo.
Hivyo, Waziri Mkuu
amewashauri wachimbaji wadogo wadogo wajiunge katika vikundi ili Serikali iweze
kuwapatia misaada mbalimbali ikiwemo mkopo ili waongeze mitaji.
Waziri Mkuu ameyasema hayo
leo (Alhamisi, Novemba 29, 2018) alipozungumza na wananchi baada ya kuweka jiwe
la msingi la ujenzi jengo la halmashauri ya Mbogwe.
Amewahamasisha wachimbaji
hao watumie taasisi mbalimbali za kifedha na kukopa fedha na kununua mitambo ya
uchimbaji na uchenjuaji kwa lengo la kujiongozea tija.
Waziri Mkuu ambaye yuko
mkoani Geita kwa ziara ya kikazi, amesema wachimbaji wadogo wadogo waendelee
kuwa na imani na Serikali yao, kwa kuwa imewapangia mambo mazuri.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewahakikishia wananchi wa wilaya hiyo kwamba Serikali
imedhamilia kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.
Amesema katika kumaliza
tatizo la maji Serikali imetoa zaidi ya sh. bilioni moja kwa ajili
ya uchimbaji visima virefu 11 na visima vifupi 43 katika maeneo
mbalimbali ya wilaya hiyo.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano ina mikakati ya kumaliza
tatizo la maji nchini kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John
Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani.
Waziri Mkuu amesema kampeni
hiyo inalenga kuhakikisha wananchi katika maeneo yote wanapata huduma ya maji
safi na salama karibu na maeneo yao ya makazi.
“Serikali imedhamiria
kuhakikisha wananchi wote nchini wakiwemo na wa wilaya ya Mbogwe wanapata
huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yao.”
Kuhusua suala la wanafunzi
kukatishwa masomo kwa kupata ujauzito wilayani Mbogwe, Waziri Mkuu ameitaka
jamii kukemea vitendo hivyo. Wanafunzi 54 wamepata ujauzito.
Amesema katika kipindi cha
kuanzia mwezi Januari hadi Septemba mwaka huu wanafunzi 20 wa shule za msingi
na 34 wa sekondari wameacha shule baada ya kupata ujauzito.
“Hali ni mbaya, Mbogwe
inatia aibu kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto waliopewa ujauzito. Naagiza
msiwaguse wanafunzi wa kike ni moto utawaunguza. Tukikukamata jela miaka 30.”
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko amesema wilaya ya Mbogwe inafanya
vizuri katika sekta ya madini, ambapo ina viwanda 27 vya kuchenjulia dhahabu.
Amesema katika kuhakikisha
wachimbaji wadogo wadogo wanawezeshwa kufanya shughuli zao vizuri, Serikali
imetenga eneo la hekta 547.64 kwa ajili ya kuwagawia wachimbaji hao.
Akizungumzia kuhusu leseni
za uchimbaji mkoani Geita amesema kuna jumla ya leseni 971 za uchimbaji mdogo
wa madini na kati yake zinazofanyakazi ni leseni 184 tu.
Waziri huyo amewataka
wachimbaji wadogo wadogo waendelee na shughuli zao za uchimbaji kwenye maeneo
yao waliyopangiwa na kwamba hakuna atakayewaondoa.
Awali, Waziri Mkuu alikagua na kuweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa
ofisi ya halmashauri ya wilaya ya Mbogwe katika kijiji cha Kasosobe. Ujenzi huo
utagharimu sh. bilioni 4.3. Pia alikagua mradi wa uboreshaji miundombinu na
kuzindua maabara ya Kituo cha Afya Masumbwe.
0 comments:
Post a Comment