WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba amewaondoa hofu
wabunge akisisitiza kuwa, sekta ya kilimo inatapata pesa za kutosha kwa
kuwa, Wizara yake inapata fedha nyingi kuliko nyingine yoyote kutokana
na fungu kutoka serikalini na mchango mkubwa kutoka kwa wafadhili.
Alisema hayo jana wakati akijibu hoja za wabunge takribani 136
waliochangia katika mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi
ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2017/18 iliyowasilishwa
bungeni Ijumaa iliyopita.
“Niwaombe wabunge tusipate wasiwasi kwamba kilimo kina bajeti ndogo.
Hiki ni moja ya kipaumbele, bila kilimo, viwanda itakuwa ngumu
kufanikisha ni kweli kabisa. Israel kipaumbele chao ni usalama, lakini
bajeti yao ya ulinzi pamoja na kwamba ni kipaumbele wanapata msaada
kutoka Marekani.
Mwaka jana wamepata msaada wa Dola za Marekani bilioni 38 wakati
kwenye bajeti ya ndani walitenga Dola za Marekani bilioni 4.6.”
Akaongeza, “...Hata sisi wakati tunaweka bajeti tunaangalia wenzetu
wanaotuunga mkono wanatupa kiasi gani ili tufanye mgawanyo sahihi wa
mahitaji ya ndani.”
Katika michango yao, wabunge wengi walionesha wasiwasi kutokana na
bajeti ya wizara hiyo kuendelea kushuka mwaka hadi mwaka huku kiasi cha
fedha za maendeleo kwa mwaka wa fedha 2016/17 kikitolewa kwa asilimia
tatu jambo lililowafanya wahoji kuhusu kipaumbele cha serikali dhidi ya
kilimo.
Pamoja na hayo pia baadhi ya wabunge walibeza kitendo cha serikali
kufuta kodi 108 katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi na kusisitiza
kuwa kodi zilizofutwa hazimnufaishi mkulima, bali mtu wa kati na
mfanyabiashara.
Akihitimisha hoja yake, Waziri Tizeba alisema bajeti ya sekta ya
kilimo si yote iliyoko kwenye wizara yake ya Kilimo kwani ipo pia kwenye
maeneo ya nje ya wizara hiyo kama vile Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ambako huko ndiko kwenye utekelezaji wa
shughuli za kilimo na kwenye halmashauri.
“Wizara inajihusisha zaidi na sera na miongozo ya kitaifa, lakini
kule kwenye mzizi kunashughulikiwa na Tamisemi. Pia Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, nao wanafanyakazi zinazohusu kilimo ingawa si
moja kwa moja,” alieleza Dk Tizeba.
Alisema kwa uchache taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Kilimo
zinakusanya maduhuli na kutumia katika sekta ya kilimo jumla ya Sh
bilioni 260 ambapo pia alibainisha kuwepo kwa taasisi nyingi za wabia wa
maendeleo wanaochangia kwenye kilimo, lakini si katika mfumo wa
serikali.
“Mfano mwaka jana 2015/16, kwa jumla wadau wa maendeleo walichangia
shilingi trilioni 1.73 katika kilimo moja kwa moja wakati bajeti ya
serikali kwa jumla ilikuwa trilioni 1.01. ukijumlisha ni karibia
trilioni 2.7 ni fedha nyingi kuliko wizara nyingine,” alifafanua.
Alieleza kuwa hadi sasa fedha kwenye kilimo ni nyingi katika mwaka
huu wa fedha wa 2016/17 kwani hadi bado wafadhili wanaendelea kujitolea
fedha katika kilimo ambapo takribani Sh bilioni 400 zimeingizwa kwenye
kilimo kupitia miradi mbalimbali.
Akizungumzia tozo zilizofutwa, alisema amesikitishwa kuona kuwa
pamoja na jitihada za serikali kuchukua hatua dhidi ya kero zilizokuwa
zikiwasumbua wananchi katika tozo na kodi mbalimbali, bado kuna wabunge
wanaobeza hatua hiyo.
Alisisitiza kuwa, utitiri wa kodi na tozo zilizofutwa katika sekta za
kilimo, mifugo na uvuvi, ulizingatia mnyororo wa thamani na namna
zinavyomuathiri mtu mmoja, hivyo maamuzi ya kuziondoa yatanufaisha watu
wote.
Wednesday, May 24, 2017
KARIBU TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA
Popular Posts
-
Katibu Mkuu wa Wizara ya kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma Katibu Mkuu wa Wizara ya kilim...
-
📌 Asema Rais, Dkt. Samia anafanya kazi kubwa ya kuwaunganisha Watanzaia 📌 Atak...
-
Timu ya Sevilla FC leo wamefanya mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Timu ya...
-
Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango akiapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamis Juma kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungan...
-
Edson Kamukara enzi za uhai wake Anaandika Mathias Canal, Iringa "Mwandishi wa habari, Edson Kamukara amefariki dunia jana j...
Powered by Blogger.
0 comments:
Post a Comment