METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, June 21, 2017

BAJETI MPYA 2017/18 NA FURSA ZILIZOPO KWA VIJANA

Bajeti Mpya ya Serikali ya mwaka 2017/2018 ndiyo Bajeti ya pili tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani chini ya Uongozi mahiri wa Mhe. Rais Dr. John Joseph Pombe Magufuli, bajeti hii iliyopitishwa kwa asilimia 73 ya wabunge wote wa Bunge la Jamuhuri 20/07/2017 imeonyesha nia ya dhati kabisa katika kuyafikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 ambayo ni kuufikia Uchumi wa Kati wenye sifa kubwa ya Viwanda.

Kilichogusiwa katika bajeti hii ni kuongeza kasi ya kukua kwa Uchumi kwa ujumla, kusimamia Rasilimali za Taifa na kuthibiti Mapato yatokanayo na rasilimali hizo, kuimarisha nidhamu ya watumishi wa Umma na kuhakikisha tunakuwa na Miundombinu safi na salama ili kujihakikishia wawekezaji wengi zaidi kutoka ndani na nje ya nchi.

Bajeti hii pia imehakikisha kuwa tunanufaika vilivyo na Rasimali zetu za Madini na Gesi, tunakuza zaidi Sekta ya watu binafsi, tunakuza hali ya kilimo chetu kuwa chenye tija na ufanisi zaidi kuliko hapo awali, kufanya juhudi zaidi za kuongeza idadi ya watalii hapa nchini kwa kuvitangaza zaidi vivutio vyetu, kuongeza ufanisi katika Sekta nzima ya Elimu, Serikali imejidhatiti kutoa Elimu bora na yenye tija kwa maendeleo ya nchi yetu, pia Serikali imeamua kuondoa Urasimu usiokuwa na maana sehemu zote za kazi na kupambana na Rushwa kwa vitendo kama ambavyo juhudi zimeshaanza kufanyika.

Sehemu zilizotiliwa mkazo katika Bajeti hii ni pamoja na kuongeza kasi ya Ukuaji wa Uchumi, kuongeza kasi ya ukuaji wa Sekta ya viwanda kama ambavyo Rais ameweza kusisitiza. Kukuza Ueledi katika kazi miongoni mwa wanataaluma na kutengeneza mazingira rafiki sana kwa biashara mbalimbali na viwanda pia.

FURSA MBALIMBALI ZA VIJANA ZILIZOPO KATIKA BAJETI MPYA 2017/2018
KUONDOLEWA KWA KODI YA ONGEZEKO LA THAMANI KATIKA SHUGHULI ZA USAFIRISHAJI NA FORODHA
Mwaka jana kodi hii ililalamikiwa sana mpaka baadhi ya watu walidai imepunguza idadi ya watumiaji wa Bandari yetu, ni jambo la kushukuru kuona kwamba Serikali ilisikia kilio chetu na kulifanyia kazi na sasa hakuna VAT za watoa huduma Bandarini. Tulishuhudia wateja wetu wakubwa wa bandari yetu kama DRC, ZAMBIA, MALAWI, UGANDA, BURUNDI na RWANDA wakitumia bandari zingine kama Mombasa, Beira hadi Pretoria, sasa kikwazo hakipo tena. Hivyo tunawasihi vijana wachangamkie fursa hii adhimu kwa vile barabara zetu bado ni bora sana, na kijiografia sisi ni karibu sana na wao, tujitahidi kufanya kazi kwa bidii tuwarudishe wote na kuongeza zaidi.

KUFUTWA KWA KODI YA ONGEZEKO LA THAMANI (VAT) KWENYE BIDHAA ZA MITAJI (CAPITAL GOODS)
Hili ni jambo la heri ambalo linafaa vijana wote kulijua vizuri. Kodi hii ndiyo ilikuwa inafanya gharama za ununuzi wa mashine za kutengenezea bidhaa mbalimbali kuwa ghali sana, kwa sasa ukiagiza mashine za kuzalishia bidhaa zingine hutotozwa VAT wala Import duty, hii inahamasisha sana watu kununua mashine na kufungua viwanda vidogo vidogo, hima vijana tuanze kufungua viwanda, na habari njema ni kwamba kuna taasisi nyingi za kifedha zinazotoa mikopo rahisi kabisa kwa wale ambao wamedhamiria kwa dhati kabisa kuanzisha biashara. Kadharika tunayo Mifuko mbalimbali ya Maendeleo ya Jamii kutoka Serikalini inayotoa Mikopo na Ruzuku kwa makundi mbalimbali hususani vijana.

KUFUTWA KWA KODI YA ROAD LICENCE/ MOTOR VEHICLE
Kodi ya gari kutokana na matumizi ya barabara ilikuwa inakusanywa moja kwa moja na TRA kutoka kwa watumiaji wa magari, hali hii ilipelekea kuifanya kodi hii iwe inamuumiza kwa kiasi kikubwa mlipaji kutokana na ukubwa wa gharama na kodi hiyo kushindwa kubaini ni magari gani yanatumia barabara na yapi hayatumii, pia kodi hii iliifanya Serikali kupoteza mapato mengi kutokana na urahisi wa kuikwepa. Kitendo cha Serikali kuihamishia kodi hii kwenye mafuta kitaondoa maumivu ya ulipaji, kitafanya Serikali ikusanye mapato yake Stahiki na kwa kuwa itakusanywa kwa magari yanayotembea tu itaongeza uhalali kwa walengwa wote.

KUFUTWA VAT –KODI YA ONGEZEKO LA THAMANI KWA MASHINE ZA KUTOTOLESHA KUKU NA CHAKULA CHA KUKU.
Hii nayo ni nafuu kubwa kwa vijana kwa kuwa zile incubators hazitakuwa ghali tena, ilikuwa aibu kwa nchi kubwa kama Tanzania kuingiza mayai na kuku kutoka nchi jirani kwa sababu ya bei kuwa rahisi, kuondolewa kwa kodi hii kutaleta unafuu mkuwa katika kuendesha biashara ya kuku. Jambo hili litapunguza gharama kubwa za kuzalisha kuku na mayai pia, hii iwe fursa ya kuweza kuuza kuku na mayai kwenye nchi za jirani visiwani hata mbali kabisa ya maeneo yetu, iwe fursa kwetu kuongeza wigo wa ushindani wa kimataifa huku tukisaidiwa na mabalozi wetu kujua fursa mbalimbali zilizopo nje ya nchi.

KUPUNGUZWA KWA KODI YA FAIDA KWENYE SEKTA YA KUTENGENEZA MATREKTA, KUUNGANISHIA MAGARI NA BOTI ZA UVUVI
Kwa kawaida Sekta hii ilitakiwa ilipe 30% ya faida yao kama kodi, sasa kwa kuwa Serikali imeamua kunufaisha kilimo na uvuvi imeamua kwenda mbele zaidi na kupunguza kodi hii kutoka 30% mpaka 10%, kwa kufanya hivi Serikali imewapa ahueni kubwa wale wanojihusisha na uundwaji wa magari, maboti, na pia matrekta. Hii yote imefanywa ili ndoto ya kuwa na viwanda vya kutosha itimie, wawekezaji wengi wa ndani na nje hukimbilia sehemu ambazo hazina kodi kubwa kama hapa kwetu, sasa vijana yafaa kuchangamkia fursa hii kwa kuleta wawekezaji ambao watawekeza hapa na kuuza ndani na nje ya nchi yetu kutokana na unafuu mkubwa wa kodi uliopo ndani ya nchi ukilinganisha na majirani zetu.

KUFUTWA KWA KODI YA VIFAA VYA WALEMAVU. Vifaa vya watu wenye ulemavu vitapatikana kwa nafuu hivyo kuwezesha walemavu wengi kuvipata na kuwasaidia katika shughuli zao za kila siku ikiwemo utafutaji wa riziki. Pia itasaidia kupunguza utegemezi wa ndugu, jamaa na marafiki hivyo kufanya Nguvukazi ya Taifa kuwa hai katika shughuli za kimaendeleo. 

SERIKALI IMEAMUA KWA DHATI KABISA KULINDA VIWANDA VYA NDANI KWA KUFANYA YAFUATAYO;
Juisi inazotengenezwa hapa nchini imepunguziwa kodi kutoka asilimia 9.5 mpaka asilimia 9, Wine zinazotengenezwa hapa nchini zimepunguziwa kodi, Vinywaji vikali navyo vimekuwa na kodi ndogo kuliko vinavyotoka nje, Sigara zinazotengenezwa ndani zinatozwa kodi kidogo ukilinganisha za zile za nje. Kodi za mazao zimepunguzwa sana, kwa mazao ya biashara, kodi imepungua kutoka asilimia 5 mpaka asilimia 3, vile vile kodi za mazao ya chakula zimepungua kutoka asilimia 5 mpaka asilimia 2, yote hii imefanyika ili sisi vijana tukalime na tuwe washindani wakubwa wenzetu kwenye masoko ya kimataifa kwa kuwa mazao yetu yatakuwa na bei rahisi sana.

SERIKALI SIKIVU YA CHAMA CHA MAPINDUZI HAIKUISHIA HAPO BALI IMEENDELEA KUONDOA KODI KERO ZOTE KAMA IFUATAVYO;
Imeondoa TOZO zote zilizokuwa kwenye mbolea wakati wa kununua ambazo ni kama zifuatavyo, TBS- Tanzania Bureua of standards, TAEC - Tanzania Atomic Energy Commission WMA –Weight and Measures Authority. Kuondoa TOZO zote hizi kwenye mbolea kunaifanya mbolea kuwa na bei rahisi sana kiasi cha kwamba kila mkulima ataweza kumudu gharama kidogo za mbolea maaana yake atapata mazao mengi zaidi ukilinganisha na kama mbolea isingetumika kabisa, Rai ni kwa vijana kuliona hili na kulichangamkia haraka bila kupoteza wakati, kama fedha ama mtaji ni shida basi ni vyema kutumia Mifuko ya Maendeleo ya Jamii na taasisi zingine za kifedha kukopa na kuchukua hatua ya kufanya uzalishaji.

Imeondoa TOZO zote za viwango vya ubora na ukaguzi zilizokuwa zitkitozwa na TBS – Tanzania bureau of Standards kwenye mazao kama pamba, chai, korosho na kahawa. Kama ambavyo Mhe Rais aliahidi akiwa kwenye kampeni kule Bukoba kwamba watu wataenda kuuza kahawa Uganda, hakika katimiza Ahadi hizo kwa sasa tozo zote zimeondolewa, sasa kilimo kina tija tena. Hima vijana wenzetu kama tunahitaji mali basi zinapatikana mashambani.

TOZO za nyumba za kulala wageni, zile kodi za service levy kwenye guest house zimefutwa rasmi, so kwa wale wenye ndoto za kumiliki nyumba za kulala wageni hii sekta ni muhimu kwa kuwa imekuwa haina gharama tena, Rai yetu ni ile ile kwamba Serikali imeandaa mazingira mazuri kwa sisi, ni fursa ya kuchangamkia mapema ili tuweze kustawi, si vyema waje watu kutoka nje kuja kuchuma haya matunda wakati sisi tumelala na kulalamika kila uchwao.

TOZO za kupata kibali cha kuchinja wanyama zimefutwa, na tozo za kusafirisha wanyama nazo zimefutwa hii yote imefanyika ili kupunguza gharama za maisha ya sisi sote na vilevile kuhamasisha vijana kujihusisha na biashara hizi. Kwa wale ndugu zetu wenye mifugo mara nyingi wakipeleka mifugo yao kwenye minada hutozwa fedha za mnada kwa kuwepo kwenye soko husika. Sasa Mhe. Rais kafuta hii tozo kupunguza gharama zisizo na msingi na kufanya maisha yawe rahisi zaidi lakini cha zaidi ni kurahisisha ufanyaji wa hii biashara, kwa maana hiyo vijana wanahamasishwa kuingia na kufanya hii biashara.

Katika kulinda Viwanda vyetu vya ndani Mhe Rais kapandisha TOZO mbalimbali za bidhaa ambazo zinapatikana kwa wingi hapa nchini kwetu lakini bado watu wanaziagiza toka nje. Bidhaa kama za makaratasi, Sukari kwa ajili ya kulisha viwanda, Bidhaa za chuma, Bidhaa za gypsum, Mawese na bidhaa za Alminium (kaongeza kodi kwa zile za nje na kupunguza kodi kwa zile zinazozalishwa ndani).

Mgawanyo wa Bajeti yetu ni kama ifuatavyo; 61% mapato ya ndani ya kawaida, 24% mikopo ya ndani yenye riba nafuu na ya kibiashara vilevile, 13% Ni mikopo ya nje na misaada ya wahisani na 2% Hizi ni tozo kutoka Serikali za mitaa.

Tunaweza kuona ni jinsi gani tulivyopunguza utegemezi wa wahisani, sasa ni dhahiri kabisa kuwa tunaelekea sehemu nzuri zaidi ya kutotegemea misaada kabisa, kwa mfano mwaka wa fedha uliopita hatukupata fedha za kutosha kutoka kwa wahisani lakini tuliweza kuendesha Serikali vizuri na miradi mikubwa ikaendelea kama kawaida.

Jambo la kujivunia ni kwamba ukiangalia matumizi ya Bajeti hii ni kwamba takribani asilimia 62 ya matumizi ya Serikali ni kwa ajili ya Maendeleo mbalimbali ya nchi kama vile; miradi ya Barabara, Vivuko, Meli, Ndege, Maji, Umeme, Reli, na vingine vingi. Ni asilimia 38 tu ndio inaenda kwenye mtumizi ya kawaida ambayo ni pamoja na Mishahara, Posho, Vitafunwa, Safari, per diem, Stationeries na vingine vidogo vidogo.
 Hii ni hatua kubwa kuwahi kufikiwa kwa kuwa hapo miaka ya nyuma tulikuwa hatuwezi kufanya mambo ya maendeleo bila kukopa, kiasi chote tulichokuwa tukikusanya kilikuwa kinaenda kufanya matumizi ya kawaida lakini kwa sasa hali imebadilika kabisa ni vyema sasa vijana wakaona manufaa ya mabadiliko haya kwa mfano; 

Mradi Mkubwa wa Reli ya kati (Standard Gauge) unakuja na fursa nyingi sana, kuanzia mama ntilie, wasafirishaji, wenye makampuni ya ujenzi, wajenzi wa nyumba, watu wa Clearing and Forwading, mahoteli na vingine vingi sana, madereva, Mafundi. Uwepo wa Reli ya kati utawezesha usafiri wa haraka na nafuu, Mfano Samaki zinazovuliwa Mwanza zitaliwa Dar es Salaam kwa wakati zikiwa fresh, mazao ya mbogamboga kutoka kutoka Morogoro yaliyokuwa yakiozea njiani yatafika kwa wakati na kwa urahisi na Bei za bidhaa zitashuka kutokana na kushuka kwa gharama za usafirishaji. Hizi zote ni fursa zetu vijana kuzalisha mazao mbalimbali na kupata faida kubwa.
Mradi mwingine mkubwa ni ule wa bomba la kutoka Uganda mpaka Tanga. Biashara ya Mafuta ni biashara adimu na muhimu duniani kote. Mafuta ni uchumi, mafuta ni fedha. Upatikanaji wa Petrol, Mafuta ya Ndege na Diesel utasaidia kuimarisha uchumi wa nchi. Kadharika vijana wengi watapata ajira kwenye maeneo hayo na kutakuwa na uingizaji wa fedha za kigeni. Vilevile itanufaisha watu wanaojihusisha na masuala ya usafirishaji, wauza vyakula, watu wa Clearing and Forwarding, wamiliki wa Mahoteli, wenye magari ya kukodisha, malazi na vingine vingi.

Ununuzi wa ndege nyingine. Pato la Taifa litaongezeka kupitia ulipaji wa kodi, watalii wataongezeka, vijana wengi watapata ajira kwenye nafasi mbalimbali kama vile urubani, uhudumu wa ndani, uuzaji wa vyakula ndani ya ndege, uuzaji wa mafuta ya ndege. Mpaka sasa Serikali imekwisha nunua ndege mbili zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja ambapo ndege hizo zilianza kutoa huduma tangu October 2016. Huku moja nyingine inategemewa kuwasili Julai 2017, mbili zinategemewa kuwasili June 2018 na ya mwisho ambayo itakuwa ni ya masafa marefu inategemewa kuwasili Julai 2018. Kuimarisha Sekta ya Usafiri wa Anga pia kunachochea Maendeleo ya Biashara kutokana na urahisi wa kusafirisha bidhaa ndani na nje ya nchi na kuondokana na upotevu wa muda kwa wafanyabiashara. 
Ujenzi wa kiwanda kikubwa cha Chuma kule Liganga na MchuchumaNjombe. Hii ni fursa adhimu sana kwa nchi yetu vijana wakae chonjo kwa kuwa biashara ya usafirishaji, uuzaji chakula na zingine nyingi zitatokea hapa. Nchi nyingi zilizoendelea kama vile China na Ulaya hutumia madini haya kwenye viwanda vikubwa ili kupunguza gharama za uzalishaji kwenye viwanda vyao. Upatikanaji wa madini haya Tanzania utasaidia kuwa na uhakika wa uzalishaji na kuongeza ajira kwa vijana wengi kwa sababu wawekezaji wengi watavutiwa kuanzisha viwanda nchini.

Ujenzi wa LNG-PLANT, Liquified Natural Gas (Mitambo ya kusindikia Gesi kimiminika) Lindi. Gesi ni moja ya vyanzo vinavyozalisha umeme. Gesi imesaidia kurahisisha uzalishaji wa Umeme wa Grid ya Taifa ambao pia unasaidia kwa kiasi kikubwa kwenye viwanda.  kuanza kwa ujenzi wa Mradi huu kutakuwa na manufaa makubwa sana kwetu kama watanzania, Ajira nyingi zitazaliwa humu, vilevile ujenzi wa kiwanda cha mbolea inayotengenezwa kwa kutumia gesi nao utaanza, kwa hiyo wale vijana ambao ni wahandisi wakae mkao wa kula, wamiliki wa magari ya usafirishaji, wale wakulima wajiandae kupata mbolea ya bei rahisi zaidi. Taifa litajiingizia fedha za kigeni kwa kuuza gesi nje ya nchi, kadharika itarahisisha matumizi ya nyumbani yanayotokana na umeme na hatimaye kuongeza ubora wa maisha.

Kupunguza kodi kwenye Masoko ya Matunda ndani. Uzalishaji wa mazao kwa wakulima sasa utakuwa sio wa mashaka, maendeleo ya kujitegemea na kujiajiri na maendeleo ya viwanda vya ndani yatakuwa kwa kasi, itaongeza hamasa ya uzalishaji wa matunda kwa wakulima kutokana na ongezeko la soko la na pato lao hivyo kupelekea kuongezeka kwa ajira, ukuaji wa sekta ya kilimo pamoja na kuongezeka kwa pato la Taifa kadharika iatwezesha kukua kwa viwanda vinavyotengeneza Juisi. Ipo haja yetu kuongeza ubora kwenye bidhaa za ndani ili kupambana kikamilifu na ushindani mkubwa utakaoibuka. 

Usambazaji wa Umeme Vijijini kupitia Mradi wa REA.

 Kwa mujibu wa Bajeti hii mpaka sasa wateja (watanzania vijijini) 146,831 sawa na asilimia 58.7 ya lengo wameunganishwa wakati hatua za makusudi zinaendelea kwa ajili ya kuwafikia wateja wote waliolengwa. Kwanza gharama za ufikishaji wa Umeme huu majumbani ni nafuu takribani TShs 27,000 hutumika kulipia. Hii ni fursa kwetu vijana kwa sababu umeme unapunguza gharama za mafuta yaliyokuwa yakitumika kuwashia mwanga na kwenye majiko ya kupikia. Sasa kazi za ajira zitafanyika huko huko vijijini na sio kutegemea mijini, uimarishwaji wa mawasiliano kwa wafanyabiashara na uimarishaji wa biashara za vinywaji kutokana na urahisi wa kutumia friji. Ni wakati wa kuimarisha Viwanda vidogo vidogo kama vile viwanda vya uchomeleaji, wakata vyuma, Viwanda vya Useremala, Mashine ndogo za kufyatua matofali, saluni, ujenzi, usindikaji na vyakula ili kunufaika kikamilifu na fursa hii.
Urasimishwaji wa Machinga.Kutambuliwa kwa wafanyabiashara wadogowadogo kisheria kutaisaidia wao kupata haki za kisheria na faida za kibiashara kama kuweza kuongeza mitaji yao kupitia mikopo ya kati na mikubwa. Hii itapelekea kutengeneza wafanyabiashara wakubwa na wengi nchini, kupata nafasi ya kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kama NSSF, NHIF nk. Itasaidia Serikali kuongeza wigo wa mapato yatakayotokana na malipo ya Leseni ya Biashara, Ushuru wa Soko pamoja na Ushuru wa Bidhaa.

IMETOLEWA NA IDARA YA UHAMASISHAJI NA CHIPUKIZI
UMOJA WA VIJANA WA CHAMA CHA MAPINDUZI
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com