Mtaalamu wa masomo ya Sayansi, Fadhil
Leonard akiwaelekeza wanafunzi wa Shule ya Msingi namna ya kutengeneza
gari linalojiendesha bila ya kuwa na dereva wakati wa hafla ya uzinduzi
wa Wiki ya Sayansi Afrika Tanzania iliyofanyika katika viwanja vya
Shule ya Al–Murtaza Upanga jijini Dar es Salaam leo.
Mtaalamu wa masomo ya Sayansi kutoka
Shule ya Ilboru Arusha, Vedasto Biyaka akiwaelekeza wanafunzi wa Shule
ya Msingi namna ya kutengeneza magari hayo.
Wanafunzi wakipata maelekezo ya
kutengeneza magari hayo kutoka kwa mtaalamu wa masomo ya sayansi, Gibson
Kawago kutoka Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT)
Mtaalamu wa masomo ya Sayansi kutoka
Shule ya Ilboru Arusha, Vedasto Biyaka akiwaelekeza wanafunzi wa Shule
ya Msingi namna ya kutengeneza magari hayo.
Wanafunzi wakiendelea kujifunza kutengeneza magari hayo.
Balozi wa NEF, Aneth David ambaye ni
mwanataaluma wa sayansi na mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), akizungumza na wanahabari kuhusu kongamano hilo.
Na Dotto Mwaibale
KONGAMANO la Next Einsten (NEF) ambalo
ni mpango wa Taasisi ya kuendeleza Hisabati na Sayansi Afrika (AIMS) kwa
kushirikiana na Taasisi ya Robert Bosch Stiftung leo imetangaza
uzinduzi wa wiki ya sayansi Afrika kupitia kongamano la NEF jijini Dar
es Salaam.
Akizungumza katika uzinduzi wa kongamano
hilo jijini Dar es Salaam jana, Balozi wa NEF, Aneth David ambaye ni
mwanataaluma wa sayansi na mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), alisema kongamano hilo wanataaluma wa ndani, mabingwa wa sayansi
na teknolojia wataongoza kwenye tukio hilo.
“Kongamano la Next Einsten la wiki ya sayansi Afrika ni wiki la kwanza la sayansi kuratibiwa ndani ya Afrika” alisema David.
Alisema lengo la msingi la kongamano
hilo ni kuendeleza wanasayansi na wanateknolojia wa kesho kwa
kuwahusisha watoto na vijana katika shughuli za kisayansi kama vile
kujumuika pamoja na kushiriki maonesho.
“Shughuli zetu pia zitaonesha matokeo
chanya ya sayansi kwa jamii nzima kwa kuwakutanisha wadau muhimu kutoka
sekta zote na kuchochea uwekezaji katika tafiti na maendeleo pamoja na
kujadiliana njia nzuri za kuwavutia na kuendeleza vijana hususan
wasichana na wanawake katika nyanja ya sayansi” alisema Rais wa AIMS
ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu na Mwenyekiti wa NEF, Thierry Zomahoun.
Alisema wiki ya Sayansi Afrika
inayofanyika hapa nchini itashuhudia vipindi vya kusisimua kama vile
kuhusisha wanafunzi katika kujifunza kwa vitendo somo la kemia,
Teknolojia na Uhandi kwa kutumia vifaa shirikishi vya sayansi ambapo pia
wanafunzi watashiriki katika shughuli za vitendo na mashindano ya
miradi ya sayansi na baadaye kufuatia na sherehe ya kutoa tuzo kwa
washindi.
Kongamano hilo linafanyika Viwanja vya Shule ya Sekondari ya Seminari ya Al-Murtaza Upanga jijini Dar es Salaam.
(Imeandaliwa na mtandao wa www.habari za jamii.com-simu namba 0712727062)
0 comments:
Post a Comment