Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji), Dorothy Mwaluko akimsikiliza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Uchapaji wa Serikali Zanzibar, Khalfan Sheikh Saleh, wakati akimueleza namna Wakala unavyotekeleza majukuu yake wakati alipotembelea Wakala huo, Maruhubi, Zanzibar.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji), Dorothy Mwaluko akisisitiza umuhimu wa mashine za kidigitali wakati alipotembelea Wakala wa Uchapaji wa Serikali Zanzibar, , wakati alipotembelea Wakala huo, Maruhubi, Zanzibar.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji), Dorothy Mwaluko ameeleza kuwa Katika kuhakikisha kuwa Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali inakidhi mahitaji ya wateja wake kwa kuzingatia ubora wa huduma, ameitaka idara hiyo kuwekeza kwenye matumizi ya mashine za kidigitali ambazo zina uwezo wa uchapaji kwa kasi kubwa, viwango bora na kwa idadi kubwa ndani ya muda mfupi.
Akiongea mara baada kutembelea Wakala wa Uchapaji wa Serikali Zanzibar kwa lengo la kujionea namna Wakala inavyotekeleza majukumu yake, Katibu Mkuu Mwaluko amefafanua kuwa amevutiwa na utekelezaji wa majukumu ya Wakala kwa kuwa inaendesha shughuli za uchapaji kibiashara, inao usimamizi mzuri wa ubora unaozingatia teknolojia ya kisasa ya uchapaji, hivyo Idara ya Mpiga chapa Mkuu wa serikali ya Tanzania bara, hainabudi kutekeleza majukumu yake kama ilivyo kwa Wakala.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Uchapaji wa Serikali Zanzibar, Khalfani Sheikh Saleh, amefafanua kuwa Wakala umewekeza kwenye mashine za kidigitali na wamewajengea uwezo wafanyakazi wake, ambapo kutokana na uwezo huo wamefanikiwa kukidhi mahitaji ya wateja wake kwa wakati na kwa ubora husika.
Aidha, Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa Wakala wamefanikiwa kutekeleza Mpango wao wa biashara kwa kupata soko la uhakika la uchapaji hususani kwa Taasisi na idara za serikali pamoja na sekta binafsi, hivyo wamefanikiwa kuongeza mapato ya Serikali kupitia fedha zinazopatikana kupitia kazi za uchapaji na ununuzi wa vifaa vya ofisi na kuandikia.
Tangu mwaka 2018, Zanzibar imeanzisha rasmi Wakala wa Uchapaji wa Serikali Zanzibar, chini ya Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale ambapo Wakala hiyo imepewa uwezo kisheria wa kutoa huduma za uchapaji. Kwa upande wa Tanzania Bara, Idara ya Mpiga chapa Mkuu wa serikali ipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwa na jukumu la kutoa huduma ya uchapaji.
Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa serikali imeabainisha lengo lake kuu kuwa, ni Kutoa huduma za Uchapaji kwa wakati zenye ubora na kwa gharama nafuu. Idara hiyo inaongozwa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali ambaye husimamia vitengo vya Udhibiti wa Ubora, Uzalishaji, Ufundi, Masoko na Maduka ya Vitabu ya Serikali.
0 comments:
Post a Comment