MWEZI mmoja baada ya kupelekwa Marekani kwa matibabu zaidi, majeruhi
watatu wa ajali ya basi la Shule ya Mchepuo ya Kiingereza ya Lucky
Vincent ya jijini Arusha, wameripotiwa kuwa afya zao zimezidi kuimarika
kiasi cha sasa kuanza kujihudumia wenyewe ikiwamo kuoga.
Majeruhi hao, Doreen Mshana, Sadia Awadh na Wilson Tarimo, walipata
ajali Mei 6, mwaka huu wilayani Karatu huku wanafunzi wenzao 32, walimu
wawili na dereva wakipoteza maisha.
Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM) na Mwenyekiti mwenza wa Shirika la
STEMM, Lazaro Nyalandu, Alhamisi wiki hii alitoa taarifa hizo njema
kupitia mtandao wake wa Facebook, akisema madaktari wamejiridhisha
kuhusu maendeleo ya kupona kwa mifupa ya watoto hao.
Alisema Sadia na Wilson walipelekwa Kituo cha CNOS (Center for
Neurosurgery Orthopedics and Spine) Jimbo la Dakota Kusini, ambako
madaktari walijiridhisha na maendeleo ya kupona kwa mifupa, hivyo
wakawatoa bandeji ngumu.
“Sadia na Wilson wameondolewa ‘Cast’ walizokuwa wamewekewa na sasa
wanaweza kujiogesha wenyewe kwa mara ya kwanza tangu wafikishwe
hospitalini,” alisema Nyalandu.
Kauli kama hiyo imetolewa pia na Muuguzi wa Hospitali ya Mount Meru,
Symphrosa Silali aliyeongozana na majeruhi hao, akisema; “Jumatano (ya
wiki hii) watoto wote walitolewa ‘mihogo’ na wanaendelea vizuri, hatua
ambayo imewawezesha kutumia viwiko vya mikono vizuri, ikiwamo kuendelea
na kufundishwa namna ya kukunja mikono na kuinyoosha.
“Watoto wote wanafanya mazoezi mara tatu kwa wiki, wapo wataalamu pia
wanaowafanyia mazoezi ya namna gani wanaweza kukabiliana na vitu
vilivyokuwa mbele yao ili waweze kuvisahau.
Lakini pia kuna mazoezi ya viungo yanayowezesha viungo vyao kuendelea
kuzoea kutumia mikono, miguu yao. Lakini pia wanafundishwa kufanya vitu
vidogo vidogo wenyewe kama kupiga mswaki, kuoga na kuvaa nguo.”
Hiyo ndiyo iliyokuwa ndoto ya Watanzania wengi na hata timu ya
madaktari wa ndani na nje ya nchi na Mwinjilisti maarufu wa Marekani,
Franklin Graham aliyebeba gharama za kuwasafirisha na kuwahudumia watoto
hao na wauguzi wao katika kipindi chote watakachokuwa Marekani.
Na mara baada ya kufikishwa Marekani kwa ndege maalumu iliyokodiwa na
Graham kutoka Shirika la Misaada ya Kibinadamu analoliongoza, Samaritan
Purse; mwinjilisti huyo alisema; “Ninaamini Mungu ana mipango na watoto
hawa, tunawaombea waweze kupona na kurejea katika hali yao ya kawaida.”
Ndiyo, pamoja na sala na maombi ya wengi, lakini pia uwezo wa Mungu,
mkono wa Graham pia umechangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha matibabu ya
watoto hao wa darasa la saba waliokuwa wanasafiri na wenzao kwenda
Karatu kwa mtihani wa majaribio, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya
mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi baadaye mwaka huu.
Amehusika moja kwa moja na gharama za kukodi ndege ya kuwachukua
watoto hao kwa gharama ya takribani dola za Marekani 350,000 (Sh milioni
735), lakini pia alilipia gharama nyingine zote, kuanzia za matibabu,
chakula na malazi kwa wakati wote ambao wagonjwa hao na wasindikizaji
wao watakuwa nchini Marekani. Aliguswaje na ajali ya Arusha?
“Niliposikia juu ya ajali ya basi la wanafunzi Tanzania, nilijua na
kuona umuhimu wa Samaritan’s Purse kufanya jambo…ndivyo ilivyokuwa.
“Ninaamini Mungu ana mipango na hawa watoto, na tunawaombea ili afya zao
zizidi kuimarika,” Graham amekaririwa akisema kupitoa vyombo vya habari
vya Souax.
Anasema mara baada ya kupata taarifa za ajali hiyo ya Arusha na
msaada unaohitajika, alihangaikia vibali vya kuiruhusu ndege kusafiri
kwa saa 24 kutoka Marekani hadi Tanzania na kwa `Nguvu za Mungu’ kila
jambo lilifanyika pasipo na vikwazo.
“Tunafanya haya yote kwa Jina la Yesu Kristo…lakini hatubagui dini,
kwani wote ni wamoja, watoto wa Mungu,” anasema. Ilivyokuwa Timu ya
madaktari ikiongozwa na Dk Steve Meyer wa STEMME, iliwasiliana na Dk
Steven Joyce, Mkurugenzi mwenza wa Hospitali ya Mercy inayowatibu watoto
hao na kuhakikishiwa kuwa, wako tayari kufadhili tiba ya watoto hao
kama watafikishwa Marekani.
Ndipo yakaanza mawasiliano kwa njia ya simu baina ya mashirika,
serikali ya Tanzania na wadau wengine yaliyozaa matunda baada ya saa 60
na kupata uhakika wa safari hiyo. Baada ya kuzungumza na uongozi wa
hospitali ya Mercy, alimgeukia Mbunge Steve King, mtu wa karibu wa
Graham aliyemuunganisha na mwinjilisti huyo aliyepiga simu kwa Dk Meyer
kumweleza atabeba gharama za safari na mambo mengine.
Franklin Graham ni nani hasa? Franklin ambaye Julai 14 mwaka huu
anatarajiwa kutimiza umri wa miaka 65, ni mtoto mkubwa wa Mwinjilisti
bilionea, Bill Graham, mwasisi wa taasisi ya Billy Graham Evangelistic
Association (BGEA) ambayo tangu mwaka 2001 inaongozwa na Franklin. Akiwa
na umri wa miaka 22 mwaka 1974, aliokoka akiwa hotelini huko
Yerusalemu.
Mwaka huohuo, alimuoa Jane Cunningham na mpaka sasa amebahatika kuzaa
naye watoto wanne, William Franklin Graham IV (Will) aliyezaliwa mwaka
1975, Roy Austin Graham (1977), Edward Bell Graham (1979) na Jane Austin
Graham Lynch (Cissie) (1986).
Graham na mkewe wamebahatika kupata wajukuu 11. Alikomazwa katika
imani ya dini na wasaidizi muhimu wa baba yake, Bill Graham; Roy
Gustafson na John Wesley White. Na baada ya kuiva, aligeuka mhubiri,
akipata sifa kila uchao.
Tangu mwaka 1989, Graham amehubiria neno la Mungu watu milioni 126
katika mikutano mbalimbali ya kidini duniani. Mara baada ya kuokoka
mwaka 1974, Graham aliungana na Bob Pierce,mwanzilishi wa shirika la
Samaritan's Purse na kufanya naye kazi kwa wiki sita huko barani Asia.
Akiwa huko, Graham alipata nguvu zaidi ya kuigeukia dunia ili kutoa
misaada zaidi ya kibinadamu, dhamira aliyoiendeleza hata baada ya kifo
cha Pierce naye kukabidhiwa rasmi nafasi ya kuwa Mtendaji Mkuu wa
Shirika kuanzia mwaka 1979. Tangu wakati huo, shirika lake limefanya
kazi katika nchi zaidi ya 100 duniani.
Shirika hilo hutoa misaada kwa waathirika wa migogoro, maafa, njaa na
milipuko ya magonjwa sehemu mbalimbali dunia lakini pia husaidia
chakula, maji, sehemu za makazi ya muda, matibabu na huduma nyingine za
misaada ya kibinadamu.
Mbali ya kuhubiri na kusimamia misaada ya kibinadamu, Franklin pia ni
mtunzi wa vitabu vya `kiroho’, baadhi vikiwa A Wing and a Prayer
(2005), All for Jesus (2003), Kids Praying for Kids (2003), The Name
(2002), Living Beyond the Limits: A Life in Sync with God (1998), Rebel
With A Cause: Finally Comfortable Being Graham (1995), Miracle in a Shoe
Box (1995) na Bob Pierce: This One Thing I Do cha mwaka 1983.
Huyo ndiye Bill Graham, mwinjilisti aliyeongeza nguvu katika
kufanikisha matibabu ya majeruhi watatu wa ajali ya basi la shule la
Lucky Vincent ya jijini Arusha. Mbali ya misaada ya hali na mali kutoka
kwa Watanzania, hospitali ya Mercy na pia gharama nyingine zilizobebwa
na Graham kutokana na ajali hiyo, Bodi ya wadhamini ya Shirika la STEMM
(Siouxland Tanzania Educational Medical Ministries) limeamua kuwaenzi
watoto 32 waliopoteza maisha katika ajali ya Karatu kwa kuwasomesha
majeruhi hao hadi elimu ya chuo kikuu.
CREDIT: HABARI LEO
Sunday, June 18, 2017
KARIBU TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA
KARIBU TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA
Popular Posts
-
Kiongozi wa chama cha upinzani cha Forum for Democratic Change (FDC) nchini Uganda Kizza Besigye amekamatwa tena na maafisa wa polisi. ...
-
📌 Asema Rais, Dkt. Samia anafanya kazi kubwa ya kuwaunganisha Watanzaia 📌 Atak...
-
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea hundi ya sh. 4, 000,000,000/= kutoka kwa Meneja Mkazi (Country Manager) wa Kampuni ya Madini ya...
-
Mvua kubwa za El-Nino zilizonyesha zimeleta athari maeneo mbalimbali...
-
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akifungua kikao kazi cha vyama vya ushirika kuhusu ununuzi wa mbolea k...
Powered by Blogger.
0 comments:
Post a Comment