Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha
CHAMA Kikuu cha Ushirika cha Mbinga (Mbicu 1993), kilifilisiwa kutokana na kudaiwa na Benki ya NBC na wadau wengine zaidi Sh bilioni 2.1, imefahamika.
Kutokana na kudaiwa huko, Mbicu 1993, kilifutwa kwenye daftari la serikali na kilijikuta ni muflisi kutokana na mali zake kuwa na thamani ya Sh milioni 752.8. Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William ole Nasha alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbinga Vijijini, Martin Msuha (CCM).
Msuha alitaka kujua kwanini muflisi bado anashikilia mali za chama hicho badala ya kukabidhi kwa chama cha Mbinga Farmers’ Cooperative Union (Mbifacu) Ltd kwa muda mrefu. Nasha alisema kwa sasa muflisi hajashikilia mali za Mbicu Ltd, kwani baada kufutwa wanachama walianzisha Mbifacu Ltd kwa kutegemea kukabidhiwa mali za chama hicho.
“Mwaka 2007, wanachama walioanzisha Mbifacu Ltd, walirudishiwa mali zao na kuahidi kulipa madeni yaliyodaiwa kwa Mbicu Ltd likwemo la Golden Impex (T) Ltd la Sh milioni 155 ambalo lililipwa Machi 13, 2012,” alisema.
Baada ya deni hilo kulipwa Mbifacu Ltd ilikabidhiwa asilimia 70 ya mali na mufilisi na Bodi ya Uongozi ya Mbifacu Ltd ilianza kusimamia mali hizo. “Sehemu ya mali asilimia 30 iliyobaki, ilikabidhiwa baada ya Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika kujiridhisha juu ya utekelezaji wa Mkataba wa Maridhiano (MoU) baina ya muflisi na Mbifacu Ltd,” alisema.
Kuanzia 2008, serikali imekuwa ikilipa madeni ya vyama vya ushirika yaliyohakikiwa na Mkaguzi na Mdhibiti wa Serikali (CAG) ambapo hadi Desemba 2012, imelipa Sh bilioni 6.92 kati ya deni la bilioni 11.84.
Aidha serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika, inaendelea kuvisimamia na kuvishauri vyama vya ushirika kutumia sehemu ya ziada kulipa madeni ambapo hadi Mbifacu Ltd imelipa Sh milioni 36 ikiwa ni sehemu ya deni la watumishi waliokuwa wanaidai Mbicu 1993 Ltd na inaendelea kulipa mengine likiwemo la NBC Holdings
0 comments:
Post a Comment