Na Mwandishi Wetu, Singida
MKUU wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida Mhe Miraji J. Mtaturu amewaomba wananchi kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli katika juhudi anazoendelea nazo za kupigania rasilimali za Taifa.
Aidha ametoa onyo kwa Wabunge, Madiwani na Wenyeviti wa Vijiji katika Wilaya hiyo wanaotumia majukwaa ya siasa kubeza na kutaka kukwamisha juhudi hizo za Rais na kusema kamwe hatawavumilia watu hao.
Mtaturu ametoa Rai hiyo Wilayani humo alipowatembelea wachimbaji wadogo na kuzungumza nao ikiwa ni njia mojawapo ya kuunga mkono juhudi hizo za Rais Magufuli katika sekta ya madini ambapo amesema Rais anafanya kazi kubwa na nzuri kwa maslahi ya watanzania hivyo ni jambo jema kuunga mkono nia njema aliyonayo.
“Mheshimiwa Rais anawapenda sana na anawaunga mkono katika shughuli zenu na serikali yake inaahidi kuendelea kuwapa ruzuku za mitaji ya kuwasaidia kuboresha uchimbaji wenu ili uwe na tija hivyo jambo jema kwetu ni kumuunga mkono,” Alisema Mhe Mtaturu.
Katika mazungumzo hayo amewasihi wachimbaji kuwa na ushirikiano na jamii inayowazunguka, kuchangia huduma za kijamii na kujenga utaratibu wa kuhifadhi mazingira kwa mujibu wa sheria huku akimpongeza mchimbaji Yusuph Mwandami aliyewekeza mashine ya kuchomea carbon yenye dhahabu hatua ambayo amesema itapunguza gharama za kusafiri kwenda Mwanza.
Mtaturu aliishauri wizara ya nishati na madini kuangalia upya leseni waliyotoa kwa kampuni ya Shanta Gold Mine ambayo toka mwaka 2006 walipewa leseni hiyo lakini mpaka sasa hawajaanza uchimbaji tofauti na wachimbaji wadogo ambao wana miezi mitatu tangu wapewe leseni lakini tayari wameshaanza uzalishaji na hivyo kushauri kufuta leseni kwa kampuni za aina hiyo ili kutoa nafasi kwa wawekezaji wengine wenye nia njema.
“Nawaalika wawekezaji wenye nia ya kufanya uchimbaji mje Ikungi kwa sababu dhahabu ya hapa ni bora kitaalamu kwani Purit yake ni asilimia 91- 96 lakini pia nawakumbusha wachimbaji mlioanza kuzalisha mlipe mrahaba na tozo ya huduma ya Halmashauri na katika hili Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hakikisha hadi kufikia Julai mosi mwaka huu wote wanaodaiwa wawe wamelipa” Alisisitiza Mhe Mtaturu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji cha Sambaru Bdg Hassan Maganga alimpongeza Rais Magufuli kwa hatua anazochukua kwa kuwa zitasaidia kuiwezesha nchi kupata mapato yatakayopelekea kuimarisha huduma kwa wananchi.
Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji wadogo Meneja wa mgodi wa Elizabeth Shango, Ndugu Emmanuel Mwanga aliishukuru serikali kwa kuwapa ruzuku iliyowasaidia kununua vifaa mbalimbali na kutoa ombi la kuendelea kupata ruzuku ili wanunulie Winchi ya kutolea mizigo kwenye mashimo huku akiweka bayana changamoto ya ukosefu wa nishati ya umeme waliyonayo inayopelekea kuongezeka kwa gharama za uendeshaji.
Akijibu changamoto hiyo Mhe Mtaturu
aliwahakikishia kuwa kupitia mpango kabambe wa upelekaji umeme vijijini (REA III) itafikisha umeme vijiji vitatu vya kata ya Mang'onyi ambavyo ni Mang'onyi, Mwau na Mulumbi.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment