Ugonjwa mtoto aliyeishi kwa kunywa mafuta wabainika
HATIMAYE Hospitali ya Taifa Muhimbili imebaini mtoto Shukuru Kisonga (16) aliyeishi kwa kula sukari na kunywa maziwa na mafuta ya chakula, anasumbuliwa na ugonjwa wa selimundu maarufu kwa jina la sickle cell.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu na Mkuu wa Kitengo hicho katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Stella Rwezaura alisema kwa miaka yote hiyo mtoto huyo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa huo ambao ni wa kurithi kutoka kwa wazazi wake.
Mei 16 mwaka huu Shukuru alilazwa na kufanyiwa vipimo mbalimbali vya damu katika hospitali hiyo na kubainika kuwa ana tatizo la selimundu. “Ni ugonjwa ambao amezaliwa nao, au alikuwa na vinasaba kutoka kwa wazazi wake.
Ugonjwa huu unashambulia chembechembe nyekundu za damu na kusababisha pia kuharibika chembe hizo baada ya kutengenezwa,” alisema Dk Stella. Alisema tatizo hilo linasababisha mgonjwa kupungukiwa damu mara kwa mara na pia, kubadilika rangi kama ilivyokuwa kwa Shukuru lakini kwa sababu hakuwahi kupimwa na kubainika kuwa na ugonjwa huo, hakujua kama ni selimundu iliyokuwa ikimsumbua.
Mama yake Shukuru, Mwanabibi Mtenje alisema tiba aliyokuwa akimpa yaani ya kumnywesha maziwa lita moja kila siku, sukari pamoja na mafuta ya chakula alielekezwa na mganga Msumbiji wakati akihangaika ili mtoto wake apone.
“Nilihangaika sana na mtoto huyu, nilienda sehemu mbalimbali, Malawi, Msumbiji ambapo walinielekeza niwe namnywesha vitu hivyo ili mwili ulainike, “ alisema mama huyo. Alisema kuwa aliuza ng’ombe 10 aliokuwa nao kupata fedha za kumtibu mtoto wake, lakini sasa anaishukuru Hospitali ya Muhimbili kwa kubaini tatizo na tiba ya Shukuru.
Akizungumzia mtoto huyo kunywa mafuta ya kula, sukari na maziwa alisema, katika vipimo alivyopimwa Shukuru alikutwa pia na upungufu wa madini ya chuma ambayo mtu akikosa madini hayo mwili unamlazimisha kuyatafuta katika vitu vya ajabu.
“Ndio maana unakuta mtu mwingine au mama wajawazito wanakuwa na upungufu wa madini haya wanakula sana udongo, mchele au vitu vya ajabu, kwa Shukuru kwa sababu alikuwa na upungufu wa madini haya ikamsaidia,” alisema
0 comments:
Post a Comment