METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, June 18, 2017

Mangula alia na ‘wapanga safu’ CCM

 MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Philip Mangula

Na Katuma Masamba

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Philip Mangula amesema chama hicho hakitasita kuwavua uanachama Makatibu wa chama hicho katika ngazi za Shina hadi Taifa wanaoendelea kusaliti kwa kupanga safu za wagombea.

Amesema watakaobainika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni za chama hicho. Mangula alitoa kauli hiyo jana wakati akipokea tamko la kumuunga mkono Rais John Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama hicho katika utendaji kazi wake ikiwemo kuzuia mchanga wa dhahabu kwenda nje ya nchi.

“Ndani ya CCM bado kuna baadhi ya makatibu ngazi ya mashina hadi Taifa, wanaendelea kupanga safu katika chaguzi ndogo zinazoendelea ndani ya chama, tutawashughulikia kwa mujibu wa kanuni za chama,” alisema Mangula.

Aidha, Mangula amewapongeza viongozi wa chama hicho mkoa wa Dar es Salaam, kwa kuandaa tamko hilo na kupokelewa vizuri na wanachama waliojitokeza katika mkutano huo.

Akizungumza katika mkutano huo, Katibu wa CCM, mkoa wa Dar es Salaam, Saad Kusilawe alisema, hatua zinazochukuliwa na Rais Magufuli za kupambana na watu wanaoshiriki katika kuhujumu na kuiba rasilimali zinapaswa kupongezwa na kuungwa mkono na kila mmoja.

Kusilawe ambaye pia ni Mkurugenzi wa uchaguzi ndani ya chama ngazi ya mkoa, alisema ameshatoa maelekezo kwa kamati ya wilaya na kamati za siasa kwamba mtu atayebainika kuwa msaliti afukuzwe ndani ya chama.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Dar es Salaam, Angela Kizigha, alisema suala la kufukuza viongozi ndani ya chama halikuanza sasa bali limeanza tangu ulipofanyika mkutano mkuu wa chama hicho Taifa, Dodoma, ambapo baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu waliobainika kusaliti chama hicho walivuliwa uanachama.
Share:

Related Posts:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2025 WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com