Wakazi wa Kijiji cha Kakola, Kata ya
Bulyanhulu, Wilaya ya Msalala mkoani Shinyanga wameazimia kufanya
maandamano yasiyo na ukomo kushinikiza mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu
kuwalipa fidia zao.
Wakizungumza kwenye kongamano la Kijiji
hicho lililofanyika jana juni 20,2017, wakazi hao wamepanga kupeleka
kero zao Jijini Dar es salaam kwa Rais John Pombe Magufuli pamoja na
kufanya maandamano ya kufunga barabara kushinikiza kulipwa fidia zao.
“Kongamano la leo ni kumuunga mkono Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Magufuli kwa
kugundua kwamba tulikuwa tunaibiwa kwa muda mrefu. Tangu mwaka 1996
mpaka leo sisi tumeibiwa tu, hatujapata haki hata moja. Hakuna huduma za
jamii zinazotambulika ambazo zimefanywa na mgodi”. Alisema mchimbaji
mdogo Aziz Mbaga.
Mjumbe wa serikali ya Kijiji cha
Bulyanhulu, Mhidini Mfwanguro alisema maazimio ya wananchi wa Kijiji
hicho ni fidia kwa wafukiwa na waathirika wa Bulyanhulu mwaka 1996
pamoja na waathirika wengine wakiwemo wafanyakazi waliochishwa kazi kwa
kuumia kazini bila kulipwa na kwamba watawasilisha madai hayo kwa
wamiliki wa mgodi huo, kampuni ya Barrick Gold Mine.
Mwenyekiti wa kijiji cha Kakola,
Emmanuel Bombeda amesema kijiji hicho kilikuwa na vitongoji tisa lakini
vitongoji vinne vilichukuliwa na mgodi wa Bulyanhulu bila wananchi
kulipwa fidia huku nyumba zao zikibomolewa.
“Tunataka maandamano ya kufunga barabara
tulipwe, siwezi kufanya maandamano halafu tusambae, nataka maandamano
kama tuliyofanya umeme ukaletwa kijiji cha Kakola, maandamano kama yale
ya Musoma ya kupigwa mabomu lakini tulipwe”. Alisema Bombeda.
Diwani wa Kata ya Bulyanhulu, John
Kiganga alikiri wananchi wengi kukosa stahiki zao baada ya kuondolewa
kwenye maeneo yao ili kupisha uwekezaji wa mgodi wa Bulyanhulu na
kusisita kwamba wanapaswa kulipwa fidia zao maana fomu za tathimini zipo
na kwamba hata wale waliolipwa fidia, walilipwa kinyume na tathimini
ambapo mmoja wa wananchi aliyepaswa kulipwa shilingi milioni 375
alilipwa shilingi laki tano.
Wananchi wa Kijiji cha Kakola
wanalalamika kutolipwa fidia zao baada ya maeneo na makazi yao
kuchukuliwa na mgodi wa Bulyanhulu, wengine ndugu zao kufukiwa kwenye
mashimo, waliokuwa wafanyakazi wa mgodi huo kutaka stahiki zao baada ya
kuumia kazini na kuachishwa kazi pamoja na kutaka huduma bora za kijamii
ikiwemo barabara za lami na vituo vya afya/hospitali kutokana na uwepo
wa mgodi.
0 comments:
Post a Comment