METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, September 10, 2017

SHAKA AFANYA MAZUNGUMZO NA MZEE MALECELA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Kaimu Katibu Mkuu UVCCM Taifa amemtembelea na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu na makamu wa kwanza wa Rais wa zamani, Mzee John Malecela ambapo alimpongeza kutokana na mchango wake wa kutumikia Taifa kwa uaminifu na utendaji uliotukuka uliopelekea kuliletea Taifa maendeleo  ikiwa ni pamoja na kupigania uhuru.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Nyumbani kwake Mtaa wa Kilimani Mjini Dodoma Shaka alimpongeza Mzee Malecela kwa matendo ya mfano wa kuigwa katika Utumishi wake pindi akiwa Mtumishi wa umma Jambo lililochagiza pia Taifa kuwa na Mshikamano na amani iliyopo kwa ushirikiano mkubwa na Rais wa awamu ya kwanza Hayati Mwl Julius Kambarage Myerere.

Alisema kuwa upendo uliopo nchini baina ya wananchi wote ni tunu ya uwajibikaji mzuri uliofanywa na Wazee wetu hivyo Taifa linapaswa kuendelea kuunga mkono uzalendo ili kutokuwa na matabaka ya utengano wa kidini, kisiasa na ukabila.

Shaka alisema Malecela ni mfano wa viongozi bora ambao wametoa mchango katika uongozi wa nchi huku akimuhakikishia kuwa Jumuiya ya vijana inaendelea kuimarika na kuzitambua mbinu zaidi za ushindi na kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi.

Kwa upande wake Mzee John Malecela alimpongeza kaimu katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana kwa kufika nyumbani kwake kumsalimu huku akimsisitiza kuendeleza ujenzi wa Jumuiya ya Vijana kwani ndio msingi imara wa ushindi wa Chama Cha Mapinduzi.

Mzee Malecela alisema kuwa Jumuiya ya Vijana kwa sasa inazidi kuimarika kupitia uongozi wa Shaka Hamdu Shaka huku akisema kuwa anapaswa kuwa na misimamo mikali kwani ndio msingi na uimara wa chama na watendaji ndio nguzo katika maamuzi.

Alisema Laimu Katibu Mkuu huuo wa Umoja wa Vijana anafanya mambo makubwa katika jumuiya hiyo ambayo matokeo yake hayawezi kuonekana haraka kwani anajenga misingi mikubwa ya ushindi wa CCM ambayo matokeo yake ni kwa muda mrefu.

Aliongeza kuwa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi ndio tanuru la kupika viongozi ambapo alitolea mfano wa Rais Mtaafu wa Serikali ya awamu ya nne Mhe Dkt Jakaya Mrisho Kikwete ambaye amekuwa kiongozi mkubwa nchini aliyetokana na UVCCM.

Aidha, Mzee Malecela alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli kwani amerejesha Uadilifu, Uaminifu, Uchapakazi, kupiga Vita dhidi ya Rushwa, kupiga Vita dhidi ya ubadhilifu wa mali za chama na mali za Umma, pamoja na Unyenyekevu na kusikiliza watu.

Alisema uwajibikaji na uzalendo ulioonyeshwa na Rais Magufuli katika kipindi kifupi Cha utawala wake ni matokeo mazuri ya utekelezaji wa Azimio la Arusha analolifanya kwa vitendo kwa kurejesha heshima na nidhu ya Nchi japo zipo changamoto za kutoelewana baina ya wananchi na hizo zinatokana na matabaka yaliyopo baina ya walio na wasionacho.

MWISHO

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com