Mratibu wa Umoja wa Mataifa nchini na Mwakilishi wa UNDP, Alvaro Rodriguez
SHIRIKA la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) limechangia Sh milioni 110 kuwezesha huduma za maji kwa wakazi zaidi ya 10,000 wa Jimbo la Kikwajuni.
Mradi huo ulizinduliwa na Rais wa Zanzibar, Dk Mohamed Shein miaka miwili iliyopita. Akizungumza na wananchi wa jimbo hilo baada ya kutembelea vituo na vyanzo vya mradi huo vya Migombani na Kilimani, Mratibu wa Umoja wa Mataifa nchini na Mwakilishi wa UNDP, Alvaro Rodriguez alisema lengo lao ni kuona jamii inapata huduma mbalimbali ili kuleta maendeleo.
Alisema UNDP imechangia Sh milioni 110 ili mradi huo uweze kukamilika. Akizungumza kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira, Salama Abood Talib, alisema lengo la serikali ni kuhakikisha inashirikisha wadau mbalimbali katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa wananchi wa maeneo mbalimbali visiwani humo.
Alimshukuru mwakilishi huyo wa UNDP kwa msaada waliotoa kumalizia mradi huo. Mradi wa Maji Kikwajuni unakadiriwa kugharimu Sh milioni 344, ambapo awamu ya kwanza na ya pili ikiwezeshwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), mbunge wa jimbo hilo, michango ya wananchi na Serikali ya Japan.
0 comments:
Post a Comment