Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
amewahakikishia wananchi wa Pwani kuwa Serikali ya Awamu ya Tano
imejipanga kuhakikisha miradi mikubwa ya maendeleo yenye manufaa kwa
mkoa huo na Taifa kwa ujumla inatekelezwa kama alivyoahidi.
Mhe.
Rais Magufuli amesema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika
uwanja wa Bwawani Mjini Kibaha akiwa katika siku ya kwanza ya ziara
yake ya kikazi ya siku 3 Mkoani Pwani.
Mhe.
Dkt. Magufuli ameitaja miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa reli ya kati kwa
kiwango cha kisasa (Standard Gauge) ambayo imeanza kujengwa, ujenzi wa
barabara ya njia sita kati ya Dar es Salaam na Chalinze yenye urefu wa
Kilometa 128, ujenzi wa bandari kavu ya Ruvu itakayopokea mizigo ya
kutoka bandari ya Dar es Salaam na ujenzi wa mradi wa umeme katika
maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge) ambao mipango ya utekelezaji
kwa kushirikiana na Ethiopia imeanza.
Amebainisha
kuwa pamoja na kutekeleza miradi hiyo Serikali ya Awamu ya Tano
itaendelea kuchukua hatua dhidi ya watu wanaolihujumu Taifa ikiwemo
kujihusisha na vitendo vya wizi na rushwa na haitakatishwa tamaa na watu
wanaolalamika na kubeza juhudi hizo.
“Stiegler’s
Gorge mradi ambao ulifanyiwa utafiti tangu enzi ya Mwl. Julius Nyerere,
tukautelekeza, nataka tujenge bwawa litakalozalisha umeme
utakaotosheleza katika nchi yetu, nchi ya viwanda, ili Watanzania
wasilalamikie tena suala la umeme, nataka tuachane na umeme wa matapeli
wanaokuja hapa wanawekeza kwa lengo la kutuibia.
“Mimi
nachukia wezi, na kwa kweli wezi watakoma tu, awe mwizi wa Tanzania,
awe mwizi wa Ulaya, awe anatoka magharibi, mashariki, kaskazini au
kusini, mwizi ni mwizi tu” Alisisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Aidha,
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza viongozi na wananchi wa mkoa wa Pwani
kwa Mkoa huo kutekeleza vizuri sera ya ujenzi wa viwanda na ametaka
viongozi wa Mikoa mingine waige mfano huo ili kuwawezesha wananchi
kupata ajira na kujiongezea kipato.
Kuhusu
mauaji yanayotokea katika Wilaya za Kibiti na Rufiji Mkoani humo, Mhe.
Rais Magufuli amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola
ili kuwabaini wanaofanya vitendo hivyo lakini amesema Serikali imeanza
kuwashughulikia wanaowahalifu hao na itahakikisha inakomesha tatizo
hilo.
Mapema
akitoa taarifa ya maendeleo ya Mkoa wa Pwani, Mkuu wa Mkoa humo
Mhandisi Evarist Ndikilo amesema mkoa huo una jumla ya viwanda 371
vikiwemo viwanda 9 vikubwa na kwamba ujenzi wa viwanda hivyo unaendelea
katika hatua mbalimbali.
Leo
tarehe 21 Juni, 2017 Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake Mkoani
Pwani ambapo atazindua viwanda vitatu ambavyo ni kiwanda cha
vifungashio cha Global Packaging Co. Ltd, kiwanda cha matrekta cha
Ursus-TAMCO Co. Ltd na kiwanda cha chuma cha Kiluwa Steel Group.
Pia atazindua mradi wa maji wa Ruvu na kuzungumza na wananchi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
0 comments:
Post a Comment