METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, June 19, 2017

Rugemerila, Singh kortini kwa uhujumu uchumi


 Harbinder Singh (kulia) na James Rugemarila (kulia kwake) wakiwa katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam walipofikishwa kujibu mashitaka ya uhujumu uchumi. (Picha na Mpigapicha Wetu).

Na Francisca Emmanuel

Wafanyabiashara wawili, James Rugemarila na Harbinder Singh Sethi walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana, wakikabiliwa na mashitaka sita ya uhujumu uchumi, likiwemo la kuisababishia serikali hasara ya dola za Marekani milioni zaidi ya 22 sawa na Sh bilioni 309.

Rugemarila ni Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing wakati Sethi ni Mmiliki wa Kampuni ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL). Hata hivyo, washitakiwa wote wawili walisomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Huruma Shaidi saa 8.35 mchana, hawakutakiwa kujibu mashitaka hayo na kupelekwa mahabusu katika Gereza la Segerea, kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi ya aina hiyo na kutoa maamuzi ya dhamana.

Akisoma mashitaka hayo, Wakili wa Serikali, Paul Kadushi, alisema ni matakwa ya sheria kwa kesi za uhujumu uchumi kusikilizwa na Mahakama Kuu au Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) atoe hati maalum ya kuipa mamlaka mahakama hiyo kusikiliza kesi ya aina hiyo, ambapo kwa kesi hiyo bado kibali cha aina hiyo hakijatolewa. Kadushi alidai washitakiwa wote wanadaiwa kuwa kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India kwa lengo la kutenda kosa.

Alidai katika shitaka la pili kuwa washitakiwa walijihusisha na mtandao wa wahalifu ambapo inadaiwa kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19,2014 jijini Dar es Salaam wakiwa siyo watumishi wa umma, walishirikiana na watumishi wa umma kutekeleza mtandao huo wa uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.

Katika shitaka la tatu linayomkabili Sethi, inadaiwa kuwa Oktoba 10, 2011 katika mtaa wa Ohio, Ilala Dar es Salaam akiwa na nia ya ulaghai alighushi fomu namba 14 A ya usajili wa Kampuni na kuonesha kuwa yeye ni Mtanzania anayeishi Kitalu namba 887 Mtaa wa Mrikau Masaki wakati akijua sio kweli.

Pia, Sethi anadaiwa alitoa nyaraka ya kughushi ambayo ni fomu namba 14 A ya usajili wa kampuni kwa Ofisa Msajili wa Kampuni, Seka Kasera kwa njia ya kuonesha kwamba yeye ni Mtanzania na mkazi wa Mtaa wa Mrikau, Masaki, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Aidha, Kadushi alidai katika mashitaka ya kujipatia fedha kwamba kati ya Novemba 28 na 29, 2011 na Januari 23,2014 katika Makao Makuu ya Benki ya Stanbic Kinondoni na Benki ya Mkombozi Tawi la Mtakatifu Joseph, kwa ulaghai washitakiwa hao walijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Dola za Marekani milioni 22.2 sawa na Sh za Tanzania bilioni 309.5.

Pia washitakiwa wote wanadaiwa kuisababishia serikali hasara, ambapo inadaiwa walitenda makosa hayo Novemba 29, 2013 katika Benki ya Stanbic Tawi la Kati Kinondoni, kwa vitendo vyao waliisababishia serikali hasara ya Dola za Marekani milioni 22. 2 sawa na Sh bilioni 309.5 Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi alidai upelelezi wa mashitaka hayo haujakamilika na kwamba wanaomba tarehe kwa ajili ya kutajwa tena kesi hiyo. Wakili wa utetezi, Respicius Didas akiwawakilisha mawakili wenzake watano, aliomba mahakama iwapatie wateja wao dhamana kwa sababu mashitaka yanayowakabili yanadhaminika.

Pia alidai kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, washitakiwa wana haki ya kupata dhamana. Hata hivyo, upande wa mashitaka uliiomba mahakama hiyo kuyatupilia mbali maombi ya utetezi ya kuwapatia dhamana washtakiwa hao. Wakili Kadushi alieleza mahakama hiyo kuwa haina mamlaka si tu ya kutoa dhamana bali hata kusikiliza maombi ya dhamana hiyo.

Alidai mahakama yenye mamlaka ya kusikiliza mashitaka ya uhujumu uchumi ya zaidi ya Sh milioni 10 ni Mahakama Kuu na ndiyo maana washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote wakati wakisomewa mashitaka yao. Kadushi alidai mazingira pekee ambayo yangeifanya mahakama iweze kusikiliza maombi hayo ni baada ya DPP kutoa cheti maalumu cha kuipa mamlaka mahakama ya Kisutu kuisikiliza kesi hiyo.

“Maombi ya dhamana yameletwa katika mahakama isiyo na mamlaka ya kisheria na mamlaka ya kutoa dhamana kwa kesi za uhujumu uchumi inayozidi Shilingi milioni 10 kwa mujibu wa sheria ni Mahakama Kuu,” alieleza Wakili Kadushi. Kwa upande wa Wakili wa Serikali Mkuu, Nchimbi aliomba mahakama kutupilia mbali hoja zote za maombi ya dhamana za upande wa utetezi na ijielekeze kwa jinsi inavyoona inafaa na washitakiwa waende mahabusu wakati wakisubiri taratibu za zinazoendelea za kesi hiyo.

Kutokana na hali hiyo, Hakimu Shaidi alisema ni mahitaji ya sheria kwamba kesi za uhujumu uchumi zinazozidi kiasi cha sh milioni 10 Mahakama yake haina mamlaka ya kuisikiliza wala kutoa dhamana, isipokuwa kwa cheti maalum cha DPP cha kuiipa mamlaka. Alisema upande wa utetezi, unatakiwa kwenda Mahakama Kuu kupata dhamana, bali yeye anatoa tarehe ya kutajwa. Washtakiwa hao wamepelekwa rumande hadi Julai 3, mwaka huu.
Share:

Related Posts:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2025 WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com