Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mkurugenzi wa UNESCO Kanda ya Afrika Bi. Ann Therese NDONG-JATTA pamoja na Mwakilishi Mpya wa UNESCO nchini Tanzania Bw. Tirsa A.S Dos Santos ofisini kwa Makamu wa Rais, Ikulu jijini Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi wa UNESCO Kanda ya Afrika Bi. Ann Therese NDONG-JATTA (kushoto) na Mwakilishi Mpya wa UNESCO nchini Tanzania Bw. Tirsa A.S Dos Santos (kulia) ofisini kwa Makamu wa Rais, Ikulu jijini Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Samia Suluhu Hassan leo amekutana na kufanya mazungumzo kwa nyakati
tofauti na Balozi wa Italia nchini Mhe. Roberto Mengoni, Balozi wa Falme za
Kiarabu nchini Mhe. Khalifa Abdulrahman Mohamed Al-Marzooqi pamoja na
Mkurugenzi wa UNESCO Kanda ya Afrika Bi. Ann Therese NDONG-JATTA ambaye
alimtambulisha Mwakilishi mpya wa UNESCO nchini Tanzania Bw. Tirso A.S Dos
Santos.
Balozi wa Italia nchini Mhe. Roberto Mengoni
amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na kuisaidia Tanzania katika masuala
mbalimbali hususani kwenye sekta ya Elimu ambayo kuna mikataba na Tanzania na
kwenye sekta Afya kupitia taasisi isiyo ya kiserikali ya CUAMM.
Balozi huyo amesisitiza kuwa Italia itaendelea
kusaidia yale mambo ambayo nchi imeyapa kipaumbele.
Balozi Mengoni ameipongeza Serikali kwa kuanzisha
mfumo wa visa na vibali vya ukaazi vya kielektroniki ambao utarahisisha huduma ya upatikanaji wa visa.
Makamu wa Rais amemueleza Balozi huyo kuwa Tanzania
itaendelea kushirikiana na Italia na kuiomba nchi hiyo kupitia taasisi isiyo ya
Kiserikali ya CUAMM kutoa elimu ya lishe bora kwa watoto.
“Tanzania inazalisha chakula kingi
sana ukitembea huko vijijini watu wanalima sana lakini lishe bora kwa watoto
bado ni tatizo, kunahitajika elimu zaidi” alisema
Makamu wa Rais.
Makamu wa Rais pia alikutana na Balozi wa Umoja wa
Falme za Kiarabu Nchini Mhe. Khalifa Abdulrahman Mohamed Al-Marzooqi ambaye
alimueleza Makamu wa Rais nia ya kujenga Ofisi za Ubalozi mdogo Zanzibar
mwakani.
Pamoja na mambo mengine Balozi huyo amewataka
Watanzania kuchangamkia fursa katika maonyesho ya kimataifa ya Expo 2020 yatakayofanyika
Dubai.
Kwa upande wake Makamu wa Rais alimueleza Balozi
huyo kuwa Tanzania inashukuru kwa ushirikiano mzuri na itaendelea kutoa
ushirikiano katika nyanja mbali mbali.
Mwisho Makamu wa Rais alikutana na Mkurugenzi wa
UNESCO Kanda ya Afrika Bi. Ann Therese NDONG-JATTA ambaye alimtambulisha
Mwakilishi mpya wa UNESCO nchini Tanzania Bw. Tirso A.S Dos Santos.
Mkurugenzi huyo wa UNESCO Kanda ya Afrika
alimueleza Makamu wa Rais mafanikio ambayo UNESCO wameyapata kupitia mradi wake
wa kutoa elimu kwa maeneo yasiyofikika kwa mfumo wa kidijitali, elimu kwa
watoto wa kike, radio jamii pamoja na huduma ya telemedicine ambapo mgojwa
anaweza kupata huduma kwa simu.
“UNESCO imeendelea kutoa semina na
elimu mbali mbali hasa katika Nyanja ya habari ili kuhakikisha watoaji habari
wanatoa habari sahihi” alisema Mkurugenzi huyo.
Kwa upande wake Makamu wa Rais alimpongeza
Mwakilishi mpya wa UNESCO nchini na kumkaribisha, pia ameipongeza UNESCO kwa
ujumla kwa kazi nzuri wanayoifanya Tanzania.
“Ningeomba radio jamii zitoe elimu
zaidi katika kampeni za masula ya ukeketaji, lishe bora kwa watoto na afya ya
mama na mtoto” alisema Makamu wa Rais.
0 comments:
Post a Comment