METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, May 29, 2017

TFF wadaiwa kuwatelekeza Serengeti


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limekiri kudaiwa na shule ya Alliance, ambako wanasoma na kucheza soka watoto watakaounda timu ya taifa ya wachezaji wenye umri chini ya miaka 17 watakaoshiriki Afcon 2019.

Mashindano ya Mataifa ya Afrika (Afcon 2019) yatafanyika nchini na tayari TFF imeanza maandalizi kwa kuwaweka kambini wachezaji hao watakaochukua nafasi ya Serengeti Boys ya sasa.

Serengeti Boys ya sasa ilishiriki mashindano ya Mataifa ya Afrika nchini Gabon, ambako ilitolewa katika hatua ya makundi, nafasi yao itachukuliwa na wenzao hao wanaosoma Mwanza.

Msemaji wa TFF, Alfred Lucas alikiri jana kuwa wanadaiwa na Alliance, lakini alisisitiza kuwa walikuwa na majukumu makubwa ya kuisimamia Serengeti nchini Gabon, ambapo alimtaka Mkurugenzi wa Alliance, James Bwire kuwa mvumilivu na mzalendo.

Alisema anamshangaa Bwire kwa kulipeleka suala hilo katika vyombo vya habari wakati alitakiwa kwanza kuwasiliana na TFF. Alisema kuwa wanafunzi wale wako pale (Alliance) kwa makubaliano maalumu, ambapo alimtaka mwandishi wetu kumtafuta Rais wa TFF, Jamal Malinzi kuzungumzia mkataba.

Mkurugenzi wa Alliance, James Bwire alisema hivi karibuni kuwa, TFF imekuwa ikipiga chenga kuingia mkataba na shule yake, baada ya kuahidi kutoa vifaa vya michezo kama mipira,koni,jezi na vingine.

Alisema mbali na kutotoa vifaa hivyo kama walivyoahidi, TFF pia wamekuwa wazito kulipa ada ya wanafunzi 12, ambao wanawagharimia wakati wengine 10 wanalipiwa na shule hiyo.

Bwire ambaye pia ni Meya wa Jiji la Mwanza alisema kuwa, TFF Desemba mwaka jana walifika shuleni hapo na kuahidi kusaini mkataba Januari mwaka huu, lakini hawajafanya hivyo.

Alisema kuwa TFF ni sawa kama wamewatelekeza watoto hao na kuliacha jukumu la kuwagharimia kuwa chini ya Alliance wakati makubaliano hayakuwa hivyo. Aliongeza kusema kuwa baada ya yeye kuilalamikia sana TFF, uongozi wa taasisi hiyo ulitishia kuwaondoa watoto hao katika shule hiyo, wengi wao wakiwa darasa la saba. Pia Bwire alisema TFF pamoja na kuahidi kupeleka kocha kwa ajili ya kuwafundisha watoto hao, lakini hadi sasa haijafanya hivyo.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com